1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Moto wa mlima Kilimanjaro umeathiri mfumo wa ikolojia

Veronica Natalis
19 Novemba 2020

Mtafiti wa masuala ya mimea wa chuo kikuu cha Bayreuth, Ujerumani, Andreas Hemp, amefanya utafiti juu ya moto uliotokea mlima Kilimanjaro na ameandika makala inayoelezea athari za moto huo katika mfumo wa ikolojia.

https://p.dw.com/p/3lYya
Tansania Feuer auf dem Kilimandscharo
Picha: DW/Veronica Natalis

Mtafiti wa masuala ya mimea wa chuo kikuu cha Bayreuth, Ujerumani, Andreas Hemp ameandaa makala inayoeleza mlima kilimanjaro utakuwa na muonekano wa kipekee kimazingira kwa siku za usoni kutokana na moto huo. 

Katika ripoti yake mtafiti huyo wa mimea Andreas Hemp amebainisha kuwa sio mara ya kwanza kwa moto kutokea katika baadhi ya maeneo ya mlima huo mrefu kuliko yote barani Afrika, hasa katika kipindi cha mwishoni mwa msimu wa kiangazi mwezi februari hadi machi, na mwezi septemba hadi oktoba. Soma Zaidi  Juhudi za kuuzima moto Mlima Kilimanjaro zaendelea

Utafiti huo ambao umefanywa kwa ushirikiano na watafiti wengine wa masuala ya mimea, umetumia sehemu ya mbegu za mimea zinazotumika  kwenye uchavushaji  yaani Poleni, ambazo zimedumu ardhini kwa miaka zaidi ya elfu 50 iliyopita ambazo zilitoa majibu kuwa moto unasaidia kutengeneza ukanda wa uoto hasa katika maeneo ya hifadhi.

Kwa mantiki hiyo moto uliowaka katika sehemu ya hifadhi ya milima Kilimanjaro kipindi cha mwezi oktoba mwaka huu na vipindi vya nyuma, utasaidia kuotesha mbegu za mimea ambazo maganda yake ni magumu na yanatakiwa kuunguzwa kwa moto. Vile vile moto unasaidia aina nyingine ya mimea kukua baada ya kubanwa na kukosa mwanga kwa muda mrefu. Hii lakini haizuii kuleta madhara kama hatua za kudhibiti hazitachukuliwa.

Tansania Kilimandscharo Brand | Satellitenbild
Picha ya Satelaiti inanyesha moshi kileleni mwa mlima KilimanjaroPicha: NASA MODIS Satellite Image/Reuters

Athari zilikuwa kubwa zaidi

Andreas Hemp anasema "Kina kitu kimoja kikubwa serikali ya Tanzania inatakiwa kufanya, kwanza ni kuwa na ndege za kusaidia uzimaji wa moto unapotokea. Katika tukio la moto lililopita kulikuwa na ndege moja tu, hivyo inahitajika ndege kubwa inayoweza kubeba maji mengi ya kuzima moto.”

Sehemu ya ripoti hiyo inaeleza kuwa athari za moto  uliotokea mlima Kilimanjaro katika kipindi cha nyuma zilikuwa kubwa zaidi ikilinganishwa na athari ambazo zimetokea  mwezi oktoba ambapo moto uliowaka  uliathiri ardhi ya msitu na sio msitu wenyewe.

Hii ni kutokana na urefu wa mlima Kilimanjaro, na hivyo kuufanya kuwa na kanda kadhaa za mimea, na  kuifanya hifadhi hiyo ya taifa la Tanzania, kuwa na utajiri wa bioanuwai na miti mirefu zaidi barani Afrika. 

Tansania Berg Kilimanjaro
Mlima KilimanjaroPicha: Finbarr O'Reilly/Reuters

Hata hivyo ripoti hiyo imeeleza kuwa kwa zaidi ya miaka 150 iliyopita joto limeendelea kuongezeka kwa  mkoa wa Kilimanjaro na maeneo jirani, na hivyo kusababisha kupungua kwa barafu kwa karibu asilimia 90 ya kiwango chake cha zamani. Hiyo ni moja kati ya sababu zilizotajwa kuchangia kusababisha matukio ya moto katika mlima Kilimanjaro, japo pia matukio ya moto huwa na athari chanya katika maeneo ya hifadhi. Haya yanaungwa mkono  na  Joseph  Thomas  Mwenda, mwanamazingira kutoka Tanzania.

Hata hivyo milima huo ambao ni kivutio kikubwa cha utalii duniani, unakabiliwa na kitisho cha kupoteza mimea ya asili kutokana na ongezeko la idadi ya watu wanaoishi kuzunguka mlima huo. Asilimia 50 ya msitu wake wa asili umepotea kutokana na shughuli za kilimo na makazi ya watu, huku sehemu ya juu ikipoteza misitu ya asili kwa sababu ya majanga ya moto.

Andreas amesema "Katika mlima Kilimanjaro karibu kila sehemu misitu ya pembezoni mwa mito inapotea. Ni muhimu kutunza  uoto ulio pembezoni ili kulinda mfumo wa ikolojia.” 

Mtafiti Andreas Hemp anatoa maoni kuwa, hifadhi ya taifa ya mlima Kilimanjaro inakuwa kisiwa cha ikolojia kilichotengwa kabisa na kuzungukwa na kilimo, na hii inazuia ubadilishaji wa idadi ya wanyama na inaathiri bioanuwai, na hivyo juhudi zaidi zinahitajika kutoka serikali ya Tanzania kuilinda hifadhi hiyo.

Juhudi za kuudhibiti moto Kilimanjaro zinaendelea