Netanyahu ateuliwa kuunda serikali nchini Israel | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.02.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Netanyahu ateuliwa kuunda serikali nchini Israel

Benjamin Netanyahu ajiandaa kurejea tena madarakani

default

Kiongozi wa Likoud,Benjamin Netanyahu


Rais Shimon Peres wa Israel amemteuwa hii leo mkuu wa chama cha mrengho wa kulia,Benjamin Netanyahu, kuunda serikali kufuatia uchaguzi wa bunge wa February 10 iliyopita.Tangazo hilo limesadif wakati seneta wa chama cha Democratic cha Marekani yuko ziarani Mashariki ya kati.


Mara baada ya kuchaguliwa ,kiongozi huyo shupavu anaefuata siasa kali za mrengo wa kulia, amesema anataka kuunda serikali ya umoja wa taifa kwa ushirikiano pamoja na chama cha Kadima kinachoongozwa na Tzipi Livni na kile cha mrengo wa shoto cha Labour.


"Nnamtolea mwito mwenyekiti wa Kadima, bibi Tzipi Livni, na mwenyekiti wa Labour, Ehud Barak, na ninawaambia- tuungane ili tulinde mustaskbal wa taifa la Israel. Ninawaomba tukutane kwanza tuzungmzie uwezekano wa kuunda serikali ya muungano wa vyama vingi kwa masilahi ya umma na taifa la Israel"- amesema hayo Benjamin Netanyahu wakati wa mkutano na waandishi habari.


Hata hivyo kiongozi wa Kadima Tzipi Livyi ameshasema hapendelei kujiunga na serikali itakayoongozwa na Benjamin Netanyahu.Yeye mwenyewe alikua akiamini angechaguliwa kwanza kuunda serikali kutokana na ule ukweli kwamba chama chake ndicho kilichojikingia viti vingi zaidi ya Likoud-viti 28 dhidi ya 27.


Rais Shimon Peres akizungumza katika mkutano huo huo wa waandishi habari, baada ya kumteuwa Netanyahau kuunda serikali,amesema wazi kabisa amepitisha uamuzi huo kwa sababu mkuu huyo wa mrengo wa kulia anaweza kupata uungaji mkono wa vyama vyengine vya mrengo wa kulia na kudhibiti wingi wa viti bungeni.


Wabunge 65 wanamuunga mkono Netanyahu-amesema rais Peres.


Netanyahu,aliyewahi kuwa waziri mkuu shupavu wa Israel kati ya mwaka 1996 na mwaka 1999, amesema ataendeleza siasa ya kudhamini usalama na amani pamoja na majirani wa Israel.


Akigusia maneno aliyokua akiyasema wakati wa kampeni yake ya uchaguzi,Benjamin Netanyahu amesema Israel inakabiliwa na kitisho kutoka "

Iran na ugaidi."


Wakati huo huo, wawakilishi watatu wa baraza la Senet na la wawakilishi wa Marekani wamefika ziarani bila ya kutarajiwa huko Gaza.Seneta wa chama cha Democratic, John Kerry, na wenzake wawili wa baraza la wawakilishi waliitembelea Gaza jana na kujionea hasara iliyosababishwa na hujuma za kijeshi za Israel.


Seneta John Kerry ambae hii leo anatazamiwa kuzungumza na viongozi wa serikali ya Israel na wale wa Palastina amesema ziara yake hii haimaanishi  siasa ya Washington kuelekea Hamas imebadilika.


Senetor John Kerry,amekabidhiwa risala iliyopenyezwa katika makao makuu ya shirika la misaada la Umoja wa mataifa huko Gaza,risala ambayo imedhamiriwa rais wa Marekani Barack Obama.Msemaji wa shirika hilo la Umoja wa mataifa,Chris Gunness amesema wanaamini risala hiyo imeandikwa na Hamas.


Seneta John Kerry anatazamiwa kwenda Damascus Syria kesho.

 • Tarehe 20.02.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GyDc
 • Tarehe 20.02.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GyDc

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com