Marekani yatafuta washirika dhidi ya ISIS | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.08.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Marekani yatafuta washirika dhidi ya ISIS

Marekani imeongeza kasi yake ya kujenga kampeni ya kimataifa dhidi ya wapiganaji wa kundi la Dola ya Kiislamu nchini Syria na Iraq, ikiwemo kupata washirika wa uwezekano wa operesheni ya pamoja ya kijeshi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Washington, msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani Jen Psaki alisema hivi sasa wanawasiliana na washirika wao na kuwauliza ni namna gani wataweza kuchangia kibinaadamu, kijeshi, kijasusi na hata kidiplomasia.

Uingereza na Australia ndiyo zina uwezekano mkubwa wa kujiunga na kampeni hiyo, Ujerumani ilisema siku ya Jumatano kuwa ilikuwa katika mazungumzo na Marekani juu ya uwezekano wa hatua za kijeshi, lakini ikabainisha wazi kutokuwa tayari kushiriki operesheni yoyote ya aina hiyo.

Ndege ya kivita ya Marekani ikiruka kwenda kushambulia ngome ya IS.

Ndege ya kivita ya Marekani ikiruka kwenda kushambulia ngome ya IS.

Marekani kwenda kivyake ikibidi

Maafisa wa Marekani walisema nchi hiyo inaweza kuchukuwa hatua kivyake ikibidi, dhidi ya wapiganaji hao walioteka theluthi moja ya kila mmoja ya mataifa ya Iraq na Syria, na kutangaza vita dhidi ya mataifa ya magharibi.

Wasaidizi wandamizi wa ikulu ya White House walikutana wiki hii kujadili mkakati wa kutanua mashambulizi dhidi ya Dola ya Kiislamu, ikiwa ni pamoja wa uwezekano wa mashambulizi ya angani dhidi ya ngome za wapiganaji hao mashariki mwa Syria -- ongezeko ambalo bila shaka litakuwa la hatari zaidi kuliko operesheni ya sasa ya Marekani nchini Iraq.

Wakati serikali ya Iraq iliyakaribisha mashambulizi ya ndege za Marekani dhidi ya wapiganaji wa Dola ya Kiislamu, rais wa Syria Bashar al-Assad ameonya kuwa mashambulizi yoyote yatakayofanywa bila idhini ya nchi yake yatachukuliwa kama kitendo cha uvamizi, na yumkini yakautumbukiza muungano utakaoogozwa na Marekani katika mgogoro mpana zaidi na Syria.

Assad siyo mshirika wa mapambano dhidi ya ugaidi

Rais wa Ufaransa Francois Hollande, alionya siku ya Alhamisi kuwa rais wa Sayria Bashar Assad hawezi kuwa mshirika wa mataifa ya magharibi katika mapambano dhidi ya ugaidi, bali ni mshirika wa Waislamu wenye itikadi kali wanaofanya vurugu nchini Syria na Iraq.

RAis wa Syria Bashar al-Assad.

RAis wa Syria Bashar al-Assad.

"Assad hawezi kuwa mshirika katika mapambano dhidi ya ugaidi, ni mshirika asiye rasmi wa majihadi," aliuambia mkutano wa mabalozi kutoka duniani kote uliyofanyika mjini Paris.

Matamshi yake yalikuja kufuatia kauli ya utawala wa Assad siku ya Jumatatu, kwamba uko tayari kushirkiana na jamii ya kimataifa, ikiwemo Washington, kukabiliana na wapiganaji wenye misimamo mikali katika taifa hilo lililoharibiwa na vita.

Uingereza, Australia bado kuthibitisha

Ubalozi wa Uingereza mjini Washington ulisema haujapokea maombi kutoka kwa Marekani kwa ajili ya mashambulizi ya angani. Msemaji wa waziri mkuu wa Australia Tony Abbott, alisema msaada wa kibinaadamu nchini Iraq utaendelea, lakini alikataa kusema iwapo Australia itajiunga na operesheni ya pamoja inayoongozwa na Marekani.

Seriakali ya Ujerumani imesema itatoa silaha kwa vikosi vya Wakurdi vinavyopambana dhidi ya Dola ya Kiislamu katika eneo hilo, lakini Kansela Angela Merkel amekuwa akirudia mara kwa mara kwamba Ujerumani haitatuma wanajeshi wa mapambano nchini Iraq.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier alisema serikali ya Ujerumani inataka kuwasaidia Wairaq lakini haijafikia uamuzi wa hasa msaada gani utatolewa, ingawa jeshi la Ujerumani tayari limetuma waratibu wa msaada huo kaskazini mwa Iraq.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Samantha Power.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Samantha Power.

"Nadhani tunapaswa kuwasaidia wale wanaopambana kuwadhibiti magaidi kwa kuwapa msaada wowote ulioko ndani ya uwezo wetu ili waweze kuizuwia Dola ya Kiislamu kulichukuwa eneo lote na kuunda khilafa itakayokuwa kubwa sana. Nadhani kufikia Jumapili, serikali itafikia uamuzi juu ya nini hasa tutawapatia, alisema waziri Steinmeier.

Msemaji wa ikulu ya White House Josh Earnest alisema rais Obama ataitisha mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba kujadili kitisho kinachotolewa na wakaazi wa mataifa ya magharibi walioingiwa na misimamo mikali wanaorejea kutoka katika mapigano nchini Syria.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre,dpa, afpe.
Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com