Mazungumzo ya amani ya Yemen kufanyika mwezi ujao | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.10.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mazungumzo ya amani ya Yemen kufanyika mwezi ujao

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, Ismail Ould Cheikh Ahmed, amesema ana uhakika mazungumzo ya amani kati ya serikali na waasi wa Kishia, huenda yakafanyika katikati ya mwezi Novemba mjini Geneva, Uswisi.

Ismail Ould Cheikh Ahmed

Ismail Ould Cheikh Ahmed

Akizungumza kwa njia ya simu na shirika la habari la Ufaransa-AFP, Ahmed amesema timu yake inawasiliana na pande hizo zinazohasimiana nchini Yemen, kujadiliana kuhusu mazungumzo ya amani yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa.

Amesema ana matumaini kwamba mazungumzo hayo yatafanyika kati ya Novemba 10 na 15. Mwanadiplomasia huyo amefafanua kuwa wamekubaliana kwa asilimia 90 kwamba mkutano utafanyika Geneva, lakini pia kuna uwezekano mkutano huo ukafanyika Muscat.

Jaribio la kwanza la kufanyika kwa mazungumzo ya amani mjini Geneva lilishindikana mwezi Juni, bila ya pande zinazohasimiana kukaa pamoja kwenye chumba kimoja. Mwezi uliopita, serikali ya Rais wa Yemen, Abed-Rabbo Mansour Hadi ilijiondoa kwenye mazungumzo ambayo yalikuwa yafanyike Oman, ikisisitiza kwanza waasi waondoke kwenye maeneo inayoyadhibiti.

Rais Abd-Rabbu Mansur Hadi

Rais Abed-Rabbo Mansur Hadi

Wakati hayo yakijiri shirika la madaktari wasio na mipaka-MSF, wanataka majibu kutoka jeshi la muungano linaloongozwa na Saudi Arabia kutokana na kushambuliwa kwa hospitali za shirika hilo kaskazini mwa Yemen. Shirika hilo limekataa hatua ya Saudia Arabia kukanusha kuhusika na shambulizi hilo.

Hospitali hiyo iliyoko kwenye mji wa kaskazini mwa Saada, ilishambuliwa jioni ya Jumatatu, hatua iliyolaaniwa vikali na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, ambaye pia alisema anahisi vikosi vya muungano vinahusika.

Vikosi vya muungano wa kijeshi vinahusika

Mkuu wa shughuli za oparesheni za shirika la MSF, Isabelle Defourny, amesema bila shaka yoyote ile, hospitali hiyo ilishambuliwa kwa ndege za kivita za muungano unaoongozwa na Saudia Arabia.

Aidha, mkuu wa idara ya dharura ya shirika hilo, Laurent Sury, amesema wanachotaka kwa sasa ni vikosi vya muungano kutambua kuwa mashambulizi hayo yamefanyika, waelezee kile kilichotokea na wahakikishe kuwa watasaidia kupeleka misaada ya kibinaadamu.

Wakati huo huo, Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa, WFP limetoa wito wa kuwepo kwa njia salama zitakazowawezesha kufika kwenye mji wa Taiz, likisema kwamba mapigano kati ya makundi yanayohasimiana, yamezuia chakula kupelekwa kwenye eneo hilo, huku maelfu ya watu wakiwa katika njaa kali.

Wapiganaji wa Houthi

Wapiganaji wa Houthi

Mkurugenzi mkaazi wa WFP, Muhannad Hadi, amesema wanawake, watoto na wazee wako katika hali mbaya na iwapo hali itaendelea kuwa hivyo, basi kutakuwa na janga la kibinaadamu.

Siku ya Jumatano, ndege za kivita za vikosi vya muungano ambavyo vinaiunga mkono serikali ya Yemen, viliwashambulia wapiganaji wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran, kuzunguka nchi nzima ya Yemen pamoa na kuwashambulia wapiganaji wenye itikadi kali za Kiislamu kwenye mji wa Taiz, ulioko kusini-magharibi.

Majimbo 10 kati ya majimbo 22 ya Yemen, yameelezwa kuwa katika hali mbaya tangu mwezi Juni na yanahitaji msaada wa dharura wa chakula. Kwa mujibu wa WFP, robo ya idadi ya watu wa Yemen ambayo ni sawa na watu milioni 7.6 wanahitaji msaada wa haraka wa chakula.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE
Mhariri: Yusuf Saumu

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com