Mbuga ya wanyama ya Selous, Tanzania: Paradiso iliyo hatarini
Mbuga ya wanyama ya Selous ndiyo mbuga kubwa zaidi Afrika na ni kumbukumbu ya dunia ya turathi. Lakini itasalia kuwa hivyo? Serikali inataka kujengwa bwawa katika mbuga hiyo ila wanamazingira wanapinga.
Mazingira yanayopendeza
Hifadhi ya wanyama ya Selous ni mojawapo ya hifadhi kubwa zaidi duniani na ndiyo kubwa zaidi Afrika. Ina ukubwa wa kilomita za mraba 50,000 ya ardhi yenye miteremko na savana, kusini mashariki mwa Tanzania. Ni nyumbani kwa wanyama kama viboko, ndovu, nyati, yimba, mamba, duma, paa na zaidi ya aina 400 za ndege.
Historia ya kikoloni
Mbuga hiyo ya wanyama ilianzishwa na Wajerumani wakati wa ukoloni 1896. Baada ya kuichukua Tanzania kama koloni lake, Uingereza iliipa jina Frederick Selous, ambaye alikuwa afisa wa uingereza na mwindaji wa wanyama wa porini. Aliuwawa katika vita vya Kwanza vya dunia na kuzikwa katika mbuga hiyo. Mwaka 1982, UNESCO iliifanya kumbukumbu ya turathi kutokana na wanyama na mimea yake ya kipekee.
Turathi ya dunia ihatarini
UNESCO na mashirika mengine ya uhifadhi ya mazingira yanayachukulia mazingira ya Selous kuwa katika hatari kubwa. Miaka mitatu iliyopita, mbuga hiyo iliwekwa katika orodha ya kumbukumbu za turathi zilizo kwenye hatari. Licha ya serikali ya Tanzania kupinga hilo, UNESCO hivi majuzi iliamua kuiweka kwenye orodha hiyo.
Bwawa katika mbuga?
Mto Rufiji ni mwokozi wa mbuga hiyo. Ni mto wenye urefu wa kilomita 600 na unaishia katika Bahari ya Hindi kusini mwa Dar es Salaam. Hivi majuzi Rais John Magufuli alitangaza atajenga bwawa ambalo limepangwa kujengwa kwa miongo kadhaa. Umeme hautoshi Tanzania na rais huyo anataka mto Rufiji uwe chanzo cha nguvu za umeme.
Ukuta katika asili
"Hilo litakuwa pigo kwa asili," lilisema shirika la uhifadhi wa asili la World Wildlife Fund (WWF). Bwawa hilo litakuwa na urefu wa mita 130 na upana wa mita 700. Litatengeneza ziwa kubwa la zaidi ya kilomita 1000 mraba, na maji yatasambaa katika eneo ambalo ni kubwa hata kushinda Berlin.
"Kupeleka viwanda porini"
Kujenga bwawa hilo kunaamisha barabara, viwanda na makaazi ya wafanyakazi yatajengwa katika mbuga hiyo. WWF inahofia "kuharibiwa kwa mazingira safi na mojawapo ya makaazi ya wanyama walio katika hatari ya kupotea." Mipango ya kujenga bwawa hilo huenda likageuka na kuiumisha kichwa serikali ya Ujerumani pia.
Hatua ya Ujerumani kuilinda Selous
Siku moja kabla ya tangazo la Magufuli kwamba bwawa litajengwa karibuni, serikali yake na balozi wa Ujerumani nchini Tanzania walitia saini "mpango wa kuiendeleza na kuihifadhi mbuga ya Selous." Mpango huo unalenga kulinda na kuhifadhi mbuga hiyo kama kumbukumbu ya turathi ya dunia. Ujerumani ililipa Yuro milioni 18 kwa mradi huo.
Uchimbaji wa madini ya Urani eneo la kusini
Serikali ya Tanzania pia inalaumiwa kwa kuruhusu uchimbaji wa gesi na mafuta, na mgodi mmoja wa urani katika eneo la kusini la Selous. Katika maji ya mto Rufiji, kunatarajiwa kupatikana nururishi au Radioactive. Mashimo ya kwanza tayari yamechimbwa. WWF imeonya huenda hatua hii ikauchafua mto huo na kufika maji yaliyoko chini kabisa ardhini.
Uwindaji haramu umedhibitiwa
Serikali ya Tanzania inakataa kukosolewa na inaangazia ufanisi wake kuukabili uwindaji haramu pekee. Ni kweli kwamba idadi ya tembo katika mbuga ya Selous wameongezeka kwa kiasi fulani. Awali kulikuwa na zaidi ya tembo 100,000. Lakini uwindaji haramu na uuzaji wa magendo wa pembe ulifikia kiwango cha kwamba kati ya mwaka 1982 na 2014, karibu asilimia 90 ya tembo wote walikuwa wameuliwa.
Kupendeza kusikojulikana
Uwindaji kwa ajili ya biashara unaruhusiwa katika mbuga ya Selous. Ni chanzo cha pato kwa mbuga hiyo na zaidi ya watu milioni 1.2 ambao wanaishi viungani mwa mbuga hiyo. Katika baadhi ya maeneo, uwindaji haukubaliwi kabisa. Watalii lakini wanaweza kuzuru. Lakini kuna watalii wachache ikilinganishwa na mbuga ya kitaifa ya Serengeti, ingawa mbuga ya Selous imeizidi Serengeti mara tatu kwa ukubwa.