1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa G7 unafanyika Ufaransa

Grace Kabogo
24 Agosti 2019

Viongozi wa kundi la nchi saba tajiri kabisa dunaini - G7 wanaanza leo mkutano wao wa kilele kusini magharibi mwa Ufaransa.

https://p.dw.com/p/3OQFX
G7 Frankreich
Picha: Imago Images

Suala la kutetekea msitu wa Amazon, kutikisika kwa masoko ya hisa na tofauti kubwa zilizopo baina yao ni mambo yanayotarajiwa kutawala ajenda ya mazungumzo yao.

Rais wa Marekani, Donald Trump na viongozi wenzake wa nchi za Magharibi pia watakabiliwa na maandamano wakati wakiwasili katika mji wa Biarritz, ijapokuwa idadi kubwa ya polisi imeweka doria kuzuia vurugu.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron ambaye ndiye mwenyeji wa mkutano huo wa G7 ameongoza sauti za viongozi wa kimataifa katika kumuekea shinikizo Rais wa Brazil, Jair Bolsonaro kuhusiana na moto unaoendelea kuutekeza msitu wa Amazon, akimwambia kuwa Ufaransa itazuia juhudi za kufikia makubaliano muhimu ya kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya na Amerika Kusini.