Pambano la kusaka dhahabu
Gramu bilioni moja za dhahabu: Tanzania ina hazina yenye thamani ya mabilioni. Kijiji cha Kewanja mkoani Mara kinataka kufaidika na hazina hiyo. Watu wanahatarisha maisha yao kwa ajili ya gramu chache tu za dhahabu.
Hazina
Gramu milioni 10.8 za dhahabu zinapatikana kwenye migodi iliyopo kaskazini mwa mkoa wa Mara, kaskazini magharibi mwa Tanzania. Mgodi huu ni mmoja kati ya sita nchini kote. Tangu mwaka 2006 mgodi huu unaendeshwa na African Barrick Gold, kampuni iliyo sehemu ya Barrick Gold ikiwa ni kampuni inayoongoza kwa uchimbaji wa dhahabu duniani.
Mgodi
Moja ya machimbo matatu katika mgodi uliopo Mara ya kaskazini unaitwa “Gokona”. Kila siku miamba hulipuliwa hapa ili kuifikia dhahabu. Kwa kila tani moja ya miamba zinapatikana kati ya gramu nne na tano za dhahabu. Hata hivyo, dhahabu itakuwa imekwisha kabisa ndani ya miaka kumi ijayo.
Tumaini la ajira
Mgodi unaomilikiwa na African Barrick Gold ni miongoni mwa ile inayotoa ajira kwa watu wengi kabisa katika mkoa wa Mara. Zaidi ya watu 2,000 wameajiriwa moja kwa moja au na mashirika yanayofanya kazi kwa ajili ya Barrick Gold. Licha ya hayo, sehemu kubwa ya wakaazi wa mkoa huu hawana ajira.
Ulinzi
Waya wa seng’enge umezungushwa katika eneo la mgodi kuzuia wezi. Hata hivyo, wezi hao wanafanikiwa kuukata waya huo na kupata upenyo. Kwa sababu hiyo kampuni imeamua kuongeza walinzi binafsi na hata kuleta polisi. Pamekuwepo mapambano yaliyosababisha baadhi ya watu kuuwawa na wengine kujeruhiwa.
Wavamizi
Mara nyingi wanakuja kwa makundi ya mamia ya watu. Wanalivamia eneo la mgodi asubuhi, mchana na jioni wakitafuta mawe yenye japo kiasi kidogo cha dhahabu. Wakipata mawe hayo wanaweza kuwauzia walanguzi.
Wachimba dhahabu
Tunachukua tu kile kinachobaki,” anasema Jumanne. “Lakini polisi wanatufukuza na wakati mwingine kutufuata hadi vijijini kwetu.” Jumanne ni mmoja tu ya wavamizi wengi wa eneo la mgodi wanaotaka kampuni iwaachie wanakijiji mavumbi ya mawe ili nao wafaidike.
Mwoshaji
Mchanganyiko wa mawemawe na vumbi unaoshwa na wavamizi ili kuangalia kama kuna walau chembe za dhahabu. Kazi hii ngumu hufanywa hasa na wanawake. Wanatumia masaa mengi kutafuta dhahabu katika tope lakini mara nyingi hawaambulii chochote. Mwanamke kama huyu analipwa shillingi 20,000 tu za kitanzania kwa mwezi.
Eneo lililosahaulika
Eneo la kaskazini la Mkoa wa Mara ni miongoni mwa maeneo yenye maendeleo duni kabisa Tanzania. Watu wengi wanaoishi katika vijiji saba vinavyouzunguka mgodi wamewahi kufanya kazi ya kuchimba dhahabu. Lakini mambo yalibadilika katikati ya miaka ya 1990, makampuni ya kimataifa yalipowasili. Shughuli za ufugaji na kilimo haziwaingizii raia kipato cha kutosha.
Waliovunjwa matumaini
"Mgodi hauna faida yoyote kwetu," wanasema wanakijiji wa Kewanja. Hawana huduma ya maji wala umeme. Zaidi ya wanafamilia 20 wanategemea shilingi 300,000 za kitanzania kwa mwezi.
Mwana aliyepotea
"Mgodi umenipora kila nilichokuwa namiliki," anasema Gati Marembera Mwita. Tarehe 6 Novemba 2012 askari polisi mmoja alimuua kwa risasi mwanae wa kiume. Vyombo vya habari vinaeleza kwamba tukio hilo lilitokea baada ya mamia ya wavamizi kuingia katika eneo la mgodi. "Mwanangu hakuwa mmoja wao," anasema baba huyo. "Alikuwa akichunga mbuzi na kondoo karibu na eneo la tukio."
Unyonyaji
Mawe – vumbi – dhahabu. Wanakijiji wamebobea katika hatua mbalimbali za uzalishaji. Zote ni za hatari. Mwishoni vumbi lenye dhahabu huchanganywa na madini ya zebaki (mercury) yenye sumu kali ili kuunganisha chembechembe za dhahabu. Thamani ya granu moja ya dhahabu ni takriban shillingi 42,000 za kitanzania. Mwandishi: Julian Hahn/ Elizabeth Shoo