Mauaji mapya yazusha wasiwasi nchini Kenya
27 Januari 2008Ripoti kutoka Naivasha zinasema watu 6 wamechomwa moto na 4 wengine wameuawa kwa kupigwa mapanga.Sasa si chini ya watu 60 wameuawa katika machafuko ya siku mbili zilizopita magharibi mwa Kenya.
Siku ya Jumamosi,baada ya kutembelea maeneo yaliyokumbwa na machafuko katika Bonde la Ufa,Annan alionya kuwa ghasia zilizozuka kufuatia kuchaguliwa tena kwa Rais Mwai Kibaki Desemba mwaka jana,sasa si mgogoro unaohusika na uchaguzi bali ni tatizo kubwa la ukiukaji wa haki za binadamu.Kiongozi wa upinzani Raila Odinga anamtuhumu Kibaki kuwa uchaguzi wa Desemba ulifanyiwa udanganyifu.
Hii leo,Kofi Annan baada ya kukutana na Odinga alitoa mwito kwa pande mbili zinazohasimiana kuwateua maafisa wanne kufanya majadiliano zaidi.Hali ya wasiwasi imezuka,kwa sababu ya mapambano yaliyotokea katika miji ya Naivasha na Nakuru.Takriban watu 800 wameuawa na kama watu laki mbili na nusu wamekimbia makaazi yao tangu kuzuka kwa machafuko yanayohusika na matokeo ya uchaguzi wa rais.