Mazungumzo ya Syria mashakani | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.01.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mazungumzo ya Syria mashakani

Mazungumzo ya amani ya Syria, yaliyosubiriwa kwa muda mrefu na yaliyopangwa kuanza Ijumaa yako mashakani baada ya kundi kuu la upinzani linalougwa mkono na Saudi Arabia kuonekana kusita kushiriki.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Syria Steffan de Mistura.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Syria Steffan de Mistura.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Syria Steffan de Mistura, Alhamisi alitoa ujumbe wa video kwa Waysria, ambamo alisisitiza kuwa miaka mitano ya mgogoro unaoendelea nchini mwao ni mingi sana, na kusema Wasyria wemeteseka vya kutosha, hivyo mkutano huu ambao ni wa tatu hauwezi kushindwa kufikia lengo.

Ujumbe wake ulikuwa mwepesi mno: Khalas, inatosha. Inatosha kwa majengo kuendelea kulipuliwa, inatosha kwa miji kushambuliwa kwa mabomu, inatosha kwa watu kuhatarisha maisha yao na kukabiliana na fedheha za kuishi kama wakimbizi, ni hatari tosha.

"Kitisho kiko machoni mwa kila mmoja. Laazima mfahamu pia kwamba tunawategemea nyinyi kupandisha sauti, na kusema inatosha, kumuambia kila mmoja anaetokea nchini Syria na ng'ambo kuhudhuria mkutano huu," alisema de Mistura.

Maeneo mengi nchini Syria yameharibiwa vibaya.

Maeneo mengi nchini Syria yameharibiwa vibaya.

Aliongeza kuwa kuna matarajio kwa wajumbe wa mazungumzo hayo kuhakikisha kuwa maono yao, uwezo wao wa kutoa tahfifu katika majadiliano ya kufikia suluhu ya mani nchini Syria ni sasa na wanahitaji kutoa hilo, na kusisitiza kuwa mkutano huu hauwezi kushindwa," alisema de Mistura katika ujumbe huo.

Upinzani wakaza msimamo

Lakini kundi kuu la upinzani la kamati ya juu ya majadiliano lilisema halitakwenda mjini Geneva, na kwamba lingefanya mazungumzo zaidi ya ndani siku ya Ijumaa katika mji mkuu wa Saudi Arabia Riyadh ili kutoa uamuzi wa mwisho juu ya ushiriki wao katika mazungumzo hayo.

Wajumbe muhimu wa upinzani wamekuwa wakionyesha kuwa ushiriki wao utategemea usitishwaji wa mashambulizi ya ndege za serikali ya Syria, na kuacha kuizingira miji iliyoko ndani ya nchi hiyo iliyoharibiwa kabisaa na vita. Kiongozi wa kamati hiyo Riyad Hijab, alisema wajumbe wa kamati hawaoni uwezekano wa kufanikiwa kwa mazungumzo hayo.

Hijab aliiambia televisheni ya Al Arabiya yenye makao yake Dubai, kuwa hawaendi kwenye mazungumzo hayo kwa sababu ajenda inayojadiliwa haikubaliki kwao. Wanadiplomasia wa magharibi wameongeza shinikizo kwa upinzani kushiriki mazungumzo hayo, ambayo ndiyo yatakuwa mjadala wa pili kati ya Wasyria wenyewe tangu kuanza kwa mgogoro huo.

Kiongozi mkuu wa muungano wa upinzani wa Syria Riyad Hijab.

Kiongozi mkuu wa muungano wa upinzani wa Syria Riyad Hijab.

Watakiwa wafikirie upya msimamo wao

Kamati hiyo imeomba ufafanuzi baada ya Umoja wa Mataifa kutoa mialiko kwa makundi mengine ya upinzani, na inataka uhakikisho kutoka kwa jamii ya kimataifa kwamba itachukuwa hatua kukomesha mashambulizi ya utawala dhidi ya raia na kuruhusu kuingizwa kwa misaada ya kiutu.

Marekani ilisema jana kuwa madai hayo ya muungano wa upinzani ni halali lakini pamoja na hayo iliwasihi wahudhurie mazungumzo hayo. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Mark Toner, alisema mazungumzo haya ni fursa ya kihistoria kwa pande zote kwenda Geneva na kupendekeza njia halisi za kuondokana na mkwamo nchini Syria.

Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya Wasyria robo milioni wameuawa katika vita hivyo, ambavyo vinakaribia kuingia katika mwaka wake wa tano, na mamilioni wameitoroka nchi hiyo.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,dape.

Mhariri: Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com