Papa Francis aomba msamaha | Masuala ya Jamii | DW | 14.10.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Papa Francis aomba msamaha

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Francis, ameuomba umma msamaha kwa niaba ya Kanisa kutokana na kashfa za miaka ya hivi karibuni zilizolikumba Kanisa hilo.

Papa Francis

Papa Francis

Papa Francis ameuomba msamaha huo alipokuwa akizungumza leo mchana wakati akiwahubiria maelfu ya watu waliokusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Peter, mjini Vatican, katika utaratibu wake wa kila juma.

''Kabla ya kuanza kwa Katekesi, nataka kwa niaba ya Kanisa, kuomba msamaha kwa kashfa ambazo hivi karibuni zimeikumba Roma na Vatican. Naomba msamaha wenu,'' alisema Papa Francis.

Msamaha huo ameuomba katika kipindi ambacho Kanisa Katoliki limejikuta kwenye kashfa kadhaa, ikiwemo ile ya kujitokeza hadharani kwa Padri shoga anayepinga msimamo wa kanisa kuhusu mapenzi ya jinsia moja na kauli dhidi ya Meya wa Roma, aliyejiuzulu wiki iliyopita.

Papa Francis ameomba radhi wakati anaongoza mkutano wa wiki tatu wa baraza la makardinali na maaskofu kujadili namna ya kupitia mafundisho ya kanisa hilo pamoja na kuhusu masuala ya familia.

Makardinali na Maaskofu wakiwa katika Sinodi

Makardinali na Maaskofu wakiwa katika Sinodi

Hata hivyo, Papa hakutaja hasa aina ya kashfa anayoizungumzia wala kutoa mifano. Siku moja kabla ya kuanza kwa mkutano huo kuhusu masuala ya familia, padri wa Poland alitangaza hadharani kuwa yeye ni shoga, huku mpenzi wake akiwa pembeni yake. Padri huyo aliyefanya kazi yake Vatican kwa miaka 17, alifukuzwa kazi yake ya ukasisi.

Kashfa zaongozana

Kashfa hiyo ilifuatiwa na ile ya kujiuzulu kwa Meya wa Roma, Ignazio Marino, kutokana na kashfa ya kuwaandalia karamu marafiki na familia yake kwa kutumia fedha za jiji. Papa na Kanisa walisema kuwa hawana imani na uwezo wa meya huyo katika kuwashughulikia mamilioni ya mahujaji wakati wa 'Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu', utakaoanza mwezi Disemba mwaka huu.

Aidha, katika kashfa nyingine, barua yenye utata iliyovuja ambayo ilionyesha kwamba makardinali kadhaa wahafidhina wamekosoa namna Sinodi hiyo inavyoendeshwa na kuhoji kuhusu maafikiano yoyote yaliyofikiwa kuhusu ndoa katika Kanisa.

Aliyekuwa Meya wa Roma, Ignazio Marino

Aliyekuwa Meya wa Roma, Ignazio Marino

Hata hivyo, msemaji wa Vatican, Padri Federico Lombardi, ameshutumu vikali kuhusu barua hiyo iliyoandikwa kwa Papa, lakini aliwakumbusha wahusika kwamba utaratibu wa mkutano unaandaliwa na kazi yao ni kufuata utaratibu huo.

Papa Francis ambaye alichaguliwa Machi mwaka 2013, wakati Kanisa Katoliki linakabiliwa na kashfa, ikiwemo ile ya mapadri kuwanyanyasa watoto kingono, leo pia amekutana na ujumbe wa wachimbaji madini 30 wa Chile, ambao walikwama kwenye mgodi kwa siku 70, miaka mitano iliyopita.

Papa aliwashukuru kutokana na imani waliyonayo kwa Mungu na alisema anajua kila mmoja atakuwa na uwezo wa kuelezea maana ya matumaini.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE, APE, DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com