1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan Kusini

Njaa, majeraha ni mateso kwa watoto wa Sudan Kusini

18 Februari 2026

Mapigano mapya nchini Sudan Kusini yanaendelea kuzorotesha hali ya kibinadamu katika taifa hilo changa zaidi duniani. Hospitali zimeelemewa, chakula ni haba, na watoto ndio wanaoathirika zaidi.

https://p.dw.com/p/58zBt
Sudan Kusini-Vita-Njaa
Mtoto wa Sudan Kusini ambaye ni mkimbizi akiteka maji katika jimbo la JongleiPicha: Maura Ajak/AP/picture alliance

Tangu mwezi Desemba, mamia ya maelfu ya watu wamekimbia makazi yao kufuatia mapigano kati ya majeshi yanayomuunga mkono Rais Salva Kiir na yale yanayomtii makamu wake wa zamani Riek Machar.  Kutoka jimbo la Jonglei, simulizi za wakimbizi zinaonyesha taswira ya mateso, njaa na kukata tamaa.

Katika hospitali ndogo ya mji wa Akobo, mtoto wa miezi 18 amelazwa kimya kitandani akiwa na jeraha la risasi mguuni. Risasi hiyo pia ilimuua mama yake. Ni mmoja wa watoto wengi waliobaki yatima katika wimbi jipya la ghasia.

UN yatoa tamko

Umoja wa Mataifa unasema takribani watu 280,000 wamekimbia makazi yao tangu mapigano yalipozuka upya. Zaidi ya nusu yao ni watoto.

Wengi wamekimbia kwa mara ya pili au ya tatu tangu Sudan Kusini ijipatie uhuru mwaka 2011 na kisha kutumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Michael Alier Deng Alier, mkimbizi wa ndani mwenye umri wa miaka 47, anaeleza sababu ya kukimbia kwao: "Tuliikimba kutoka kwa ardhi yetu huko Jonglei kwa sababu ya mapigano kati ya SPLA ya upinzani na ile ya serikali. Mzozo huo umesababisha vifo vya watu wetu ambao hawkuwa na uwezo kuvikimbia na sisi tulikimbilia hapa. Tulipofika hapa, baa la njaa ndiyo changamoto kubwa inayotuathiri.”

Kurejea kwa Riek Machar Sudan Kusini

Baada ya kufika kambini, changamoto kubwa imekuwa njaa. Shirika la UNICEF linaonya kuwa zaidi ya watu 825,000 wako katika hatari ya utapiamlo mkali katika majimbo ya Jonglei, Unity na Eastern Equatoria.

Makambi yasiyo rasmi

Katika kambi isiyo rasmi kandokando ya Mto White Nile, mamia ya wanawake na watoto wanaishi chini ya miti wakisubiri msaada. Akeer Amou, mwenye umri wa miaka 33, alijifungua mtoto wake wa tano baada ya kukimbia mapigano. Mume wake aliuawa vitani.

"Mume wangu aliuawa nilizaa mtoto wake akiwa amekwisha uawa katika mapigani ambayo yalitulazimu kuyakimbia makazi yetu hadi hapa tulipo”

Amou alimpa mtoto wake jina "Riak” likimaanisha "janga”. Anasema hana chakula cha kutosha hata cha kumwezesha kunyonyesha ipasavyo.

Sudan Kusini Old Fangak 2021 | Madaktari Wasio na Mipaka wakiwatibu wagonjwa katika Mkoa wa Jonglei
Madaktari Wasio na Mipaka wakiwatibu wagonjwa katika Mkoa wa JongleiPicha: Sam Mednick/AP Photo/picture alliance

Wakati huo huo, katika mji mkuu wa jimbo la Jonglei, Bor, hospitali zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa dawa na vifaa. Baadhi ya vituo vya afya vimeharibiwa katika mashambulizi ya awali, na sasa madaktari wanaonya huenda wakapoteza wagonjwa kwa kukosa vifaa muhimu.

Lakini mateso haya yamewaathiri zaidi wanawake. Nyadak Kurjiok, mwenye umri wa miaka 35, amepoteza mume wake na watoto watatu katika vita. "Ujumbe wangu kwa pande zote zisimamishe mapigano na tukiwaruhusu wanawake katika majadiliano ya mapatano itakuwa bora zaidi kwa sababu sisi kama wanawake tumeteseka sana katika nchi hii. Kwa hakiki nimempoteza mume wangu katika vita hivi. Kizazi hiki kina fursa hii tu kuwa na waume zao ulimwenguni. Wanawake hawa unaowaona hapa ni wajane, baadhi yao hata wamepoteza watoto wao katika vita hivi.”

Sudan Kusini, ambayo tayari inategemea wafadhili wa kimataifa kwa zaidi ya asilimia 80 ya huduma za afya, sasa inakabiliwa na kizazi kingine cha watoto wasio na elimu, chakula wala matumaini ya maisha bora.