1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria yamwita balozi wake aliyeko Libya

Kabogo Grace Patricia19 Machi 2010

Hatua hiyo inafuatia matamshi yaliyotolewa na kiongozi wa Libya, Muammar Gadhafi ya kuitaka Nigeria igawanywe kati ya Waislamu na Wakristo.

https://p.dw.com/p/MWqm
Rais wa Nigeria, Umaru Yar'Adua, (kulia), akiwa na rais wa zamani wa nchi hiyo, Olusegun Obasanjo, (shoto) na Kaimu rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan (kati).Picha: AP

Nigeria imemuita balozi wake aliyeko nchini Libya, baada ya kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gadhafi, kupendekeza kuwa nchi ya Nigeria igawanywe pande mbili kati ya Waislamu na Wakristo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje wa Nigeria, Ozo Nwobu, alisema jana kuwa balozi wa nchi hiyo nchini Libya ameitwa kwa ajili ya mashauriano ya haraka. Nwobu alisema kuwa matamshi ya Kiongozi wa Libya, Muammar Gadhafi, yamepunguza hadhi na uaminifu wake. Msemaji huyo wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Nigeria aliyazungumza hayo wakati akisoma taarifa iliyotolewa na serikali yake iliyoonyesha wasi wasi mkubwa kufuatia matamshi hayo ya Gadhafi.

Taarifa hiyo ya Nigeria pia imemtuhumu Gadhafi kwa kuingilia na kulichukulia kama jukwaa kila tukio linalotokea. Gadhafi alipendekeza kuwa Nigeria ifuate mfumo wa Pakistan na kuigawa nchi hiyo, ikiwa kama njia ya kumaliza mzozo wa kidini uliopo nchini humo. Kanali Gadhafi alipendekeza kuwa Wakristo wachukue eneo la kusini ambalo litaufanya mji wa Lagos kuwa mji mkuu wake, huku Waislamu wakilichukua eneo la kaskazini na kuufanya mji wa Abuja kuwa mji mkuu wake. Aidha, alipendekeza kuwa pande hizo mbili zikubaliane katika njia ya amani kugawana eneo lenye utajiri mkubwa wa mafuta pamoja na madini.

Mamia ya wananchi waliuawa katika mapigano ya kidini yaliyotokea wiki iliyopita katika Jimbo la Plateau. Jimbo hilo, likiwa mji mkuu wake ni Jos, limegawanyika kati ya Wakristo walioko upande wa kusini na Waislamu upande wa kaskazini. Taarifa ya wizara hiyo imefafanua kuwa matamshi ya Kanali Gadhafi kufuatia mapigano hayo ya Jos, hayakubaliki kutoka kwa kiongozi yoyote yule anayedai kuwa bingwa wa kutetea kuwepo amani, muungano na Umoja wa Afrika. Nigeria, yenye jumla ya idadi ya watu milioni 140, imegawanyika karibu sawa kati ya Waislamu na Wakristo.

Mapema rais wa bunge la Nigeria, David Mark, alimuelezea Kanali Gadhafi kama mwendawazimu. Kauli hiyo aliitoa siku ya Jumatano wakati akijibu maswali ya wabunge. Aidha, taarifa hiyo ya wizara ya mambo ya nchi za nje imesema Nigeria inapokea ushauri na maoni mazuri yenye kujenga kutoka kwa wanachama wote wa jumuiya ya kimataifa.

Wakati huo huo, bunge la Nigeria limemtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, kumuamuru Gadhafi kufuta pendekezo lake la kutaka kuigawa Nigeria kwa misingi ya kidini. Aidha, bunge hilo limeutaka Umoja wa Afrika kuamuru kufanyika uchunguzi wa kuangalia sababu zilizomfanya Kanali Gadhafi kutoa mapendekezo kama hayo. Hata hivyo, Nwobu alisema kitendo cha kumuita balozi wake kutoka Libya hakimaanishi kuwa uhusiano kati ya Nigeria na Libya umeharibika, lakini ni katika kuonyesha kuwa Nigeria imechukizwa na kitendo hicho.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)

Mhariri:Othman Miraji