Bunge la Uingereza laidhinisha kupelekwa wahamiaji Rwanda
23 Aprili 2024Hatua hiyo imefikiwa baada ya vuta ni kuvute iliodumu hadi usiku wa manane kati ya baraza la juu la bunge la Uingereza - House of Lords na baraza la House of Commons.
Wajumbe wa baraza hilo la juu, ambao hutathmini sheria iliyopendekezwa, walirejesha mara kadhaa mswada huo kwa marekebisho katika chumba cha chini lakini hatimaye waliafiki kuwa mswada huo hauhitaji mabadiliko zaidi, na hivyo kuhakikisha kuwa mswada huo sasa utakuwa sheria.
Siku ya Jumatatu, Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak aliahidi kuanza mnamo miezi michache ijayo, kuwapeleka nchini Rwanda waomba hifadhi wanaowasili nchini humo, kama mpango wenye utata wa serikali ya Uingereza wa kuwapeleka waomba hifadhi nchini Rwanda.
Kuwapeleka wahamiaji Rwanda, ni sehemu muhimu ya majibu ya Waziri Mkuu Sunak katika kukomesha vitendo vya waomba hifadhi kuingia kinyume cha sheria nchini Uingereza.
Mpango wa kukabiliana na idadi ya wahamiaji wanaowasili Uingereza
Wahamiaji hao huhatarisha maisha kwa kutumia usafiri wa boti ndogo wakitokea Ufaransa. Pendekezo la kuwaondoa wahamiaji Uingereza limekabiliwa na utata na changamoto za kisheria tangu aliyekuwa Waziri Mkuu Boris Johnson alipoliwasilisha mwaka 2022.
Idadi ya wahamiaji waliowasili Uingereza kwa boti ndogo iliongezeka hadi kufikia 45,774 mnamo mwaka 2022 kutoka 299 miaka minne iliyopita. Wahamiaji hao huwalipa magenge ya wahalifu maelfu dola ili kuwavusha kwa boti hizo hadi Uingereza.
Soma pia: Mpango wa Uingereza kuwahamishia wakimbizi Rwanda kugharimu pauni milioni 300
Mwaka jana, idadi ya waliowasili kwa boti ndogo nchini humo ilipungua hadi 29,437 wakati serikali mjini London ikipambana vikali na makundi hayo ya wahalifu na kufikia makubaliano ya kuwarejesha Waalbania katika nchi yao.
Mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, Kamati ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa iliitolewa wito Uingereza kuachana na mpango huo wenye utata wa kuwapeleka waomba hifadhi nchini Rwanda, kwa hoja kwamba makubaliano kati ya nchi hizo mbili hayakujali uamuzi wa Mahakama Kuu ya Uingereza iliyosema kuwa mpango huo unakinzana na sheria za kimataifa.
(Chanzo: AP)