Mshambuliaji wa St. Petersburg ni kutoka Kyrgyzstan | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.04.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mshambuliaji wa St. Petersburg ni kutoka Kyrgyzstan

Mtu aliyefanya shambulizi la bomu mjini St. Petersburg, Urusi ametambuliwa kuwa mzaliwa wa Kyrgyzstan. Mshambuliaji huyo anahusishwa pia na makundi ya kigaidi. Watu 14 wengine wengi wamejeruhiwa.

Kamati ya Usalama wa Taifa ya Kyrgyzstan imesema katika taarifa yake kwamba mlipuaji wa bomu katika kituo cha treni mjini St. Petersburg, ni mzaliwa wa taifa hilo lililokuwa sehemu ya Umoja wa Kisovieti, na kuongeza kuwa mtu huyo sasa ni raia wa Urusi. Kamati hiyo imesema inashirikiana na maafisa wa Urusi katika uchunguzi unaoendelea.

Mlipuko huo wa bomu ulitokea katika kituo cha treni ya chini ya ardhi katika mji wa pili kwa ukubwa wa Urusi hapo jana. Watu 14 wameuawa na wengine zaidi ya 40 wamejeruhiwa.

Hamna kundi lolote lilojitokeza kukiri kuhusika na shambulio hilo, ambalo lilitokea wakati Rais wa Urusi Vladimir Putin alipokuwa akizuru mji huo alipozaliwa ili kumpokea mgeni wake, kiongozi wa Belarus.

Russland Polizei nach Terroranschlag auf U-Bahn in St. Petersburg (picture-alliance/AP Photo/E. Kurskov)

Polisi katika eneo la tukio la tukio St.Petersburg

Viongozi wa dunia walaani shambulio hilo

Viongozi kadhaa wamelaani shambulio hilo akiwamo Rais wa Belarus Alexander Lukashenko aliyetoa rambirambi zake kwa familia za waathirika. Rais wa Marekani Donald Trump amelitaja shambulio hilo kuwa ni kitu kibaya na kinachoendelea kutokea duniani kote. Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Anthonio Guterres amesema waliohusika lazima wawajibishwe.

Waziri Mkuu wa Japana Shinzo Abe amelaani shambulio hilo la kigaidi na kusema kuwa Japan ipo pamoja na Rais wa Urusi Vladimir Putin na watu wake.

"Ningependa kutoa salamu zangu za rambirambi kwa familia za waathirika na waliopata majeraha. Matukio ya kigaidi hayawezi kustahamilika na Japan ipo pamoja na Rais Vladimir Putin na watu wa Urusi katika kipindi hiki kigumu. Tupo tayari kupambana na ugaidi tukishirikiana na jumuiya ya kimataifa," amesema Shinzo Abe.

Katika miongo miwili iliyopita, ndege na treni za Kirusi zimekuwa zikilengwa mara kwa mara kwa mashambulizi, ambayo aghlabu lawama likiwaangukia wanamgambo wa Kiislamu.

Pande zote mbili, mamlaka ya Urusi pamoja na ya Kyrgyzstan hazikuweka wazi kama mshambuliaji huyo alijitoa muhanga au alifanikiwa kukimbia.

Russland Terroranschlag auf U-Bahn in St. Petersburg (picture-alliance/AP Photo/D. Lovetsky)

Rais wa Urusi Vladimir Putin akiweka shada la maua

Mshukiwa ana mafungamano na makundi ya kigaidi

Shirika la habari la Interfax limesema mamlaka husika zinaamini mshukiwa, mwenye umri wa miaka 23 aliyetokea taifa la Asia ya Kati lilowahi kuwa katika Muungano wa Kisovieti na anayehusishwa na makundi yenye siasa kali za dini ya Kiislam, aliingia na bomu hilo katika treni wakati akiwa amelibeba katika mkoba wa mgongoni.

Masaa mawili baada ya shambulio, shirika la kupambana na ugaidi limegundua na kulikongoa bomu la pili katika kituo kingine cha treni. Ni kituo kikubwa cha treni kinachotumika na watu wengi wanaotaka kuunganisha vituo viwili vya treni na pia kinatumika kupanda treni zinazokwenda mji mkuu wa Moscow.

Mfumo mzima wa treni wa mji wa St. Petersburg ulifungwa jana na watu wote kuhamishwa , lakini baadhi ya huduma zilirudi kama kawaida baada ya masaa sita.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/dpae/ape

Mhariri: Daniel Gakuba

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com