1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama azuru Palestina

21 Machi 2013

Rais Barack Obama amewasili mjini Ramallah, kufanya mazungumzo na kiongozi wa Palestina Mahmoud Abbas. Ziara yake inafanyika kukiwa na hali ya kukataa tamaa miongoni mwa wapalestina juu ya hatima ya uhuru wa taifa lao.

https://p.dw.com/p/181Ai
Obama akutana na Mahmoud Abbas kwa mazungumzo
Obama akutana na Mahmoud Abbas kwa mazungumzoPicha: Reuters

Ziara ya rais Barack Obama katika ardhi ya wapalestina imekaribishwa kwa maroketi yaliyovurumishwa kutoka ukanda wa Gaza, mawili yakianguka ndani ya Israel, bila kujeruhi mtu yeyote. Mashambulizi hayo ni ishara ya mapokezi anayotegemea kuyapata rais Obama, ambaye analaumiwa na wapalestina wengi kuiruhusu Israel kufanya inavyotaka na kuikwamisha ndoto ya kuwa na taifa lao huru.

Kwenye siku yake ya pili ya ziara yake Mashariki ya Kati, Obama amekutana na kiongozi wa wapalestina Mahmoud Abbas mjini Ramallah, na baadaye atarejea mjini Jerusalem ambako atatoa hotuba mbele ya hadhara ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya Israel ambao wamechaguliwa kwa umakini mkubwa.

Hakuna wazo jipya katika mchakato wa amani

Akizungumza nchini Israel jana, Obama alisema hakuja na mpango mpya wa kuyapa msukumo mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina ambayo yamekwama. Badala yake, amesema amekuja kufanya mashauriano na pande zinazohusika. Mazungumzo yake na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu yalituama zaidi juu ya mpango wa nyuklia wa Iran, na mgogoro unaoendelea nchini Syria. Obama alimhakikishia Netanyahu kuwa Marekani inaunga mkono haki ya Israel kuhakikisha usalama wa wananchi wake. Lakini pia aligusia umuhimu wa suala la amani katika eneo la Mashariki ya Kati.

Akiwa nchini Israel, Obama alisema hakuja na wazo jipya kuhusu amani ya Mashariki ya Kati
Akiwa nchini Israel, Obama alisema hakuja na wazo jipya kuhusu amani ya Mashariki ya KatiPicha: Reuters

''Upepo wa mageuzi unaovuma katika kanda hii unaambatana na matumaini lakini pia na hatari kubwa.Naichukulia ziara hii kama nafasi nzuri, tunasimama pamoja kwa sababu amani lazima ije katika ardhi takatifu. Hata kama tunaelewa changamoto zilizopo, hatutapoteza dira ya kutaka Israel, ambayo inaishi kwa amani na majirani zake.'' Alisema Obama.

Rais Barack Obama alisema kuwa suala hilo la amani ambalo limekuwepo kwa miongo sita ni gumu, kwa vile pande husika zinayo maslahi yenye mizizi mirefu,ambayo mtu hawezi kuyarahisisha. Alikiri kwamba anaweza kuwa amefanya makosa kuhusu suala hilo, lakini akaongeza kuwa hatakuwa rais wa kwanza wa Marekani kugonga ukuta katika mazungumzo hayo.

Matumaini yafifia Palestina

Wanaharakati wa kipalestina wameweka kambi ya mahema karibu na makazi ya walowezi wa kiyahudi, wakimtaka Obama kuacha kuipendelea Israel, ambayo mpango wake wa kujenga makaazi mapya katika eneo lijulikanalo kama E1  unatishia kuitokomeza ndoto ya wapalestina kuwa na taifa lao wenyewe.

Wapalestina wengi wanaamini Obama amekwamisha ndoto yao ya kupata taifa huru
Wapalestina wengi wanaamini Obama amekwamisha ndoto yao ya kupata taifa huruPicha: SAIF DAHLAH/AFP/Getty Images

Na afisa wa Palestina katika mazungumzo ya amani Nabil Shaath, kupitia makala iliyochapishwa na gazeti la Israel la Haaretz, amemtaka raia Obama kuthibitisha msimamo wake wa kutaka mataifa mawili, Israel na Palestina, kwa kuweka ahadi zake katika vitendo.

''Nina uhakika kwamba yapo mambo ambayo ningekuwa nimeyafanya yangeleta matokeo mazuri zaidi'' Alisema Obama, na kuongeza kuwa iwapo mwishoni mwa ziara yake kesho ataweza kuelewa vyema zaidi vizingiti vilivyopo katika mchakato wa kutafuta amani kati ya Israel na Palestina, basi ziara yake itakuwa imepata mafanikio.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/DPAE

Mhariri: Ssessanga Iddi