1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Moto unaoangamiza Amazon pia wateketeza Bonde la Kongo

Yusra Buwayhid
28 Agosti 2019

Moto wa Amazon umeanza kusababisha matatizo ya kupumua kwa wananchi wa Brazil, huku shirika la kulinda mazingira Greenpeace likionya kwamba moto pia unaharibu msitu wa Bonde la Kongo barani Afrika.

https://p.dw.com/p/3Objw
Brasilien Waldbrände
Picha: picture-alliance/AP/E. Peres

Serikali ya jimbo la Amazon la Rondonia imeonya kwamba moshi unaotokana na moto huo unaweza kuchafua sana hewa na  kuweka maisha ya wengi hatarini. Na matatizo ya kiafya tayari yameshaanza kujitokeza katika jimbo hilo.

Moshi huo umeshaanza kusababisha wasiwasi kwa wananchi wa Brazil wanaosema matatizo ya kupumua hasa kwa watoto pia yameongezeka kadri moto huo unavyoteketeza eneo hilo la msitu. Idadi ya watu waliotibiwa kutokana na matatizo ya kupumua imeongezeka katika siku za hivi karibuni katika hospitali ya watoto ya jimbo la Rondonia.

Lakini licha ya hayo, suala la moto wa Amazon limetawalia zaidi na mvutano na majibizano ya maneno kati ya Rais wa Brazil Jair Bolsonaro na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron. Bolsonaro awali alidai Macron alimtusi na hatopokea msaada wa G7 hadi Macron amuombe msamaha. Lakini hapo jana alibadilisha kauli yake hiyo kupitia msemaji wake, Otavio Rego Barros, na kusema Brazil  iko tayari kupokea msaada wa kigeni wa kusaidia kuzima moto katika msitu wa Amazon, lakini ikiwa itaweza kuamua jinsi ya kuzitumia fedha hizo.

"Serikali ya Brazil kupitia Rais Jair Bolsonaro iko tayari kupokea msaada wa kigeni, lakini Bolsonaro amesema msaada huo usikiuke uhuru wa nchi na Brazil ndiyo itaamua jinsi ya kuzitumia fedha hizo,” amesema Barros.

Katika mkutano ya kilele wa kundi la mataifa sana yaliyoendelea katika sekta ya viwanda G7, kuliahidiwa msaada wa kifedha wa dola milioni 20, mbali na zilizoahidiwa na Uingereza dola milioni 12 na nyingine dola milioni 11 kutoka Canada.

Soma zaidi: Brazil yakataa msaada wa G7 kuzima moto wa Amazon

Kongobecken Regenwald Nebel Kongo Afrika
Umande katika msitu wa mvua bonde la Congo magharibi.Picha: picture alliance/ WILDLIFE

Lakini Rais wa Brazil Jair Bolsonaro alitilia mashaka msaada huo akidai kwamba ni njama ya kutaka kutumia rasilmali za msitu wa Amazon pamoja na kudhoofisha ukuaji wa kimaendeleo wa Brazil.

Msitu wa Bonde la Kongo pia wateketezwa kwa moto

Wakati hayo yakijiri shirika la kimataifa la ulinzi wa mazingira Greenpeace limezitaka serikali za mataifa yaliyo katika Bonde la Kongo kuchukua hatua zaidi kupambana na moto wa msitu wa Afrika ya kati, katika wakati ambapo ulimwengu umeelekeza macho yake katika moto unaoteketeza msitu wa mvua wa Amazon huko Brazil.

Msitu ya Bonde la Kongo - sehemu inayofunika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Gabon, Kongo-Brazzaville na Cameroon - unashika nafasi ya pili duniania baada ya msitu wa Amazon.

Kama ilivyo kwa msitu wa Amazon, msitu wa bonde la Kongo unachangia kusafisha hewa chafu ya kaboni kwa kiasi kikubwa na ni njia muhimu kwa mujibu wa wataalamu ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Soma zaidi: Maoni: Macron aitumia G7 kuthibitisha umahiri wa diplomasia

Chanzo: (ap,afp)