Ouattara akabiliwa na kazi ngumu | Matukio ya Afrika | DW | 13.04.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Ouattara akabiliwa na kazi ngumu

Licha ya kushika madaraka baada ya kumshinda Laurent Gbagbo kisandukuni na vitani, Rais Alassane Ouattara ana kibarua kizito cha sio tu kuijenga upya nchi yake, bali pia kuvuna imani ya wafuasi wa Gbagbo.

Laurent Gbagbo, kushoto, na Alassane Ouattara, wakati wa uchaguzi wa Novemba 2010

Laurent Gbagbo, kushoto, na Alassane Ouattara, wakati wa uchaguzi wa Novemba 2010

Alassane Ouattara anajua kwamba amesimamiwa na jukumu kubwa mbele yake. Karibu nusu ya wapiga kura wa Cote d'Ivoire miezi mitano iliyopita hawakumchagua yeye kuwa kiongozi wao, licha ya kuwa jamii ya kimataifa imekuwa ikitambua urais wake. Hawa waliweka ufuasi nyuma ya hasimu wake, Laurent Gbagbo, na kwa hakika walikuwa dhidi yake.

Miezi kadhaa baada ya uchaguzi huo, ikashuhudia nguvu za nchi zikiporomoka na raia wakigawanyika tena. Sasa Ouattara anapigana vita vipya, si vya kutafuta ushindi kwa njia ya silaha, lakini vya kutafuta suluhu na maridhiano.

Tayari ameunda tume ya kuchunguza matokeo ya vurugu na mauaji ya maangamizi, lakini hata jambo hili nalo linawafanya wale wanaojijuwa kuwa walishiriki kwenye mambo hayo, kujiweka katika hali ya tahadhari na kujihami.

"Gbagbo lazima awe hai"

Laurent Koudou Gbagbo

Laurent Koudou Gbagbo

Na bado kuna jengine. Kuanzia sasa, maisha na hatima ya hasimu wake, Gbagbo, imo mikononi mwake. Lazima ahakikishe kuwa Gbagbo hafi, maana akija akifariki hivi sasa, Cote d'Ivoire huenda ikazama kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe, maana wafuasi wake watamchukulia kuwa amekufa shahidi mikononi mwa adui.

"Bwana Gbagbo lazima abakie hai. Yuko hali na hatakiwi kupatwa na jambo lolote lile baya. Hatakiwi atokewe na bahati mbaya yoyote wakimo mikononi mwa maadui zake. Lazima abakie hai na hilo ni jukumu la wale wale ambao alikuwa akipigana nao vita." Anasema Rinaldo Depagne wa International Crisis Group.

Ouattara peke yake hawezi kuiunganisha nchi

Baadhi ya wafuasi wa Gbagbo wakiwa wameshikiliwa na wanajeshi wa Ouattara

Baadhi ya wafuasi wa Gbagbo wakiwa wameshikiliwa na wanajeshi wa Ouattara

Vile vile, wataalamu wengine wanaona kuwa si jambo rahisi kwa Rais Ouattara peke yake, kuanzisha mchakato wa amani na maridhiano katika nchi hii iliyogawika; na ni muhimu kwa serikali ya Ouattara kuzijumuisha pande zote mbili zinazozozana.

"Ikiwa mshindi si mtu wa vita na ana nia ya kujenga jamii yenye amani na maridhiano, lazima mgogoro huu auzike kabisa. Na hilo linatawezekana kwa kila mmoja kumshirikisha kwenye madaraka. Kwa hivyo ni lazima pawe na serikali ya umoja wa kitaifa. Na ni muhimu zaidi kwa tume ya ukweli, haki na maridhiano kuundwa. Hali ya baada ya mgogoro huu na baada ya uchaguzi ilimuhusu kila mtu, kwa hivyo lazima wananchi wote wa Cote d'Ivoire waridhiane." Anasema Alioune Tine wa Jumuiya ya Haki za Binaadamu ya Senegal, RADDHO.

Katika uchaguzi uliosababisha mgogoro huu, Gbagbo alipata asimilia 46, kiwango ambacho hakiwezi kudharaulika.

Hili likizingatiwa na ukweli kwamba chama chake cha FPI kina historia refu ya kufanya siasa za mafanikio kwenye upinzani na kwenye serikali, ni wazi kuwa nafasi ya Gbagbo bado ni kubwa.

Kitakachomsibu Gbagbo kitajuilikana katika siku za karibuni. Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu imekuwa ikikusanya vielelezo vya ushahidi na inatarajiwa kuamua hatima ya kiongozi huyu wa zamani. Rais Ouattara naye ameagiza kuanza kwa mchakato wa kisheria wa kumshitaki na pia kutafuta suluhu ya mgogoro.

Ama iwe kwa kiwango cha kimataifa au cha kitaifa, kwa mtaalamu wa masuala ya haki za binaadamu, Alioune Tine ni wazi kuwa Gbagbo lazima afikishwe mbele ya mahakama.

"Gbagbo lazima apande kizimbani ili awajibike kwa matendo yake. Kwa sababu yeye alikuwa sehemu ya maafa haya. Ili hali kama hii isijitokeze tena si kwa Cote d'Ivoire tu, bali kwa nchi nyengine pia. Kesi dhidi ya Gbagbo ni kesi kwa ajili ya demokrasia barani Afrika."

Mwandishi: Dirk Köppe/ZPR
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohammed Abdulrahman

DW inapendekeza