1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mateka wa Israel na Daktari wa Kipalestina wafariki

3 Mei 2024

Mateka mmoja wa Israel amefariki mikononi mwa kundi la Hamas, huku daktari bingwa wa Kipalestina akiripotiwa pia kufariki akiwa kizuizini katika gereza la Israel.

https://p.dw.com/p/4fTL0
Mzozo katika Ukanda wa Gaza- Hospitali ya al Shifa
Mzozo katika Ukanda wa Gaza - Wapalestina wakisubiri kupatiwa matibabu katika Hospitali ya al ShifaPicha: picture alliance/dpa/XinHua

Serikali ya Israel imefahamisha hivi leo kuwa mateka huyo ambaye ni sehemu ya wengine zaidi ya 130 wanaoshikiliwa na kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza amekufa kama makumi ya wengine waliotekwa nyara wakati wa shambulio la Oktoba 7.

Serikali mjini Tel-Aviv imetoa taarifa hiyo jana jioni kwenye mtandao wao wa kijamii wa X (zamani Twitter), na kusema kuwa mwili wa mwanaume huyo bado upo katika  Ukanda wa Gaza . Hata hivyo, sababu za kifo chake hazikubainishwa na haikuwa wazi ni lini aliuawa au ni kwa njia gani Israel ilipata taarifa ya kifo cha mateka huyo.

Mke wa mateka huyo aliripotiwa pia kuuawa wakati wa shambulio la Oktoba 7 huku watoto wake wawili kati ya watatu wakitekwa nyara hadi katika Ukanda wa Gaza. Binti yake mwenye umri wa miaka 13 na mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 17 waliachiliwa mwezi Novemba mwaka jana, kama sehemu ya makubaliano kati ya serikali ya Israel na kundi la Hamas.

Kifo cha Daktari bingwa wa Kipalestina katika jela za Israel

Polisi wa Israel wakiizingira Hospitali ya al Shifa huko Gaza
Polisi wa Israel wakiizingira Hospitali ya al Shifa huko Gaza wakiwasaka wapiganaji wa kundi la Hamas: 22.11.2023Picha: Ronen Zvulun/Reuters

Mashirika mawili ya kutetea haki za wafungwa wa Kipalestina yamesema katika taarifa yao ya pamoja kwamba Daktari Adnan Al-Bursh, alikuwa mkuu wa madaktari wa mifupa katika Hospitali ya Al Shifa na alikamatwa na kuzuiliwa na vikosi vya Israel alipokuwa akifanya kazi kwa muda katika Hospitali ya Al-Awada kaskazini mwa Gaza. Dokta huyo amekuwa akizuiliwa kwa zaidi ya miezi minne.

Mashirika hayo yamesema kuwa hayo ni "mauaji ya wazi" na kusisitiza kuwa mwili wa Daktari huyo bado umezuiliwa na vikosi vya Israel. Mamlaka ya magereza ya Israel ilitoa taarifa mnamo Aprili 19, ikisema kuwa mfungwa mmoja aliyekuwa anazuiliwa kwa sababu za usalama wa taifa alikufa katika gereza la Ofer lakini hawakutoa maelezo zaidi juu ya sababu za kifo chake. Baadaye walithibitisha kuwa taarifa hiyo ilimhusu Dokta Burshi, na kusema kuwa uchunguzi umeanzishwa kuhusu tukio hilo.

Soma pia: Misri ina matumaini kuwa Israel, Hamas watafikia makubaliano

Mashirika ya afya ikiwa ni pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO) waliionya Israel mara kadhaa kusitisha mashambulizi dhidi ya wahudumu wa afya ambao hadi sasa karibu 200 tayari wameuawa kulingana na makadirio ya kundi la watafiti la Insecurity Insight. Lakini wizara ya afya ya Palestina imesema kifo cha Dokta Burshi kimepelekea idadi ya wahudumu wa afya waliouawa na Israel huko Gaza kufikia 496.

Watu 7 wauawa Rafah huku Uturuki ikisitisha biashara na Israel

Gaza | Uharibifu huko Rafah kufuatia mashambulizi ya Israel
Uharibifu mkubwa unaoshuhudiwa huko Rafah kufuatia mashambulizi ya Israel:08.04.2024Picha: Bassam Masoud/REUTERS

Israel imeendeleza mashambulizi huko Rafah na kusababisha vifo vya watu 7 wakiwemo wanawake na watoto kama anavyoelezea Sana Z´oroub shangazi wa watoto waliouawa:

"Makombora matatu yamewaripua watoto wasio na hatia. Mama na mabinti zake wawili waliokuwa wamelala mapajani mwake wamekutwa vipande vipande. Walikuwa darasa la kwanza na la sita. Bisan na Basmala walilala kwenye mapaja ya mama yao na sasa wako vipande vipande. Je, Waisraeli wananufaika vipi na jambo hili? Wanafaidika nini kwa kuwaua watoto wasio na hatia?”

Soma pia: Netanyahu aapa kuushambulia mji wa Rafah

Hayo yakiarifiwa, Uturuki imethibitisha msimamo wake wa kutofanya biashara na Israel hadi pale kutakapopatikana makubaliano ya usitishwaji mapigano huko Gaza na kuhakikisha misaada ya kibinaadamu inawasilishwa kikamilifu katika eneo hilo. Mwaka jana, thamani ya biashara kati ya nchi hizo mbili ilifikia kiasi cha cha dola bilioni 6.8.

(Vyanzo: Mashirika)