1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa Sunak bado unakabiliwa na changamoto chungunzima

Saumu Mwasimba
18 Januari 2024

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak alifanikiwa kuvuka kiunzi cha kambi ya wabunge waasi ndani ya chama chake kuhusu mpango wake wa kutaka kuwahamisha wahamiaji Rwanda kupitishwa bungeni.

https://p.dw.com/p/4bQMP
Rishi Sunak
Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak Picha: James Manning/PA/dpa/picture alliance

Yapo mengi ambayo waziri mkuu huyo wa Uingereza Rishi Sunak anatakiwa kuyakabili kabla ya kufanikisha lengo lake hilo la kuwapeleka Rwanda wakimbizi walioingia Uingereza kwa njia zisizo halali.

Baada ya masaa kadhaa ya mjadala wa kina,wabunge wa Uingereza walipitisha muswaada wa Sunak,unaojulikana kama muswaaada wa Rwanda'' kwa kura 320 dhidi ya 276 za walioupinga na miongoni mwa waliopinga walikuweko pia 11 kutoka kambi ya chama chake cha kihafidhina.

Lengo kubwa la muswaada huo ni kufuta uamuzi uliopitishwa na mahakama ya juu ya Uingereza,ambapo mahakama hiyo mnamo mwezi Novemba mwaka jana ilisema  sera hiyo ya bwana Sunak inakwenda kinyume na sheria.

Muswada wa Sunak wa kuwapeleka wahamiaji Rwanda wapita

Hivi sasa lakini baada ya kupitishwa bungeni muswaada huo unabidi upitie katika baraza la juu la bunge la Uingereza ambako waziri mkuu Sunak hana ushawishi wa moja kwa moja na ambako wajumbe  wengi wa baraza hilo wanaweza kuupinga muswaada huo ambao wanaoukosoa wanasema  huenda ukaitumbukiza Uingereza katika hatua ya kukiuka sheria ya Kimataifa.

Inawezekana wajumbe wa baraza hilo wakajaribu kutaka kuurekebisha muswaada huo hatua ambayo inamaanisha litageuka suala la kuupiga danadana kutoka taasisi moja hadi nyingine.

Mpango huo haukujumuishwa katika manifesto ya chama cha Conservative

Uingereza| Bunge la Uingereza
Rishi Sunak akiwa bungeni Uingereza Picha: UK Parliament/Jessica Taylor/REUTERS

Kawaida wajumbe wa baraza hilo la juu la bunge hujiepusha mara zote kusababisha matatizo katika miswaada iliyopitishwa na bunge, na kwa mujibu wa katiba ya Uingereza muswada uliotajwa katika manifesto ya chama kinachotawala haupaswi kukataliwa katika baraza hilo.

Hata hivyo mpango juu ya kutaka kuwapeleka wahamiaji haramu nchini Rwanda haukujumuishwa katika manifesto ya chama cha Conservative ya mwaka 2019,hivyo basi maana yake ni kwamba wajumbe wa baraza kuu wanaweza kimsingi kukataa kuupitisha muswaada huo ikiwa hautofanyiwa mabadiliko.

Na katika mazingira ya utata mkubwa kama haya yanayoshuhudiwa sasa,huenda ikachukuwa muda mrefu hata mwaka sheria hiyo kupitishwa.Kwa mtazamo huu maana yake ni kwamba inawezekana muswaada huo usipitishwe mpaka baada ya uchaguzi ujao.

Ukitazama hali ilivyo hivi sasa tayari zimeshaonekana dalili za muswaada huo wa Rwanda kupingwa katiba baraza hilo la juu, kamati ya baraza hilo ambayo ina jukumu la kuichunguza mikataba ya kimataifa imeshasema mkataba kati ya serikali ya Uingereza na Rwanda usipitishwe.Kamati hiyo inasema mkataba huo unakosa vigezo vya kiusalama ikiwemo mfumo wa kuzuia watu kutorudishwa katika nchi zao za uzawa ambako wanaweza kuwa katika hatari ya kupata mateso.

Pamoja na hayo waziri mkuu Sunak anasema  muswaada huo ndio wenye mapendekezo makali zaidi ya sheria ya uhamiaji japo wakosoaji wake katika mrengo wa kulia wanasema bado haujakwenda mbali vya kutosha  na kwamba una mapungufu yanayoweza kutumiwa na waomba hifadhi kuzuia kuondolewa nchini Uingereza.