1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Operesheni ya kuikomboa miji ya Mosul na Raqqa

Zainab Aziz
8 Novemba 2016

Wapiganaji wa Kikurdi wameshambulia mji unaoshikiliwa na IS Kaskazini Mashariki mwa Mosul. Majeshi ya Irak yanapambana dhidi ya vikundi vya Jihad, Operesheni kama hiyo inafanyika pia Syria kuukomboa mji wa Raqqa.

https://p.dw.com/p/2SKFz
Irak Kampf um Mossul gegen den IS
Picha: Getty Images/A. Al-Rubaye

Mapambano dhidi ya kundi la IS yameingia katika wiki ya nne sasa kwenye juhudi zinazoungwa mkono na majeshi ya kimataifa kwa ajili ya kilidhoofisha kabisa kundi la IS katika nchi za Irak na Syria.  Lengo la mapambano hayo ni kuukomboa mji wa Raqqa huko nchini Syria ambao ndio ngome kuu ya wapigananji wanaojiita Dola la Kiislamu IS na mji wa Mosul wa nchini Irak.

Kikosi kinachoungwa mkono na Marekani kinachowajumuisha wapiganaji wa Kikurdi na wa Kiarabu kimesonga mbele na kufikia karibu na mji wa Raqqa.  Kikosi hicho cha Kikurdi kutoka nchini Syria SDF kimetoa taarifa kuwa wapiganaji wake wamefanikiwa kusonga mbele kuelekea kusini mwa mji wa Raqqa ijapokuwa kinakabiliana na upinzani mkali kutoka kwa wapiganaji wa ISIS.

Kwingineko wanajeshi wa Irak wameuteka mji wa Hamam al Alil ulio kusini mwa mji wa Mosul baada ya kufanikiwa kuwatimua wapiganaji wa ISIS wakati huo huo mjini Baghdad wapelelezi wanachunguza kaburi la halaiki lililogunduliwa siku moja kabla ya vikosi vya kijeshi vya Irak kuendelea kusonga mbele katika hatua ya kuukaribia mji wa Mosul.  

Miji ya Raqqa na Mosul ndio miji  mikubwa ya mwisho katika nchi za Syria na Irak ambayo bado inashikiliwa na makundi ya wapiganaji wa Jihad na kukombolewa kwa miji hiyo kutalidhoofisha zaidi kundi la wapiganaji wa IS  waliyoiteka tangu mwaka 2014.

Kundi la ISIS taabani

Majeshi washirika  yanayoongozwa na Marekani yalianzisha mapambano dhidi ya IS tangu miaka miwili iliyopita yanaendelea kutoa ushirikiano kwa kutumia ndege za kivita pamoja na vikosi maalum vya kutoa ushauri kuhusu mashambulio ya nchi kavu.

Msemaji wa kikosi cha Kikurdi kinachoungwa mkono na Marekani bibi Jihan Sheikh Ahmed ameeleza kwamba vikosi vya muungano wa wapiganaji wa Kikurdi na Kiarabu vimesonga mbele kilomita 10 katika eneo la kusini kuelekea miji ya Ain Issa na Suluk na kwamba wapiganaji wake wako takriban kilomita 30 kuweza kuufikia  mji wa Raqqa. kwa mujibu wa bibi Ahmed wapiganani wa SDF wameviteka vijiji 10 hadi kufikia sasa na mapambano yanaendelea kama yalivyopangwa.

Syrien PK SDF Strum auf Rakka
Kikosi cha wanajeshi wa SDFPicha: Getty Images/AFP/D. Souleiman

Hata hivyo kamanda wa SDFameeleza kuwa wapiganaji wa kundi la ISIS wanaendeleza mbinu yao ya kuwatumia wapiganaji wa kujitoa muhanga ambao wanatumia magari yaliyojazwa mabomu dhidi ya wapiganaji wa kikosi chake chenye takriban askari 30,000. Maafisa wa SDF wamesema kuwa mapambano hayo huenda yakachukua muda mrefu.

Hatua ya kulizingira kundi la IS kutoka pande zote ndio inayoaminiwa kuwa itafaulu kulimaliza kundi hilo, takriban wataalamu wa kijeshi 50 wa Marekani wanahusika katika operesheni ya kuukomboa mji wa Raqqa huko nchini Syria na wanahusika zaidi katika kutoa ushauri.

Makundi ya kutoa misaada ya kibinadamu yametahadharishajuu ya hatari ya kutumiwa raia na kundim la IS kama ngao au ukuta wa kujikinga katika miji ya Raqqa na Mosul.  takriban watu 34,000 wamepoteza makao yao katika mji wa Mosul tangu operesheni dhidi ya kundi la ISIS ilipoanza tarehe 17 mwezi Oktoba.

Mji wa Mosul una takriban watu millioni moja huku mji wa Raqqa ukiwa na watu 240,000 ambapo inaaminiwa huenda watu elfu 80 wamekimbilia katika mji huo kutoka katika miji mingine ya nchini Syria. 

Mwandishi:  Zainab Aziz/AFPE/RTRE

Mhariri: Daniel Gakuba