Mgombea wa upinzani aongoza matokeo ya uchaguzi Tunisia | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.09.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Watunisia waamua kumchagua mgombea wa upinzani

Mgombea wa upinzani aongoza matokeo ya uchaguzi Tunisia

Asilimia 27 ya kura zimehesabiwa kwa mujibu wa tume ya uchaguzi na Kais Saed anaongoza katika duru ya mwanzo ya uchaguzi wa rais uliofanyika Jumapili na ulioshuhudia vijana wengi kutojitokeza kupiga kura

Wagombea wawili kutoka upinzani nchini Tunisia ndio wanaosemekana kuongoza katika uchaguzi wa Jumapili ambao ni wa duru ya mwanzo. Ulikuwa ni uchaguzi wa pili huru uliofanyika kwa njia za kidemokrasia tangu vuguvugu la kudai demokrasia lililopiga katika nchi nyingi za kiarabu mwaka 2011.

Kwanza kabisa dalili zilizoonekana katika uchaguzi wa Tunisia ni wananchi kukosa hamasa na hamu ya kushiriki kwenye zoezi hilo na hali hiyo hasa imeonekana miongoni mwa vijana.Tume ya uchaguzi inasema waliojitokeza kupiga kura ni asilimia 45 ya Watunisia idadi ambayo ni ndogo ikilinganishwa na duru ya kwanza ya  uchaguzi uliofanyika mwaka 2014 ulioshuhudia asilimia 64 ya wapiga kura. Katika kambi ya mgombea huru Kais Saeid mwenye umri wa miaka 61  profesa wa sheria  na mtalaamu wa masuala ya katiba,tayari wanasherekea ushindi.

Tume ya uchaguzi imesema Kais Saed anaongoza mpaka sasa baada ya asilimia 27 ya kura kuhesabiwa.Hayo ni matokeo ya  awali kabla ya matokeo kamili ya mwanzo yanayotarajiwa kutangazwa kesho Jumanne. Lakini pia katika makao makuu ya chama cha mgombea tajiri anayemiliki kituo cha televisheni Nabil Karoui aliyezuiliwa jela kufuatia tuhuma za kuhusika na utakatishaji fedha shangwe zilitawala

Mamia ya wafuasi wake wanashangilia baada ya kudai pia ameshinda na amefanikiwa kuingia katika duru ya pili ya uchaguzi. Hatem Mlikimsemaji wa timu ya Kampeni ya Karoui amesikika akisema hivi.

"Tunafuraha kwasababu bwana Nabil Karoui amefanikiwa kuingia duru ya pili kwa mujibu wa hesabu zetu tulizokusanya''

Wagombea wengine maarufu katika duru hiyo ya kwanza walikuwa ni AbdelFattah Mourou  akiwania kupitia  chama cha kiislamu cha  Ennahda  pamoja na waziri mkuu Youssef Chahed. Chama cha Ennahda kinasisitiza kitasubiri kuona matokeo yatakayotangazwa na tume.

Umaarufu wa Chahed umetiwa doa na hali mbaya ya kiuchumi pamoja na kupanda kwa gharama ya maisha nchini Tunisia.Waziri mkuu huyo pia amelazimika kukanusha tuhuma kwamba kukamatwa kwa Karoui tangu mwishoni mwa mwezi Agosti zilikuwa njama za serikali zilizochochewa kisiasa.

Uchunguzi wa maoni umeonesha kwamba kushikiliwa jela kwa Karoui siku kumi tu kabla ya kampeini ya uchaguzi huo wa jumapili ni suala lililotawala sana na kuchukua nafasi kubwa katika uchaguzi na ndiko kuliko mpa umaarufu zaidi.

Karoui mfanyabiashara anayeonekana kuwa mwenye utata alijijengea jina kupitia televisheni yake ya Nessam kwa kuanzisha kampeni kubwa ya kutoa msaada akihusika kugawa msaada wa chakula kwa baadhi ya wananchi masikini kabisa wa Tunisia.

Lakini wapinzani wake wanampa sifa ya kuwa mtu mwenye tabia sawa na  waziri mkuu wa zamani wa Italia Silvio Berlusconi. Katika uchaguzi wa jana kiasi walinda usalama 70,000 walipelekwa kwenye vituo vya kupigia kura. Matokeo kamili ya awali yanatarajiwa kutangazwa kesho lakini pia tarehe ya duru ya pili ambayo ni ya mwisho kati ya wagombea wawili watakaoibuka washindi wa duru ya mwanzo haijatangazwa ingawa duru hiyo ya pili inapaswa kufanyika kufikia Oktoba 23.

Mwandishi Saumu Mwasimba

Mhariri : Gakuba, Daniel

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com