Merkel, Karzai wazungumzia usalama Afghanistan | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.01.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Merkel, Karzai wazungumzia usalama Afghanistan

Kansela wa Ujerumani Angela alifanya mazungumzo na rais Hamid Karzai kuhusu ushiriki wa Ujerumani nchini Afghanistan mwaka huu, na uwezekano wa kusogeza muda wa uwepo wa vikosi vya Ujerumani nchini humo baada ya 2014.

Kansela Angela Merkel na rais Hamid Karzai.

Kansela Angela Merkel na rais Hamid Karzai.

Msemaji wa serikali ya Ujerumani aliiambia DW kuwa Afghanistan ni moja ya vipaumbele vya Kansela Merkel kwa mwaka huu wa 2014, na hivyo mazungumzo kati yake na rais Karzai yalijikita katika ushiriki wa Ujerumani na jumuiya ya kimataifa nchini Afghanistan mwaka huu, na uwezekano wa kusogeza ushiriki huo zaidi ya mwaka huu.

Mazungumzo hayo pia yaliangazia hali ya usalama inayozidi kudorora katika eneo linalosimamiwa na wanajeshi wa Ujerumani kaskazini mwa Afghanistan, ambako kumekuwa na ongezeko katika matukio yanayotishia usalama, yakiwemo mashambulizi dhidi ya vikosi vya kimataifa na vya Afghanistan, na pia miripuko ya mabomu na ufyatuaji risasi.

Kansela Merkel alipowatembelea wanajeshi wa Ujerumani walioko nchini Afghanistan.

Kansela Merkel alipowatembelea wanajeshi wa Ujerumani walioko nchini Afghanistan.

Usalama hautabiriki
Kwa mujibu wa kamanda wa operesheni za vikosi vya Ujerumani, jumla ya matukio 1660 ya kiusalama yalirekoidwa kuanzia Januari hadi Novemba 2013, ikilinganishwa na jumla ya matukio 1228 katika mwaka mzima wa 2012. Wanajeshi wa Ujerumani walikuwa mkoani Kunduz kwa zaidi ya miaka 10. Oktoba mwaka jana, aliekuwa waziri wa ulinzi Thomas die Maiziere, na wa mambo ya kigeni Guido Westerwelle, walikabidhi kambi ya Kunduz kwa vikosi vya Afghanistan, ambapo wanajeshi wa mwisho wa Ujerumani waliondoka tarehe 19 Oktoba.

Baadhi ya wakaazi wa eneo hilo walithibitisha kuwa hali ya usalama bado ni mbaya,lakini msemaji wa polisi mjini Kunduz, Sayed Sarwar Hussaini, aliiambia DW katika mahojiano kuwa hali ni tofauti. "Hali ya usalama katika mkoa wetu imeboreka tangu kuondoka kwa wanajeshi wa Ujerumani. Tunashuruku kwamba waliwapatia maafisa wetu mafunzo na wameweza kuisaidia serikali ya mkoa kuhalilisha usalama," alisema Hussain.

Jeshi la Ujerumani limeacha kutoa takwimu za matukio yanayohatarisha usalama kaskazini mwa Afghanistan kwa sababu vyombo vinavyohusika na ukusanyaji wa taarifa hizo nchini Afghanistan haviaminiki tena. Lakini chanzo kutoka wizara ya Ulinzi kilisema kuwa kwa ujumla hali ya usalama kaskazini mwa Afghanistan imeboreka kwa kiasi fulani.

Serikali yataka vikosi viendelee kuwepo
Muda wa mwisho wa kuwepo kwa vikosi vya Ujerumani nchini Afghanistani ni mwezi ujao wa Februari, na ikiwa serikali itataka kuurefusha muda huo, badi bunge linapaswa kuidhinisha mpango huo kabla ya kumalizika kwa muda wa mwisho.

Karzai na Merkel wakibadilishana nakala za mkataba wa ushirikiano baina ya mataifa yao.

Karzai na Merkel wakibadilishana nakala za mkataba wa ushirikiano baina ya mataifa yao.

Ujerumani pia inataka wanajeshi wake waendelee kuwepo nchini Afghanistan baada ya kuondoka kwa vikosi vya kimataifa vya ISAF. Kupitia mpango uliyopewa jina la "Resolute Support", Ujerumani itabakiza wanajeshi kati ya 600 na 800 mkoani Hindu Kush, ambao watasaidia kutoa mafunzo kwa vikosi vya usalama vya Afghanistan.

Hata hivyo, rais Karzai amegoma kutia saini makubaliano kati ya nchi yake na Marekani, ambayo ndiyo yangekuwa msingi wa mipango rasmi kati ya mataifa yanayochangia wanajeshi kupitia jumuiya ya NATO.

Iwapo mazungumzo kati ya Merkel na Karzai yalipiga hatua katika kutatua mgogoro juu ya makubaliano kuhusu hatma ya vikosi vya kimataifa, ni jambo ambalo serikali ya shirikisho haikuwa tayari kulizungumzia.

Mwandishi: Felden, Esther/Pöhle, Sven
Tafsiri: Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Daniel Gakuba


Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com