Obama akutana na Mfalme Abdullah II | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.03.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Obama akutana na Mfalme Abdullah II

Rais Barack Obama wa Marekani ameonya kuwa vita vya Syria vinaweza kuitumbukiza nchi hiyo kwenye hali ya kutisha na ameitaka jumuiya ya kimataifa kuwaunga mkono wapinzani.

Rais Barack Obama na Mfalme Abdullah II wa Jordan

Rais Barack Obama na Mfalme Abdullah II wa Jordan

Matamshi hayo ameyatoa wakati wa mkutano wa pamoja na Mfalme Abdullah wa Pili wa Jordan na waandishi wa habari, mjini Amman. Rais Obama amesema ni muhimu kwao kufanya kazi kama jumuiya ya kimataifa kusaidia kuharakisha kipindi cha mpito cha kisiasa. Mfalme Abdullah ameelezea wasiwasi wake kuhusu mzozo wa nchi jirani ya Syria na ametaka kipindi cha mpito cha kisiasa kifanyike haraka ili kuzuia umwagaji damu na ubaguzi wa kidini. Jordan tayari ina zaidi ya wakimbizi 460,000 wa Syria.

Mfalme Abdullah wa Pili amesema idadi hiyo ya wakimbizi wa Syria ni sawa na asilimia 10 ya watu wa Jordan. Maafisa wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, wanakadiria kuwa Jordan, Lebanon na Uturuki zinaweza zikawapokea wakimbizi milioni moja wa Syria ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, iwapo vita vya wenyewe kwa wenyewe vitaongezeka. Zaidi ya watu 700,000 wameuawa katika vita vya Syria na hivyo kufanya idadi hiyo kuwa mbaya zaidi kutokea tangu kuanza kwa vuguvugu la mageuzi madarakani katika mataifa ya Kiarabu.

Marekani yawaunga mkono wapinzani wa Syria

Waziri Mkuu mteule wa upinzani Syria, Ghassan Hitto

Waziri Mkuu mteule wa upinzani Syria, Ghassan Hitto

Ingawa hakuzungumzia suala la kuivamia Syria kijeshi, Rais Obama amesema Marekani inawaunga mkono wapinzani wa Syria kama wenye kuaminika, kuliko utawala wa Rais Bashar al-Assad.

Amesema nchi yake itaendelea kutafuta suluhu ya kisiasa ya mzozo wa miaka miwili unaoendelea nchini Syria. Aidha, Rais Obama alitangaza kuwa Marekani itaipatia Jordan Dola milioni 200 ikiwa ni sehemu ya Dola bilioni moja zinazohitajika kwa ajili ya wimbi la wakimbizi wa Syria wanaoingia nchini humo.

Amesema fedha hizo zitakuwa kwa ajili ya msaada wa kibinaadamu na huduma muhimu, ikiwemo elimu kwa watoto wa Syria ambao wako mbali na nyumbani na ambao maisha yao yameharibiwa.

Obama leo anazuru Petra

Katika siku yake ya mwisho ya ziara ya siku nne ,Mashariki ya Kati, kabla ya kurejea Marekani, Rais Obama leo atazuru mji wa Petra uliotangazwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni-UNESCO, kama eneo la turathi za dunia na moja ya maajabu saba ya dunia.

Mapema jana Ijumaa, Rais Obama alizuru maeneo kadhaa ya Israel na Palestina. Alizuru kituo cha kumbukumbu ya mauaji ya Wayahudi cha Yad Vashem kilichopo Jerusalem na kuweka mashada ya maua katika makaburi ya Waziri Mkuu wa zamani wa Israel, Yitzhak Rabin, aliyeuawa Novemba mwaka 1995 na shujaa wa Israel, Theodor Herzl.

Rais Obama akiweka maua kwenye kaburi la Yitzhak Rabin

Rais Obama akiweka maua kwenye kaburi la Yitzhak Rabin

Katika Ukingo wa Magharibi kwenye mji wa Bethlehemu, kiongozi huyo wa Marekani, alitembelea Kanisa la uzawa , linalochukuliwa na Wakristu wengi kama sehemu aliyozaliwa Yesu Kristu.

Aidha, katika kuleta maelewano kwenye ukanda huo, Rais Obama aliandaa mazungumzo ya simu kati ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na mwenzake wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan. Katika mazungumzo hayo, Netanyahu alimuomba radhi Erdogan, kutokana na vifo vya Waturuki tisa waliouawa katika shambulio la kwenye boti iliyokuwa ikielekea Ukanda wa Gaza mwaka 2010.

Shambulio hilo katika meli lilizusha mzozo kati ya mataifa hayo mawili na kusababisha kufukuzwa kwa balozi wa Israel nchini Uturuki, huku mahusiano ya kijeshi yakiwa mabaya pia. Israel na Uturuki zimekubaliana kurejesha uhusiano wao wa kidiplomasia.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPAE,APE
Mhariri: Sekione Kitojo

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com