Mjadala Vatican juu ya mageuzi ndani ya kanisa Katoliki | Masuala ya Jamii | DW | 05.10.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Mjadala Vatican juu ya mageuzi ndani ya kanisa Katoliki

Takribani makadinali na viongozi wengine wa kanisa Katoliki duniani wanaokutana mjini Vatican wamekuwa na mjadala jinsi gani kanisa linavyoweza kuregeza msimamo juu ya huduma ya sakramenti kwa baadhi ya waumini .

Makadinali na maasikofu wa kanisa Katoliki mjini Vatican.

Makadinali na maasikofu wa kanisa Katoliki mjini Vatican.

Mkutano huo ambao unatarajiwa kumalizika Oktoba 25 mwaka huu na unaojulikana kama Synodi ulioanza jumamosi kwa misa katika kanisa la mtakatifu Peter haulengi kubadilisha kanuni au mafundisho ama kanuni za kanisa hilo bali kuangalia jinsi gani mafundisho yanayotolewa yanaweza yakaendana na mazingira ya sasa ya kimaisha duniani.

Suala kubwa katika mjadala huo ni juu ya msimamo wa muda mrefu unaozuia watu waliowahi kuachika katika ndoa na kufunga ndoa tena kushiriki katika huduma ya sakramenti unavyoweza kubadilishwa na kuwaruhusu watu wa aina hiyo kushiriki tena huduma hiyo.

Makadinali ndani ya kanisa hilo tayari wameonya ya kuwa kanisa katoliki linaweza likatumbukia katika mfarakano mkubwa kuhusiana na utata uliopo katika suala hilo.

Mahusiano ya jinsia moja yaibua mjadala

Suala linalohusiana na mapenzi ya jinsia moja pia ni jambo lingine linaloibua mjadala ndani ya kanisa hilo. Kauli iliyotolewa hapo juzi na mmoja wa wanathiolojia wa kanisa hilo kupitia gazeti moja la nchini Italia ya kuwa ni shoga na amekuwa akiishi na mwanaume mwingine iliibua pia maswali mengi miongoni mwa waumini na viongozi wa kanisa hilo.

Mwanathiolojia huyo Monsignor Krystof Charasma ambaye ni raia wa Poland alivuliwa nyadhifa zake zote ndani ya kanisa hilo mara tu baada ya kukiri hadharani kuhusiana na tabia yake hiyo ya kimaisha.

Msemaji wa kanisa hilo mjini Vatican Padri Federico Lombard alisema kitendo hicho kinatia doa kanisa hilo na kusababisha kanisa hilo kuwa katika mijadala isiyotarajiwa ya vyombo katika vyombo vya habari.

Akifungua mkutano huo utakafanyika kwa muda wa wiki tatu kiongozi mkuu wa kanisa hilo duniani Papa Francis alitetea juu ya umuhimu wa kulindwa kwa ndoa kati ya mume na mke na kulitaka kanisa hilo kuwa makini na kutoongozwa na ushabiki wa hoja ambazo zinaweza zikavuruga misingi ya kanisa hilo.

Aidha Papa Francis alilitaka kanisa hilo kuwatendea haki watu walio na majeraha ya kisaikolojia miyoni mwao na kuonya kuwa hali ya kuwatenga watu hao badala ya kuwasikiliza matatizo yao inaonekana kwenda kinyume cha misingi ya kanisa hilo.

Masuala mengine yanayohusiana na jamii ambayo pia inaundwa na waumini wa kanisa hilo ambayo Papa Francis amependekeza yapewe nafasi katika mjadala huo ni pamoja na masuala ya ukosefu wa ajira, mazingira pamoja na vita.

Mwandishi: Isaac Gamba/ AFPE/DPAE

Mhariri:Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com