Mkuu wa MONUSCO aitembelea Goma
24 Aprili 2026
Mnamo mwezi Februari uliopita, naibu wa mkuu huyo wa Monusco, Viviane Van de Perre aliutembelea mji wa Goma kwa ajili ya kuanzisha timu ya utaratibu wa kuthibitisha usitishaji mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Akiwasili tu katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Goma, James Swan alisema kuwa amekuja kutekeleza utaratibu huo wa usitishaji vita.
"Ziara hii ni sehemu muhimu ya juhudi za kutekeleza usitishaji mapigano. Kama mnavyojua, Goma ina nafasi ya kipekee katika juhudi za kupunguza mvutano, kulinda raia, na kusaidia mchakato wa amani unaoendelea.”
James Swan amekuja kukutana na timu za Umoja wa Mataifa, kusikiliza tathmini zao, kubadilishana mawazo na mamlaka zilizopo, na pia kuchunguza mazingira halisi ambayo MONUSCO inaweza kuendelea kutekeleza wajibu wake kulingana na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Katika utaratibu huo wa usitishaji mapigano, MONUSCO inaonekana kama nguvu ya upande wa kati, pamoja na kutoa msaada wa vifaa, kufuatia makubaliano ya hivi karibuni ya Montreux, yenye lengo la kusaidia mchakato wa amani na kuvunjwa kwa uasi wa AFC/M23.
Hata hivyo, kinyume na matarajio, wakazi wa Goma bado wako katika hali ya sintofahamu kutokana na mgogoro unaoendelea bila dalili ya kumalizika. Kwa mujibu wa mchambuzi huru Philémon Ruzinge, serikali ya Kongo inapaswa kuongeza juhudi zake katika kutafuta amani badala ya kutegemea sana MONUSCO.
"Kwa maoni yangu, kuwasili kwake hakutakuwa na athari kubwa sana, lakini ni habari njema. Wananchi wanahitaji mwisho wa vita, uwepo wa dola, kufungwa kwa makundi yenye silaha, kufunguliwa kwa benki na uwanja wa ndege. Wanahitaji uwajibikaji wa viongozi wao. Si jukumu la mwakilishi wa MONUSCO kumaliza vita hii, bali ni la serikali ya Kongo.”
Mkuu wa Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo,MONUSCO, James Swan amesisitiza kuwa utekelezaji wa usitishaji mapigano unahitaji masharti muhimu kutimizwa.
"Ufuatiliaji wa usitishaji mapigano unahitaji kuwepo kwa masharti muhimu ili utaratibu wa pamoja wa uthibitishaji uweze kufanya kazi kwa ufanisi, kwa usalama na kwa kuaminika. Masharti hayo ni pamoja na kusitishwa kwa matumizi ya ndege zisizo na rubani za kivita, kukomesha kuvurugwa kwa ishara za GPS, uhuru kamili wa harakati za wafanyakazi wa MONUSCO pamoja na matumizi salama ya viwanja vya ndege na anga.”
James Swan amefanya kikao cha mazungumzo na viongozi wa uasi wa AFC/M23 mara tu baada ya kuwasili katika mji wa Goma, kwa ajili ya kubadilishana mawazo na kujadili matarajio.