Mgogoro wa Uturuki utaingia Ujerumani? | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.11.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mgogoro wa Uturuki utaingia Ujerumani?

Hasira na hali ya kukata tama viliwachochea Wakurdi wengi wanaoishi Ujerumani kuandamana Berlin, Cologne, Dortmund na Hanover. Maandamano hayo yanahusiana na kukakamatwa kwa wanasiasa wa Kikurdi kutoka chama cha HDP

Mamia ya watu walijiunga katika maandamano kuhusu kfungwa jela wanasiasa wa Kikurdi Selahattin Demirtas na Figen Yuksekdag kutoka chama cha Peoples Democratic Party – HDP.

Maelfu walielezea malalamiko yao kwenye mitandao ya kijamii. "hili ni tangazo la mwisho la Erdogan la vita dhidi ya Wakurdi," alisema Ali Ertan Toprak, kiongozi wa jamii kubwa ya Wakurdi nchini Ujerumani wakati akizungumza na DW:

Wanasiasa hao wamekuwa katika mgogoro na serikali ya Uturuki tangu ilipoanza kuwafunga jela watu 30,000 ambao iliwaita kuwa "maadui wa serikali” kufuatia jaribio la lililoshindikana la maponduzi ya kijeshi mwezi Julai. Serikali ya Ankara inakishutumu chama cha kiliberali cha siasa za mrengo wa shoto HDP kwa kukiunga mkono chama kilichopigwa marufuku cha Wafanyakazi wa Kikurdi – PKK na hivyo kuunga mkono ugaidi. Chama hicho kinakanusha madai hayo. Hata hivyo, katika wiki chache zilizopita, wanasiasa wa Kikurdi wanaotofautiana wameondolewa ofisini, wanahabari wameteswa na vyombo vya habari vyenye mafungamano na Wakurdi vimefungwa. Mafanikio ya uchaguzi ya chama cha HDP mwaka jana yalikifanya kuwa nguvu ya kisiasa nchini Uturuki na Demirtas kuwa mmoja wa mahasimu wakuu wa Erdogan.

Wenyekiti wenza wa chama cha HDP Selahattin Demirtas na Figen Yuksekdag

Wenyekiti wenza wa chama cha HDP Selahattin Demirtas na Figen Yuksekdag waliokamatwa na serikali

'Kuibiwa nafasi za kidemokrasia'

Toprak anasema Demirtas sio tu ishara ya matumaini kwa Wakurdi nchini Uturuki na Ujerumani bali pia wanademokrasia wa Uturuki. "kwa kuwafunga jela wanasiasa wa Kikurdi waliochaguliwa kidemokrasia waliojitolea katika kutafuta suluhisho la amani kwa suali la Kikurdi, serikali imewapora Wakurdi maamuzi ya kidemokrasia”.

Hivyo Erdogan anawapeleka Wakurdi mikononi mwa PKK. Toprak anaonya kuwa: "sasa mzozo huu utaendelea kwa njia za machafuko – na hata uwezekano wa kuwa mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa katika miongo kadhaa iliyopita”.

Ana uhakika kuwa hali hii "itaingia Ujerumani, ambako Waturuki na Wakurdi wanaishi”. Wakati anazungumzia Waturuki na Wakurdi nchini Ujerumani, anazungumza kuhusu watu milioni 1.5 – wasiofungamana na dini, Waislamu, wahafidhina na waliberali. Jamii ya Waturuki wanaoishi ng'ambo imegawika kama tu ilivyo jamii yenyewe ya Waturuki walioko nyumbani. Hakuna anayefahamu hilo zaidi kuliko Gokay Sofuoglu, mwenyekiti wa Jamii ya Waturuki nchini Ujerumani, shirika la mwamvuli lenye vyama 270.

Türkei Kurden demonstrieren in Istambul (picture-alliance/dpa/S. Suna)

Polisi wazima maandamano ya waufuasi wa chama cha HDP mjini Istanbul kuunga mkono uhuru wa habari

Kioo cha jamii ya Kituruki

"Sera za ndani za Uturuki zinaonekana wazi nchini Ujerumani,” Sofuoglu anaendelea. Ukweli kwamba migogoro ya kindani ya Uturuki inaonekana katika jamii ya Kituruki nchini Ujerumani umejitokeza kwa miaka mingi kutokana na maandamano makuu ya kumuunga mkono na kumpinga Erdogan, maandamano ya AKP na hata wakati wa uchaguzi kurejea nyumbani kwa Waturuki wanaoishi Ujerumani.

Mwenendo mmoja, zaidi ya kingine, ni wazi: Wajerumani wengi wenye mizizi ya Kituruki bado wanaitambua nchi yao ya asili. Katika uchaguzi wa bunge nchini Uturuki ulioandaliwa Novemba 2015, asilimia 60 ya Waturuki wanaoishi Ujerumani walikipigia kura chama chake cha Justice and Development - AKP.

'Wanaitwa magaidi'

"Kuna makundi ndani ya jamii ya Kituruki nchini Ujerumani ambayo yanatetea kila kitu afanyacho Erdogan kwa sababu yanatamani Uturuki tofauti,” anaeleza Toprak. Anasema Erdogan anaielekeza nchi hiyo kwa udikteta wa uislamu wa itikadi kali. Na wafuasi wengi wa Erdogan wanaona kinachofanyika sasa kuwa ni "hatua muhimu kueleeka kutimiza lengo hilo”. Mkuu wa jamii ya Wakurdi nchini Ujerumani anaongeza kuwa: wale wenye mawazo tofauti "wanaitwa magaidi na kushughulikiwa hivyo”.

Waandamanaji wa Kikurdi mjini Cologne, Ujerumani

Waandamanaji wa Kikurdi mjini Cologne, Ujerumani

'Ulimwengu umesalia kimya'

Toprak na Sofuoglu wanatabiri kuwa kutakuwa na maandamano kadhaa katika siku kadhaa zijazo. "Wakurdi na Waturuki wapenda demokrasia watataka kuoa maoni yao". Alieleza Sofouglu. "hilo litaufikisha mgogoro huo kwa jamii ya Waturuki nchini Ujerumani. Toprak anaendelea kusema: "kama wazalendo wa Uturuki watamiminika barabarani katika siku chache zijazo na kutoa wito wa kuwapo maandamano pinzani, hauwezi kufuta uwezekano kuwa kutakuwa na maandamano Ujerumani”. Anasisitiza "Wakurdi wamekata tama kwa sababu wawakilishi wao waliochaguliwa kidemokrasia wamekamatwa na ulimwengu hausemi lolote kuhusu hilo.” Kama watu watapata hisia kuwa hakuna anayewasikiliiza huenda ikasababisha matendo yasiyofikiriwa.

Toprak anasema serikali ya Ujerumani ina wajibu maalum wa kutuliza hali kwa "kwa kulaani vikali vitendo vya Erdogan”. Matakwa ya Wakurdi ni wazi: kusitishwa maramoja mazungumzo ya uwanachama wa Umoja wa Ulaya na Uturuki, kusitisha msaada wote wa kiuchumi na kusitisha mauzo ya silaha.

Mwandishi: Bruce Amani/DW
Mhariri: Iddi Sessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com