Maoni ya wahariri juu ya hukumu iliyotolewa kwa Mohammed Morsi | Magazetini | DW | 22.04.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Maoni ya wahariri juu ya hukumu iliyotolewa kwa Mohammed Morsi

Katika maoni yao leo wahariri wanazungumzia juu ya hukumu iliyotolewa kwa aliekuwa Rais wa Misri Mohammed Morsi na juu ya sera ya Umoja wa Ulaya kuhusu wakimbizi.

Aliekuwa Rais wa Misri Mohammed Morsi

Aliekuwa Rais wa Misri Mohammed Morsi

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linatilia maanani kwamba aliekuwa Rais wa Misri Mohammed Morsi amepewa kifungo cha miaka 20 jela badala ya adhabu ya kifo! Mahakama ya mjini Cairo ilimtia Morsi hatiani kwa kosa la mauaji ya waandamanaji.

Mhariri wa gazeti la "Frankfurter Allgemeine" anasema kwa kutoa adhabu hiyo ya kifungo jela, mahakama ya nchini Misri imelenga shabaha za ndani na nje ya nchi. Kuhusu ndani lengo ni kuwaandama wapinzani kwa kadri itakavyowezekena hadi hapo watakapovunjika nvugu kabisa. Na kuhusu nje, inapasa kutilia maanani kwamba Rais Abdel Fattah al-Sisi anataka kutambuliwa kimataifa na hivi karibuni atafanya ziara nchini Ujerumani. Kutokana na hali hiyo watawala wa Misri walihofia kumpa Morsi adhabu ya kifo.

Wengine bado wanaweza kunyongwa

Hata hivyo mhariri wa"Frankfurter Allgemeine" anasema bado pana uwezekano wa kutekelezwa adhabu ya kifo iliyotolewa kwa watu wengine zaidi ya mia moja ili kuonesha, ni nani mwenye usemi nchini Misri.

Katika maoni yake gazeti la "Münchner Merkur" pia linatilia maanani kwamba Morsi amepewa adhabu ya kifungo jela badala ya kitanzi! Mhariri wagazeti hilo anaeleza kwamba adhabu iliyotolewa kwa Morsi imeonyesha ishara ya kujihadhari yenye lengo la kuepusha vita baina ya wafuasi wa chama cha Udugu wa Kiislamu na watawala wa kijeshi nchini Misri. Watawala wa kijeshi nchini Misri pia wamehofia msimamo wa jumuiya ya kimataifa laiti Morsi angelipewa adhabu ya kifo.

Mkono mrefu wa sheria wamfikia fashisti

Baada ya miaka 70 aliekuwa afisa wa jeshi la mafashisti amefikishwa mahakamani nchini Ujerumani. Mtu huyo Oskar Gröning anakabiliwa na mashtaka ya kusaidia katika mauaji ya wafungwa zaidi 300,000 katika kambi ya Auschwitz.

Juu ya kesi hiyo gazeti la "Emder" linasema jambo muhimu kabisa ni kwamba mtu huyo amefikishwa mahakamani. Siyo muhimu sana iwapo ataenda jela au la. Jambo muhimu pia ni kuuchunguza uhalifu uliotendwa na mafashisti.

Sera ya kuwawinga wakimbizi siyo jawabu
Gazeti la "Braunschweiger" linaikosoa sera ya uhamiaji ya Umoja wa Ulaya inayoelekezwa katika kuwazuia wakimbizi kwa kuwatisha.

Mhariri wa gazeti hilo anafafanua kwa kusema ikiwa watu wawili wamesimama mkabala na kila mmoja ana bunduki, bila shaka wataogopana. Lakini mtu asiekuwa na matumaini yoyote juu ya maisha katika nchi yake hataogopa kujaribu kufanya kila kitu ili kuondoka na kutafuta maisha bora kwingineko.

Na kwa hivyo badala ya nchi za Umoja wa Ulaya kupandisha kuta mipakani kuwazuia wakimbizi ,litakuwa shauri bora kuyashughulikia maombi ya wakimbizi wangali wakiwamo katika nchi zao na pia litakuwa jambo la busara kuyaweka mazingira ya kisheria ili kuwaruhusu watu kuingia Umoja wa Ulaya wanaokimbia vita katika nchi zao.

Mwandishi:Mtullya Abdu

Mhariri: Yusuf Saumu