1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano kuhusu uchumi wa Buluu wafanyika visiwani Zanzibar

Salma Said22 Mei 2023

Wakati dunia ikishuhudia athari za mabadiliko ya tabia ya nchi, kupunguwa kwa uzalishaji wa chakula, nchi zilizo kwenye Mwambao wa Bahari ya Hindi zinakutana visiwani Zanzibar kujadili uwekezaji katika Uchumi wa Buluu.

https://p.dw.com/p/4RfPO
Sansibar | President Dr Hussein Mwinyi
Picha: Shisia Wasilwa/DW

Mdahalo huo wa tisa umehudhuriwa na washiriki zaidi ya mia moja wakiwemo wataalamu wa masuala ya sayansi ya Bahari kutoka Jumuiya ya nchi za Mwambao wa Bahari ya Hindi, IORA, kwa lengo la kuimarisha uhusiano hasa katika kutatua matatizo yanayojitokeza katika uchumi baada ya pigo la janga la maradhi ya Covid-19 lililosambaratisha uchumi katika nchi kadhaa hasa za kusini kwa jangwa la sahara.

Mkutano huu ni sehemu ya maazimio yaliofikiwa Nairobi iliyoagiza nchi wanachama wa IORA kuwekeza katika Bahari katika suala la kuimarisha uvuvi, usafirishaji, uendelezaji wa mafuta na gesi asilia Pamoja na kilimo cha mwani na ufugaji wa tano Bahari ambapo wanufaika ni wanawake na vijana hasa katika kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira.

Akifungua katika kongamano hilo Makamo wa kwanza wa Rais Makamo wa Rais Othman Masoud Othman alihimiza ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama wa IORA katika kufikia malengo ya uchumi wa buluu ambayo ni miongoni mwa vipaumbele vya nchi ya Tanzania.

Soma pia: Guterres:Tuwajibike ili kuwa na dunia salama

"Nina hakikamtakubaliana nami kuwa njia ya kutufikisha katika uchumi endelevu wa buluu itategemea juhudi zetu za Pamoja katika uchumi, jamii, mazingira, na utashi wa kisiasa ili tufanikiwe kufika tunapotaka kwa manufaa ya watu wetu na utunzaji wa bahari”.

USA, Florida | kubanisches Flüchtlingsboot
Picha: David Goodhue/Miami Herald/ZUMA/picture alliance

Mkurugenzi wa uchumi wa buluu na uvuvi katika  sekretariet IORA Bi Rina Setyawati amesema tangu kuanza kwa jumuiya hiyo changamoto za Bahari zimekuwa zikitatuliwa kwa njia za ushirikiano na wadau wa jumuiya za kimataifa.

Setyawati  aliipongeza  Tanzania kwa utekelezaji wa miradi kadhaa iliyo chini ya jumuiya hiyo ya IORA waliokubaliana kufanyia kazi kama kundi ili kufikia lengo la uchumi wa buluu.

 "Tuna matumaini IORA iko tayari kuendelea kufanya kazi na Tanzania katika kushajiisha uchumi wa buluu katika eneo letu la bahari ya hindi”.

 Akizungumza katika kongamano hilo la tisa Katibu mkuu wa uchumi wa buluu Zanzibar Aboud Suleiman Jumbe amesema inawaamsha nchi wanachama katika ili kuchukua hatua za kuimarisha na kuhifadhi Bahari na kuwawezesha wananchi katika uchumi wa buluu.

Soma pia: Nchi za Afrika kufikiria kuwekeza katika mipango ya mazingira

 Ametoa wito kwa washiriki wa mkutano huo kujadiliana na kutoa uzoefu wa uchumi wa buluu katika nchi zao ili kwenda pamoja na kufikia malengo endelevu.

Kando ya mkutano huo Aboud ameelezea maazimio ya Nairobi yalivyotekelezwa katika nchi wanachama na ilivyosaidia kusogeza mbele masuala ya uchumi.

Washiriki wa Jumuia hiyo na wadau kutoka bara la Ulaya na Asia wanashiriki mkutano wa tisa wa majadiliano wa siku siku mbili katika jiji la Zanzibar