1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, mkataba wa wakimbizi wa UN bado una tija?

Angela Mdungu
28 Julai 2021

Ni miaka 70 tangu kusainiwa kwa mkataba wa Umoja wa Mataifa ya kuwalinda wakimbizi. Licha ya mkataba huo kuwa wa miaka mingi, wataalamu wanasema bado hadi sasa hakuna nia ya dhati ya kisiasa ya kulinda haki za wakimbizi.

https://p.dw.com/p/3yB09
Kenia Das Flüchtlingslager Dadaab
Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Mkataba wa kuwalinda wakimbizi wa Geneva ni wa msingi katika kuwalinda wakimbizi. Unaeleza mkimbizini mtu wa namna gani na ni haki zipi na wajibu walio nao.

Watu walioondoka nchini mwao kutokana na "hofu ya kuteswa kutokana na rangi zao, dini, utaifa, uanachama wao katika kundi fulani la kijamii ama kutokana na misimamo yao ya kisiasa” kama ilivyoainishwa kwenye maandishi ya mkataba huo, wana haki ya kuwa kwenye kundi hilo.

Kutokana na vita ya pili ya Dunia na kukua kwa mivutano; Umoja wa Mataifa ulipitisha makubaliano hayo mjini Geneva mwaka 1951. Mwanzoni, hata hivyo mkataba huu ulijikita kuwalinda baadhi ya watu pekee hasa wakimbizi wa Ulaya mara baada ya vita ya pili ya dunia.

Ili kutenda haki kutokana na mabadiliko ya hali halisi duniani kote, makubaliano yalitanuliwa mwaka 1967, na nchi 149 zimetia sahihi moja ya mikataba au yote miwili.

Schweiz | Genfer Konvetionen
Nakala ya mkataba wa Geveva wa mwaka 1949.Picha: T. Gassmann (ICRC)

Wakimbizi hupokea haki zao

Akizungumza na DW mchambuzi kutoka taasisi ya sera za uhamiaji wa mjini Brussels Susan Fratzke anasema hata sasa, mkataba huo una jukumu muhimu kwani ndiyo waraka pekee unaozitaka nchi ziwalinde wakimbizi.

Soma pia: Umoja wa Mataifa wasema wakimbizi wameongezeka maradufu katika muongo mmoja

Suzan anasema leo hii watu wanalazimika kuhama makazi yao kwa sababu mbalimbali kuliko wakati wa vita baridi. 

"Mkataba huu haujitekelezi wenyewe. Hii inamaanisha kuwa serikali zinazotia sahihi zinapaswa kuzitimiza ahadi zao wanazozitoa kwenye mkataba huo katika sheria za nchi zao.

Na nchi nyingi hufanya hivi kupitia sheria ya kuomba hifadhi inayoonesha ni nani inamtambua kama mkimbizi na ni haki zipi alizonazo kwa kuzingatia makubaliano ya mkataba," alisema Fratzke.

Naye Abiy Ashenafi, mkuu wa ofisi ya uhamiaji katika kituo cha haki za binadamu cha chuo kikuu cha Pretoria nchini Afrika ya Kusini anafikiri kuwa Umoja wa nchi za Afrika haujaelezea baadhi ya mapungufu kwenye maana hasa ya neno mkimbizi.

Anasema tatizo kwenye mkataba huo ni kuwa hautoi utaratibu wa malalamiko kwa wakimbizi dhidi ya nchi zinazowapokea.

Kulinda haki za binadamu ni jambo analolipenda Hamado Dipama aliyewahi kuwa mkimbizi. Amejitolea kufanya hivyo tangu alipokimbia machafuko ya kisiasa nchini mwake Burkina Faso.

Symbolfoto Visum / BAMF
Shirika la UNHCR ndiyo linahusika na huduma kwa wakimbizi kote duniani.Picha: Geisler-Fotopress/picture alliance

Takribani miaka 20 iliyopita wakati akiwa bado mwanafunzi yeye na wengine wengi walipinga udikteta wa Rais Blaise Compaore aliyeitawala nchi hiyo kwa mkono wa chuma kwa miaka 27 hadi pale alipopinduliwa kupitia maandamano ya mwaka 2014. Alijikuta akiishia katika mji wa Munich wa jimbo la Bavaria, Ujerumani ambako sasa anapaita nyumbani.

Soma pia: Kenya yatoa siku 14 kuzifunga kambi za wakimbizi

"Wakati nilipokuwa nakimbia machafuko, sikujua kuhusu makubaliano ya wakimbizi ya Geneva. Hili sio suala la nchi masikini, watu kule wana taarifa kidogo kuhusu hili. Hilo ni pengo. Ni pale tu nilipofika Ujerumani ndipo nilipoanza kukumbana nalo. 

Kwa sababu kwa wakati ule nilikataliwa. Ni kwa nini watu wengine walindwe lakini si mimi? Ingawa nilikuwa naweza kueleza kuhusu hali yangu Burkina Faso, kuwa niliteswa nikiwa mwanafunzi katika vuguvugu dhidi ya dikteta Blaise Compaoré, hiyo yote haikusaidia."

Hamado Dipama anakosoa taratibu zinazokwenda kinyume na makubaliano ya Geneva

Mara nyingi anaona suala la kurudishwa nyumbani kwa lazima kuwa si sahihi. Kwa mfano wakati watu walioishi Ujerumani muda mrefu na kisha wanarudishwa kwenye nchi zao ambazo bado hazijawa imara.

Dipama anafahamu hofu ya kurejeshwa nyumbani. Aliishi kama mkimbizi kwa miaka tisa na alipambana na hilo. Alipata hati ya ukaazi mnamo mwaka 2014.

Soma pia: UN yaeleza namna wakimbizi wanateseka kwenye mipaka ya Ulaya

Mwezi mmoja uliopita alituma maombi ya kupatiwa uraia anasema haikuwa rahisi kwa sababu anapaswa kuirudisha paspoti yake ya Burkina Faso.

Tangu mwaka 2017 amekuwa msemaji wa baraza la wakimbizi la Bavaria na ameanzisha kikundi cha watu wenye asili ya Afrika kinachopigania maslahi ya watu weusi.

Anasema mataifa yanapaswa kufanya yalichotia sahihi kwenye mkataba wa kuwalinda wakimbizi na kufanya marekebisho ili wakimbizi wapate ulinzi zaidi kutoka kwenye mataifa yenye matatizo.