Umoja wa Mataifa wasema wakimbizi wameongezeka maradufu katika muongo mmoja | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.06.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Umoja wa Mataifa wasema wakimbizi wameongezeka maradufu katika muongo mmoja

Umoja wa Mataifa katika ripoti yake unataka hatua zichukuliwe kutokana na kuongezeka idadi ya watu wanaokimbia mizozo na mateso huku janga la COVID-19 linapoendelea kuutesa ulimwengu.

Kulingana na Kamishna Mkuu wa shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) Fillipo Grandi, idadi ya watu wanaoyakimbia makaazi yao kwa sababu ya mateso, mizozo, vurugu, na ukiukaji wa haki za binadamu imeongezeka hadi kufikia watu milioni 82.4, hilo likiwa ni ongezeko la asilimia 4 kulinganisha na takwimu za mwishoni mwa mwaka 2019. Bwana Grandi amesema wakimbizi wanastahili msaada wa kimataifa sio tu kupitia misaada ya dharura ya kibinaadamu bali kwa ulimwengu kutafuta suluhisho la kudumu litakalomaliza shida za wakimbizi. Grandi pia ameitaja migogoro ya muda mrefu katika nchi za Syria, Afghanistan, Somalia na Yemen na jinsi inavyochochea ongezeko la wakimbizi.

Wakimbizi katika kambi ya Karatepe katika kisiwa cha Lesbos nchini Ugiriki

Wakimbizi katika kambi ya Karatepe katika kisiwa cha Lesbos nchini Ugiriki

Ripoti hiyo pia imebainisha kuwa janga la corona lilipofika kileleni mnamo mwaka 2020, zaidi ya nchi 160 zilifunga mipaka yake wakati nchi 99 hazikuwashughulikia kabisa watu waliotafuta hifadhi kwenye nchi mbalimbali duniani. Hata hivyo pamoja na kuwekwa hatua zilizoboreshwa kama vile uchunguzi wa matibabu kwenye mipaka, vyeti vya afya au karantini za muda mfupi mara tu wakimbizi walipowasili, taratibu za usajili zilizorahisishwa na kusikilizwa wakimbizi kwa njia video, nchi nyingi ziliweza kufaulu kuwawezesha wakimbizi hao kupata hifadhi na wakati huohuo hatua za kuzuia kuenea kwa virusi vya corona zilizingatiwa.

Watoto wanaathirika zaidi

Kulingana na ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa kuhusu kuongezea kwa idadi ya wakimbizi, watoto ndio wanaathiriwa zaidi hasa wakati familia zinapolazimika kuhama makaazi yao na kuendelea kuishi uhamishoni kwa miaka mingi inayofuata.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa karibu watoto milioni 1 walizaliwa kama wakimbizi kati ya mwaka 2018 na mwaka 2020. Ripoti hiyo imesema asilimia 42% ya wakimbizi ni wasichana na wavulana walio chini ya umri wa miaka 18. Wengi wao wako katika hatari ya kuendelea kuishi uhamishoni kwa miaka ijayo na kwa wengine huenda wakaishi uhamishoni maisha yao yote.

Fillipo Grandi, Kamishna Mkuu wa shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR)

Fillipo Grandi, Kamishna Mkuu wa shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR)

Uturuki ndio mwenyeji mkuu wa wakimbizi ulimwenguni ina jumla yao wakimbizi milioni 3.7, ikifuatiwa na Colombia kwa kuwa na wakimbizi milioni 1.7, Pakistan na Uganda zina wakimbizi milioni 1.4 kila mmoja na Ujerumani ina jumla ya wakimbizi milioni 1.2.

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia maswala ya wakimbizi, Filippo Grandi amesema mgogoro wa watoto wengi waliozaliwa uhamishoni na si kwa hiari yao unapaswa kuwa sababu ya kutosha ya kuongeza juhudi za kusuluhisha mizozo na vurugu kwenye nchi mbalimbali.

Chanzo: https://p.dw.com/p/3v7Kr