Marekani yataka uchaguzi ufanyike kama ulivyopangwa Senegal
14 Februari 2024Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken ahimiza uchaguzi nchini Senegal ufanyike haraka iwezekanavyo huku akitoa tahadhari yake kuhusu kucheleweshwa kwa uchaguzi baada ya kuwasiliana kwa njia ya simu na Rais Macky Sall. Kwa mujibu wa Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Matthew Miller, ameweka wazi kuwa wangependa kuona uchaguzi unafanyika kama ulivyopangwa.Miller pia alisema kuwa Marekani inawasiwasi mkubwa kuhusu hali katika taifa hilo la Afrika Magharibi, ambapo mamlaka jana Jumanne ilizuia mtandao wa simu na kupiga marufuku maandamano. Rais Sall amesogeza mbele uchaguzi wa Februari 25, na kusababisha mzozo wa kisiasa nchini Senegal, ambao kijadi ni thabiti na kutolewa mfano na Blinken kama demokrasia bora kwa Afrika katika ziara yake ya 2021.Miller ameongeza kwa kusema Blinken anahimiza uchaguzi ufanyike kwa wakati na ikiwa hautafanyika mnamo Februari 25, ungepaswa kufanyika haraka iwezekanavyo baada ya hapo.