1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Kenya kujenga barabara ya Nairobi hadi Mombasa

Sylvia Mwehozi
28 Agosti 2018

Marekani na Kenya zimekubaliana ujenzi wa barabara kubwa ya kutoka Nairobi hadi Mombasa. Makubaliano hayo yalikuja katika mazungumzo kati ya rais Donald Trump na Uhuru Kenyatta ambaye yuko ziarani mjini Washington. 

https://p.dw.com/p/33u8x
USA Uhuru Kenyatta und Donald Trump in Washington
Picha: Imago/O. Douliery

Baada ya rais Trump kumkaribisha Kenyatta katika ofisi ya Oval kwenye Ikulu ya  White house , viongozi hao walielezea ushirikiano wa karibu wa kiuchumi, unaolenga kuyafanya mataifa hayo kuwa imara na ustawi wa wananchi wake. Mradi unaojulikana kama barabara ya Nairobi hadi Mombasa utaunganisha mji mkuu wa Kenya na ule wa pili Mombasa, na utajengwa na kampuni ya kimarekani ya Bechtel Corporation.

"Tumekuwa na uhusiano mzuri kabisa na Kenya, unakuwa mkubwa kila wakati . Tumo katika mpango mkubwa wa mradi wa miundombinu, barabara kubwa itakayoweka rekodi kwa njia tofauti na tutakamilisha mambo mengi mazuri", alisema Trump.

Mkurugenzi wa shirika la uwekezaji la Marekani alikutana mwezi uliopita na kampuni ya ujenzi ya Bechtel nchini Kenya kuhusu utayari wa shirika hilo juu ya mradi, unaochukuliwa na Marekani kama njia ya kushindana na uzinduzi wa mipango ya China ya ujenzi wa barabara na reli barani afrika na mahali pengine. Mwaka jana Kenya ilifungua njia ya reli iliyofadhiliwa na China kati ya Nairobi na Mombasa, ambayo inaelezwa na Kenya kuwa mradi mkubwa wa miundombinu tangu uhuru.

USA Uhuru Kenyatta und Donald Trump in Washington
Rais Trump na Kenyatta wakiteta jambo jijini WashingtonPicha: Imago/R. Sachs

Taarifa ya Ikulu ya White House imesema pande zote zimekubaliana kutafuta ushauri zaidi ili kukamilisha masharti ya makubaliano ya ufadhili. Viongozi hao wawili pia walitangaza kwamba serikali zao zimeanzisha safari za moja kwa moja za ndege kati ya Nairobi na New York.

"Tumekuwa na ushirikiano bora, hususan katika mapambano yetu dhidi ya ugaidi kwasababu ya ujirani tulioko, tuko katika mapambano na Al-shabaab, ambayo Marekani imekuwa mshirika muhimu na imara. Muhimu zaidi tuko hapa kwa ajili ya kutafuta na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji, ambao tayari uko imara", Kenyatta aliwaeleza waandishi wa habari. 

White House imeongeza kwamba "mikataba mingine ya kibiashara inayogharimu karibu dola milioni 900 iliyotangazwa wakati wa ziara hiyi itaweza kutengeneza ajira nyingi baina ya Wamarekani na Wakenya, na baadae kuwezesha ustawi na ushindani wa kiuchumi wa mataifa yote mawili". Trump amekuwa akikosolewa kwa kutozipa kipaumbele nchi za kiafrika na kutakiwa kuomba msamaha mapema mwaka huu, baada ya maoni yake binafsi aliyosema nchi za kiafrika na nyingine zina uozo, kuvuja kwa waandishi wa habari.

Kenia Treffen Uhuru Kenyatta mit Barack Obama
Rais Kenyatta akimkaribisha rais mstaafu wa Marekani Barack Obama aliyezuru Kenya Julai 2018Picha: Reuters/Presidential Press Service

Kenyatta amekuwa akijaribu kusafisha taswira yake kufuatia mgogoro, ambapo mahakama ya juu ya Kenya ilifuta matokeo ya urais mwezi Agosti ikisema kulikuwa na mapungufu na kuitishwa uchaguzi mpya uliosusiwa na upinzani. Kenya ni taifa la tatu linalopokea misaada ya kiusalama ya Marekani katika ukanda wa Kusini mwa jangwa la sahara, kwa mujibu wa shirika linalofuatilia misaada ya usalama.

Nchi zote Kenya na Marekani zina vikosi vyake nchini Somalia na kundi la Al-shabaab lenye mafungamano na al-Qaeda limevuka mpaka kufanya mashambulizi kadhaa nchini Kenya, likisema ni malipo ya kutuma askari Somalia. Karibu maafisa wa polisi 100 wameuawa tangu mwezi Mei 2017 katika milipuko ya mabomu na mashambulizi ya kushutukiza.

Rais huyo wa Kenya pia atakutana na wafanyabiashara wa Marekani akiwa Washington ili kukuza uwekezaji katika taifa hilo la Afrika Mashariki. Naye mke wa rais wa Marekani Melania Trump anatarajiwa kufanya ziara ya peke yake barani Afrika.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AP/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman