1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya wanafunzi 280 watekwa nyara Nigeria

8 Machi 2024

Watu wenye silaha wameishambulia shule moja katika eneo la Kaskazini-Magharibi mwa nchi hiyo na kuwateka nyara wanafunzi wasiopungua 287, tukio la pili kwa ukubwa nchini humo chini ya wiki moja.

https://p.dw.com/p/4dIgB
Nigeria | Schule Kidnapping 300 Kinder in Gefahr
Wananchi na wazazi wa watoto waliotekwa wakiwa wamekusanyika nje ya shule huko kaskazini magaharibi mwa Nigeria ambapo wanafunzi zaidi ya 280 wametekwaPicha: AP/dpa/picture alliance

Huko nchini Nigeria, Watu wenye silaha wameishambulia shule moja katika eneo la Kaskazini-Magharibi mwa nchi hiyo na kuwateka nyara wanafunzi wasiopungua 287, Utekaji huo ni wa pili kwa ukubwa katika taifa hilo la Afrika Magharibi katika muda wa chini ya wiki moja.

Vyanzo vya habari katika eneo hilo vinaeleza kwamba washambuliaji waliizingira shule inayomilikiwa na serikali katika mji wa Kuriga ulioko jimbo la Kaduna wakati wanafunzi walipokuwa wanajitayarisha kuanza masomo.

Soma zaidi: Nigeria yathibitisha watoto 136 kutekwa nyara

Awali, Mamlaka katika eneo hilo zilitaja kuwa idadi ya wanafunzi waliotekwa kuwa ni zaidi ya 100. Lakini mwalimu mkuu wa shule hiyo Sani Abdullahi alieleza kwamba waliotekwa ni wanafunzi 287.

Akielezea tukio hilo gavana wa jimbo la Kaduna  Uba Sani alisema "Katika uongozi wangu, hakuna mtoto atakayeachwa bila kuokolewa, wote watarudi nyumbani, kwa neema ya Mungu. Inshallah."

Nigeria | Shule
Watu wakiwa wamebeba mabango yanayotoa ujumbe kwa Gavana wa jimbo la Kaduna nchini Nigeria Uba Sani kumhimiza kuchukua hatua zaidi baada ya watoto zaidi ya 280 kutekwa nyaraPicha: AP/dpa/picture alliance

Bado haijulikani anayehusika na utekaji

Mpaka sasa, Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo ingawa lawama zinaangukia kwa makundi yenye silaha ambayo yanajumuisha wafugaji ambao wamekuwa watuhumiwa wakubwa wa kufanya mashambulizi ya kikatili na utekaji nyara ili kujipatia fedha.

Shambulio hilo limetokea siku chache baada ya zaidi ya watu 200, wengi wao wakiwa wanawake na watoto kutekwa nyara na watu wenye itikadi kali kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Soma zaidi: Wanafunzi 35 wa Chuo Kikuu watekwa nyara Nigeria 

Wanawake, watoto na wanafunzi mara nyingi hulengwa katika matukio hayo ya utekaji nyara katika eneo la kaskazini mwa Nigeria na ili waweze kuachiliwa huru makundi hayo yamekuwa yakidai kulipwa fedha nyingi kutoka kwa serikali.

Nigeria | Jeshi
Magari ya jeshi la Nigeria yakiwa katika eneo la shule waliyotekwa wanafunzi huko kaskazini magharibi mwa NigeriaPicha: AP Photo/picture alliance

Wachambuzi: Hakuna dalili za kuimarika kwa usalama

Kwa mujibu wa ripoti ya uchambuzi ya Shirika la habari ya AP inasema waangalizi wa mambo wanasema mashambulizi yote mawili ni matokeo ya hali mbaya ya Nigeria ya mzozo wa usalama ambao ulisababisha vifo vya mamia kadhaa
watu mnamo 2023.

Matukio ya utekwaji nyara kwa wanafunzi kutoka shule za kaskazini mwaNigerialimekuwa jambo la kawaida na linalozua hofu miongioni mwa watu katika eneo hilo,Itakumbukwa mwaka 2014 wanafunzi zaidi ya 200 wa Chiobok walitekwa katika jimbo la Borno.

Hata hivyo,  mwaka uliopita raisi wa Nigeria Bola Tinubu mara tu baada ya kuchaguliwa kuwa kiongozi wa taifa hilo aliahidi kukomesha matukio hayo,lakini wachambuzi wanasema kuwa bado hakuna dalili za kuimarika usalamakufuatia mfululizo wa matukio ya utekaji nyara yanayoendelea kuripotiwa.