1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za Kiafrika zajipanga kuzuia homa ya corona

Daniel Gakuba
25 Januari 2020

Wakati homa itokanayo na virusi vya Corona ikienea duniani, nchi za kiafrika zimeanzisha juhudi za dharura kuzuia kuingia kwa ugonjwa huo, ambao tayari umeuwa watu 41 nchini China. Ugonjwa huo umeingia Ulaya na Marekani.

https://p.dw.com/p/3WnlQ
Deutschland Forschung Coronavirus
Picha: picture-alliance/dpa/C. Gateau

Mataifa kadhaa ya Afrika yameanzisha upimaji wa joto la mwili katika viwanja vya ndege na kuchukua hatua za tahadhari kuzuia kusambaa kwa virusi vipya vya Corona vilivyowakumba mamia ya watu nchini China.

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo imesema inachukua hatua za tahadhari katika viwanja vya ndege na bandari zikiwalenga watu wanaotoka mataifa yaliyoathirika na virusi hivyo.

Waziri wake wa afya, Eteni Longondo ameliambia shirika la habari la DPA, kuwa Congo haiijui homa, lakini ''tunachukua hatua za tahadhari ili isifike huku''.

Sri Lanka Corona-Virus
Miji kadhaa ya China imewekwa chini ya karantini kuzuia kasi ya kuenea kwa virusi vya CoronaPicha: Reuters/D. Liyanawatte

Vipimo kwenye vituo vya kuingilia

Nigeria, Uganda, Ghana na Ushelisheli pia zimetangaza mipango ya kuchukua hatua kama hizo kukabiliana na virusi vya Corona ambapo wasafiri watapimwa joto la mwili kubaini dalili za maambukizi ya virusi.

Kituo cha kuzuia magonjwa ya kuambukiza nchini Nigeria, NCDC kimesema kimeimarisha ukaguzi katika vituo vyote vya kuingilia nchini humo, na kuongeza kuwa wasafiri watakaowasili kutoka mji wa Wuhan, ilikoanzia homa hiyo, wataulizwa masuali kubainisha hali yao ya kiafya, na historia ya safari zao.

Nchini Uganda, msemaji wa wizara ya afya, Emmanuel Ainebyoona, amesema maafisa wa afya walioweka mpakani kuchunguza maradhi ya Ebola, hivi sasa watatumiwa pia kuchunguza homa hii itokanayo na virusi vya Corona.

China Corona-Virus
Mkakati mojawapo wa kuzuia kuenea kwa homa hiyo hatari, ni kuchukua vipimo vya joto kwa wasafiriPicha: Reuters/M. Pollard

Kitisho kinabakia katika kiwango cha chini

Zimbabwe, kupitia waziri wake wa afya Obadiah Moyo imesema ingawa haijaanza shughuli za uchunguzi mpakani na kwenye viwanja vya ndege, inafuatilia kwa karibu kama ilivyo katika nchi nyingine za dunia.

''Hatuchukui vipimo vyovyote kwa wakati huu, lakini tunawashauri wasafiri wote wanaowasili kutoka China, kwenda kuchunguza afya zao katika vituo vya afya.'' amesema waziri Moyo.

Taasisi ya magonjwa ya mripuko nchini Afrika Kusini imesema iko chonjo kufuatilia hali inayoendelea, ikisema imebaini kuwa hakuna ndege zinazoruka moja kwa moja kutoka mji wa Wuhan nchini China kuja Afrika Kusini.

Taasisi ya nchi hiyo inayohusika na magonjwa ya kuambukiza, imesema haioni kitisho kikubwa cha homa ya Corona kuingia nchini humo.

China ni mshirika muhimu wa kibiashara kwa nchi nyingi za Kiafrika, na maelfu husafiri kati ya Afrika na China kila siku kwa shughuli mbli mbali za kibiashara.

 

dpae, afpe