1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvua yaua watu 9 Dar es Salaam

Lilian Mtono
19 Aprili 2018

Mvua zinazoendelea kunyesha nchini Tanzania zimetajwa kuleta madhara mbalimbali ikiwemo vifo, kusimama kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi pamoja na miundombinu ya barabara kuharibiwa vibaya.

https://p.dw.com/p/2w8ah
Tansania Daressalam Überflutungen
Picha: DW/S. Khamis

Mvua zinazoendelea kunyesha nchini Tanzania zimetajwa kuleta madhara mbalimbali ikiwemo vifo, kusimama kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi pamoja na miundombinu ya barabara kuharibiwa. Baadhi ya huduma za kijamii zimesitishwa ikiwemo usafiri wa mabasi yaendayo kasi, kufungwa kwa shule huku mamlaka zikitahadharisha kuwa huenda matokeo mabaya yakashuhuduwa zaidi endapo watu hawatakuwa makini dhidi ya mafuriko yanayoendelea. 

Picha zilizopigwa kutoka angani zinalionesha jiji la Dar es Salaam kulemewa na maji, barabara kadhaa zimesimamishwa kutoa huduma ikiwemo barabara kuu ya dar es salaa morogoro kutokana na kufunikwa na maji.

Huduma ya usafirishaji kwa magari yaendayo kasi imesitishwa kwa tariban saa kumi na moja kwa njia ya jangwani,maeneo mengi ya makazi ya watu yamefunikwa na maji ikiwemo jangwani, baadhi ya maeneo ya buguruni, kigogo, msimbazi na mengineyo.

Wakaazi waliozungumza na Dw wanasema kuwa maji yalianza kufurika nyakati za usiku wengi wao wakiwa wamelala na hata wengine kukumbwa na umauti kutokana na kudondokewa na vitu ikiwemo kuta za nyumba na wengine kwenda na maji.

Kamanda wa polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amethibitisha kutokea kwa vifo tisa vya watu vilivyotokana na mafuriko ikiwemo watoto.

Aidha kamanda mambo sasa ametangaza huenda madhara yakashuhudiwa zaidi endapo watu hawatachukua tahadhari za kuondoka kwenye nyumba zao zilizojaa maji, kutopita na vyombo vya moto katika barabara zilizofunikwa na maji na kuvuka mito ama sehemu zilizojaa maji bila kujua kina cha maji.

Hata hivyo shule kadhaa zimetangaza kusitisha masomo kwa siku ya leo kutokana na hali ya mvua zilizosababisha mafuriko kuendelea kunyesha ndani ya jiji, na baadaye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama na mkuu wa mkoa huo Paul Makonda kutangaza kusitisha masomo kwa siku mbili ili kuepuka madhara ambayo huenda yangejitokeza kwa wanafunzi ikiwemo kupelekwa na maji.

Wakazi waliozungumza na Dw wanasema kuwa hawajaokoa kitu katika nyumba zao, wengine iliwabidi kuwabeba wagonjwa usiku wa manane na kuwahamisha kwa jamaa zao, huku wengine wakithibitisha kutolala takriban siku tatu kutokana na mafuriko.

Juma lililopita mamlaka ya hali ya hewa nchini ilitangaza na kutoa tahadhari juu ya mvua hizi zinazoshuhudiwa huku mamlaka nchini humo zikitoa onyo kwa wote wasiokuwa na shughuli za msingi kutotoka katika hifadhi zao na kuongeza kuwa mvua nyingi zitaendele kunyesha hadi mapema mwezi ujao.

Mwandishi: Hawa Bihoga Dw Dar es Salaam

Mhariri:Josephat Charo