1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Jemen Sanaa | Saudi-geführte Luftangriffe auf Häuser
Picha: Hani Mohammed/AP Photo/picture alliance

Mjumbe Maalum wa Yemen ataka usitishwaji mapigano urefushwe

16 Agosti 2022

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen Hans Grundberg amesema anafanya juhudi za kurefusha zaidi muda wa makubaliano ya kusitisha mapigano nchini humo, ili kufungua njia ya kuanza tena mazungumzo ya kumaliza vita.

https://p.dw.com/p/4FZgG

Mwanadiplomasia huyo anayemwakilisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika mzozo wa Yemen, ameelezea nia hiyo wakati alipolihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutoa tathmini ya hali ya mambo nchini Yemen.

Bw. Grundberg amesema amedhamiria kuzishawishi pande hasimu nchini Yemen kurefusha zaidi muda wa kusitisha mapigano kwa lengo la kutoa nafasi ya kukomeshwa vita na kurejea kwa mpango wa kuutafutia suluhu mzozo wa Yemen kwa njia ya kisiasa.

Amesema dhamira iliyokwioneshwa na pande hasimu nchini humo ya kuendelea na majadiliano ya kurefusha muda huo ni nafasi muhimu ya kuusaidia umma wa Yemen unaokabiliwa na mzozo mkubwa wa kibinadamu.

Grundberg aonya juu ya taathiria za kutorefushwa muda wa kusitisha mapigano 

Mnamo Agosti 2, serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa ilifikia makubaliano na waasi wa Houthi ya kuendeleza usitishaji mapigano ulioanza mnamo mwezi Aprili kwa muda wa miezi miwili zaidi.

UN-Sondergesandter für Jemen Hans Grundberg
Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, Hans Grundberg Picha: Fayez Nureldine/AFP

Mwafaka huo unaaminisha pande hizo hasimu zitaendelea kujizuia kushambuliana hadi mwanzoni mwa Oktoba.

Muda huo wa usitishaji mapigano ndiyo mrefu zaidi kuwahi kuafikiwa tangu kuanza kwa vita nchini Yemen mnamo mwaka 2014.

Pande hizo hasimu pia zimeafiki kuendeleza majadiliano yatakayowezesha kupatikana makubaliano mengine ya kusitisha mapigano baada ya Oktoba 2.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Bw. Grundberg ameonya iwapo mwafaka hautapatikana, hilo litakuwa janga kwa umma wa Yemen.

Grundberg amesema "Kushindwa kufikia makubaliano ya kurefusha usitishaji huu wa muda wa mapigano kutasababisha awamu nyingine ya machafuko, itakayokuwa na taathira za kutisha na zinazotabirika kwa watu wa Yemen. Yemen inahitaji kuzuia hilo lisitokee. Na ninazirai pande zote kuchukua mkondo wa kujenga imani itakayozuia kurejea kwa vita huku tukielekea kujenga amani ya kudumu".

Tathmini yaonesha usitishaji wa mapigano unafanya kazi 

Katika tathmini yake ya miezi minne na nusu ya mwafaka wa kusitisha mapigano, Bw. Grundberg amesema, makubaliano hayo yanaonesha kufanya kazi.

Jemen Sanaa | Kinder spielen
Picha: Mohammed Mohammed/Xinhua/picture alliance

Amearifu kwamba hadi sasa hakuna operesheni zozote kubwa za kijeshi zilizoshuhudiwa na wala hakujaripotiwa mashambulizi yoyote ya anga nchini Yemen au hujuma za kuvuka mpaka kutokea Yemen.

Pia amegusia jinsi usitishaji wa mapigano ulivyopunguza idadi ya watu wanaopoteza maisha kwenye mzozo huo.  Hivi karibuni  Grundberg aliyatembelea maeneo yanayodhibitiwa na pande hasimu na kufanikisha kufunguliwa kwa barabara muhimu za majimbo kadhaa ikiwemo huko Taiz.

Kuna ripoti pia kwamba meli 33 ziliruhuisiwa kutia nanga katika bandari ya Hodeida na kupakua shehena ya karibu lita milioni moja za mafuta. Usafiri wa anga nao umeimarika kwa sehemu fulani.

Kumekuwa na safari 31 za ndege kati ya  mji mkuu Sanaa, unaodhibitiwa na waasi wa Houthi na mji mkuu wa Jordan, Amman zilizosafirisha zaidi ya abiria 15,000.