Msako mkali waendelea mjini Brussels | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.03.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Msako mkali waendelea mjini Brussels

Waripuaji watatu wa kujitoa muhanga walioshambulia uwanja wa ndege na kituo cha treni mjini Brussels wametambuliwa, huku msako mkali ukiendelea kumtafuta mwanaume wa nne ambaye bomu lake lilishindwa kuripuka.

Uwanja wa ndege wa Zaventem unavyoonekana baada ya kushambuliwa.

Uwanja wa ndege wa Zaventem unavyoonekana baada ya kushambuliwa.

Waendesha mashtaka wamesema ndugu wawili - Ibrahim na Khalid El Bakraoui - ndiyo walifanya mashambulizi kwenye uwanja wa ndege wa Zaventem na kituo cha treni cha Maalbeek, wakati mtaalamu wa kutengeza mabomu Najim Laachraoui alitambuliwa na duru za polisi kuwa mripuaji wa pili katika shambulio la uwanja wa ndege.

Polisi imeimarisha msako wa mripuaji wa tatu wa uwanja wa ndege, alieonekana kwenye kamera za CCTV akiwa amevalia koti jeupe kwenye ukumbi wa kuondokea wa uwanja wa Zaventem, na ambaye sanduku lake la miripuko lilishindwa kuripuka pamoja na waripuaji wengine wa kujitoa muhanga.

Washukiwa hao watatu waliotambuliwa kuhusika na mashambulio mawili yaliyoua watu 31 na kuwajeruhi wengine 300, wamehusishwa pia na mashambulio ya Novemba mwaka jana mjini Paris Ufaransa, na kutilia mkazo kitisho kinachoyakabilia mataifa ya Ulaya kutoka kundi hilo la wanaojiita wapiganaji wa jihadi.

Ndugu waliohusika katika mashambulizi - Ibrahim na Khalid El Bakraoui.

Ndugu waliohusika katika mashambulizi - Ibrahim na Khalid El Bakraoui.

Rais Erdogan aikosoa Ubelgiji

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameikosoa Ubelgiji kwa kushindwa kumfuatilia Ibrahim El-Bakraoui, Mbelgiji alietiwa hatiani kwa ujambazi wa kutumia silaha, ambaye Uturuki ilimkamata karibu na mpaka wa Syria Juni 2015, na kumrudisha kama mpiganaji wa kigaidi wa kigeni.

Lakini serikali ya Ubelgji imekanusha ukosoaji wa rais Erdogan, ikisema Bakraoui mkubwa mwenye umri wa miaka 29 hakurejeshwa Ubelgiji bali nchi jirani ya Uholanzi. Maafisa wamesema kama ilivyokuwa katika kesi ya mmoja wa washmabuliaji wa Paris, hawawezi kuwashikilia washukiwa kutoka Uturuki bila kuwa na ushahidi wa wazi wa uhalifu.

"Tulimrejesha Uholanzi kulingana na ombi lake na tukaripoti urejeshwaji huo kwa Uholanzi pamoja na taarifa ya urejeshwaji. Lakini licha ya onyo letu kwamba mtu huyo alikuwa mpiganaji gaidi wa kigeni, serikali ya Ubelgiji haikuweza kutafuta kiunganishi na ugaidi," alisema rais Erdogan akiwa nchini Romania.

Urari kati ya usalama na haki za kiraia

Kisa hiki kinamulika tatizo ambalo Ubelgiji inakabiliana nalo ambapo karibu raia wake 300 wamepigana nchini Syria, idadi kubwa zaidi kutoka Ulaya ikilinganishwa na idadi jumla ya wakaazi wake milioni 11.

Waziri wa mambo ya nje Didier Reinders, akiongoza juhudi za kukabiliana na ukosoaji wa kimataifa kuhusu sera za Ubelgji kupambana na itikadi kali miongoni mwa raia wake wa Kiislamu wanaochangia asilimia tano ya wakaazi wote, alisema lazima kuwepo na urari kati ya usalama na haki za kiraia.

Siku ya Jumanne, mgombea wa urais nchini Marekani Donald Trump, alisema mateso yanaweza kutumiwa kwa wanaoshukiwa kuwa wapiganaji.

Mishumaa iliwashwa kuwakumbuka wahanga wa mashambulio hayo.

Mishumaa iliwashwa kuwakumbuka wahanga wa mashambulio hayo.

Mshambuliaji wa pili kituo cha treni

Mawaziri wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya wanakutana hii leo mjini Brussels kujadili ushirikiano bora, ingawa maafisa wanasema mataifa mengi yanazuwia taarifa zao muhimu licha ya kuwa tayari kushirikiana taarifa za ujasusi.

Wakati huo huo, vyombo vya habari nchini Ubelgji na Ufaransa vikinukuu duru zisizotajwa, vinaripoti kuwa huenda kulikuwepo na mshambuliaji wa pili katika shambulio la kituo cha treni ambaye alitoroka.

Kituo cha utangazaji cha serikali ya Ubelgiji RTBF, na gazeti la Le Monde la Ufaransa, vimesema mshukiwa huyo alikamatwa kwenye kamera akiwa amebeba begi pembeni ya Khalid El Bakraoui.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre/afpe

Mhariri: Elizabeth Shoo

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com