″Msaada uende pamoja na sera bora″ | Magazetini | DW | 18.12.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

"Msaada uende pamoja na sera bora"

Miongoni mwa yale yaliyozingatiwa ni mkutano wa wafadhili kuinua uchumi wa Palestina uliofanyika Paris na taarifa ya rais Putin wa Urusi kwamba anataka kuwa mkuu wa serikali chini ya mgombea wa rais Dimitrj Medwedew.

Washiriki wa mkutano wa wafadhili mjini Paris, Ufaransa

Washiriki wa mkutano wa wafadhili mjini Paris, Ufaransa

Kwanza kuhusu mkutano wa Paris ambao mhariri wa “Frankfurter Allgemeine Zeitung” anauchambua hivi:


“Ni lazima, jumuiya ya kimataifa ijitolee kisiasa na kifedha ili juhudi za kusaka amani Mashariki ya Kati zifanikiwe. Lakini msaada huu kwa Wapalestina utaweza tu kuinua uchumi na hivyo kuwa zaidi ya msaada wa kijamii ikiwa hali ya kisiasa itaruhusu. Yaani ikiwa Waisraeli wataruhusu uchumi wa Palestina ukue badala ya kuudhoofisha na ikiwa Wapalestina wenyewe watachukua hatua badala ya kuzungumzia tu taifa huru.”


Vilevile aliyezingatia mkutano wa wafadhili kwa ajili ya Palestina ni mhariri wa “Süddeutsche Zeitung” ambaye ameandika vifuatavyo:

“Kile kilichojitokeza wiki tatu zilizopita kwenye mkutano wa Annapolis, Marekani, sasa kinaimarika. Kama mwenyeji wa mkutano wa Paris, Rais Sarkozy wa Ufaransa, alivyothibitisha, nchi fadhili zinauunga mkono mpango wa amani wa mfalme Abdullah wa Saudi Arabia kama msingi wa kutatua mzozo wa Mashariki ya Kati. Kwa mujibu wa mpango huu, Waisraeli wanatakiwa wayahame maeneo waliyoyateka ili nalo taifa la Israel litambuliwe na nchi zote za Kiarabu, pia Israel iachane na sera yake ya kujenga makaazi mapya, maeneo ya ukanda wa gaza na ukingo wa Magharibi mwa mto Jordan yaunganishwe, na upatikane mwafaka kati ya serikali ya Fatah na kundi la Hamas linalodhibiti eneo la Gaza.”


Na kwa mada ya pili tunaelekea Urusi ambako rais Putin alitangaza rasmi kwamba anataka kugombea kiti cha waziri mkuu chini ya raisi mpya Dimitrj Medwedew. Katika gazeti la “Stuttgarter” tunasoma hivi:


“Vladimir Putin hajamaliza kazi zake huko Urusi na ana mpango fulani. Kila mara anapozungumza hadharani, anaonekana kama ana nguvu nyingi bado. Huyu si mtu anayeweza kupumzika. Anataka kuendelea kushika mamlaka katika nchi hiyo kubwa na tangu jana basi tunajua atatumia wadhifa gani, yaani ule wa waziri mkuu.”


Mhariri wa “Neue Osnabrücker Zeitung” ana maoni yafuatayo juu ya mpango wa rais Putin:


“Bila shaka, Putin kama waziri mkuu atajiweka chini ya rais kwa picha rasmi tu, lakini kwa kweli hatafuata amri ya rais. Hivyo, Putin atategemea urafiki wake na Medwedew pamoja na mtandao wa marafiki zake wa idara za ujasusi na ushawishi wao katika ikulu. Lakini kweli katiba ya Urusi itaruhusu mamlaka yaende kwa waziri mkuu? Tukumbuke tu historia. Alipochaguliwa kama rais, Putin pia hakuaminika. Hata hivyo, alitumia cheo chake vizuri, na marafiki wa mtangulizi wake Boris Yelzin, baada ya muda mfupi tu, walitoweka.”


 • Tarehe 18.12.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CdJj
 • Tarehe 18.12.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CdJj