Netanyahu: Iran itakuwa na silaha za nyuklia miaka 10 ijayo | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.10.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Netanyahu: Iran itakuwa na silaha za nyuklia miaka 10 ijayo

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ameonya kuwa Iran itakuwa na silaha za kinyuklia katika miaka 8-10 ijayo, ikiwa hakutakuwa na mabadiliko katika mkataba wa kimataifa kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

 

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ameonya kuwa Iran itakuwa na silaha za kinyuklia katika miaka 8-10 ijayo, ikiwa hakutakuwa na mabadiliko katika mkataba wa kimataifa kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran. Kauli yake hiyo ameitoa siku chache baada ya rais wa Marekani Donald Trump kukataa kuthibitisha mbele ya bunge, ikiwa Iran ilikuwa ikitekeleza sehemu yake ya makubaliano hayo.

Katika mkutano na Waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu mjini Jerusalem, Netanyahu ambaye ni mkosoaji mkuu wa mkataba wa kimataifa wa Iran kuhusu nyuklia, amesema Iran itakuwa na silaha za nyuklia katika miaka kumi ijayo ikiwa mkataba huo hautafanyiwa mabadiliko.

Kauli hiyo ya hivi karibuni inajiri siku chache baada ya rais wa Marekani Donald Trump kukataa kuuthibitisha mkataba wa Iran, na badala yake akalipa baraza la Congress la Marekani siku 60 kuamua ikiwa vikwazo vilivyoondolewa dhidi ya Iran wakati mkataba huo uliposainiwa vitarudishwa.

Wakati huo huo rais wa Iran Hassan Rowhani amekaribisha uungwaji mkono wa Umoja wa Ulaya kuhusu mkataba huo, licha ya rais Trump kuutilia mashaka.

Rais wa Iran Hassan Rowhani

Rais wa Iran Hassan Rowhani

Afisa mshauri mkuu wa kiongozi wa kidini wa Iran, amezionya serikali za Umoja wa Ulaya kuhusu kuweka vikwazo vipya dhidi ya mkataba huo. Ali Akbar Valeyati amesema " Kusema kuwa wanaukubali mkataba wa nyuklia lakini kuna haja ya mazungumzo kuhusu uwepo wa Iran katika kanda au mazungumzo kuhusu makombora ya ulinzi ya Iran, ni kuuwekea mkataba masharti na hilo halikubaliki." Amesisitiza kuwa hiyo si haki ya Ulaya na kwamba mkataba huo ambao pia unaitwa JCPOA hauna masharti hivyo ni lazima kuutekelezwa jinsi ulivyosainiwa.

Macron: Kuna haja ya mazungumzo ili mkataba udumu

Katika mazungumzo ya Ijumaa kati ya Rowhani na rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron alisema kuna haja ya mazungumzo ya usalama wa kikanda na mpango wa makombora ya Iran ili kuhakikisha mkataba huo ulioafikiwa 2015 unadumu.

Kwenye taarifa iliyochapishwa Jumanne katika tovuti ya afisi yake, Rowhani ameandika kuwa  uungwaji mkono wa Umoja wa Ulaya ni hatua muhimu ya mafanikio kisiasa kwa Iran.

Mnamo Jumatatu, mawaziri wa Mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya waliashiria uamuzi wao kuuheshimu mkataba huo jinsi ulivyo, baada ya Trump kusema atalitaka bunge kukaza sheria dhidi ya Iran.

Tofauti na tangazo la Trump, washirika kadhaa walitoa kauli za kuunga mkono mkataba wa nyuklia wa Iran, wakiwemo Ufaransa, Ujerumani na Uingereza ambao ni marafiki wa Marekani. Rowhani ameongeza kuwa hatua ya Trump imemtenga zaidi kwa kuonekana kutaka kuuhujumu mkataba huo.

Mwandishi: John Juma/DPAE/AFP

Mhariri: Gakuba, Daniel

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com