1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasafiri kutokea Tanzania kutokaa karantini

Thelma Mwadzaya16 Septemba 2020

Kenya na Tanzania zimerejesheana utaratibu wa kuziruhusu ndege zao kuingia kwenye mipaka yao ya angani kufuatia miezi miwili ya sintofahamu.

https://p.dw.com/p/3iXoL
Kenya Airways Flughafen Nairobi ARCHIV
Picha: picture-alliance/dpa

Kwa upande wake Kenya imewaondolea wasafiri wanaotokea Tanzania sheria ya karantini ya lazima pindi wanapowasili.

Jumla ya mataifa 147 yakiwemo ya Afrika mashariki yapo kwenye orodha ya yale ambayo raia wake wanaruhusiwa kuingia Kenya bila masharti katika msimu huu wa corona.

Serikali ya Kenya sasa imeiweka Tanzania kwenye orodha ya mataifa ambayo raia wake wanaweza kuingia ndani ya mipaka yake pasina masharti makali ya kupambana na covid 19. Kwa mantiki hii wasafiri wanaotokea Tanzania wameondolewa sharti la kuwekwa kwenye karantini ya lazima ya wiki mbili pindi wanapowasili ndani ya mipaka ya Kenya.

Waziri wa uchukuzi wa Kenya James Macharia amesema: "Tulichokifanya ni kuweka bayana sera na vigezo vya afya mintarafu abiria wanaotokea nchi tofauti.Tunadurusu kila wakati orodha ya abiria wasiohitaji kwenda karantini".

Tanzania pia yaondoa marufuku ya ndege zote za Kenya

Tansania Julius Nyerere International Airport Fluggäste
Abiria katika uwanja wa ndege wa Tanzania wa Julius Nyerere Picha: DW/K. Makoye

Kwa upande wake Tanzania nayo imeiondoa marufuku ya ndege zote za Kenya kuingia ndani ya anga yake kama njia ya kuimarisha uhusiano. Kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya usafiri wa ndege nchini Tanzania,Hamza Johari,ndege zote zinaruhusiwa kuingia kuanzia sasa.

Kwenye taarifa yake hii leo,Johari aliusisitizia muhimu wa kudumisha ujirani mwema na biashara kati ya mataifa hayo mawili. Haya yanajiri ikiwa imepita miezi miwili ya mvutano na sintofahamu kati ya Tanzania na Kenya mintarafu usafiri na maambukizi ya COVID 19.

Mwezi wa Agosti Tanzania ilipiga marufuku ndege ya kampuni ya Kenya Airways kuingia ndani ya mipaka yake kama njia ya kulipizana kisasi baada ya kutojumuishwa kwenye orodha ya mataifa ambayo raia wake wanaruhusiwa kuingia Kenya.

Mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya usafiri wa ndege nchini Tanzania,Hamza Johari anaelezea kilichowapelekea kuchukua msimamo huo miezi miwili iliyopita: "Kenya walikuwa wameomba kuja Tanzania. Hatukuwa na tatizo na tukawapa hiyo ruhusa.Lakini baadaye tukasikia wao wanatuzuwia sisi tusiende kule kwahiyo kwa kufuata principle hiyo hiyo ya usawa basi na sisi tufute hiyo ruksa ambayo tuliwapa".

Mataifa mengine ambayo yako kwenye orodha hiyo mpya ni pamoja na Ghana,Nigeria na Sierra Leone. Chanzo cha mzozo huo wa kidiplomasia kinaaminika kuwa msimamo wa Tanzania kuhusu maambukizi ya COVID 19 ambao hakuegemea kusitisha shughuli zao za kawaida.

Yote hayo yakiendelea, raia wa kigeni waliokuwa wamepewa msamaha wa kusalia nchini Kenya bila masharti sasa wamepewa wiki mbili kuisawazisha hali kwa kusaka vibali au kurejea kwao.

Kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa Idara ya uhamiaji Alexander Muteshi,raia hao wa kigeni wamepewa nafasi kuondoka kwani sasa ndege za kimataifa zinaruhusiwa kusafiri.

Mwezi wa Mei idara hiyo iliiomba idara ya polisi kutowakamata au kuwachukulia hatua za kisheria raia wa kigeni waliojikuta wamenasa nchini Kenya kwasababu ya corona.