Maoni mseto kuhusu uamuzi wa uavyaji mimba Kenya
27 Aprili 2026
Kesi hiyo inatokana na tukio la mwaka 2022 lililomhusisha msichana wa umri mdogo aliyepata huduma ya dharura baada ya kuharibika kwa mimba. Ingawa Mahakama Kuu ilimuondolea hatia yeye pamoja na daktari aliyemtibu na kuthibitisha kuwa utoaji mimba ni haki ya msingi, Mahakama ya Rufaa imeamua vinginevyo.
Jopo la majaji watatu limesema kuwa, "Kwa ujumla, utoaji mimba si haki ya msingi inayolindwa na Katiba. Kinyume chake, Katiba inaikataza wazi, isipokuwa katika visa vichache ambavyo vinaweza kuruhusiwa.” Kwa mujibu wa Sheria ya Adhabu, utoaji mimba ni kosa la jinai linaloweza kuadhibiwa kwa kifungo cha hadi miaka 14.
Hata hivyo, Katiba inaruhusu utoaji mimba pale ambapo mhudumu wa afya aliyehitimu anaona ni lazima kama matibabu ya dharura ili kuokoa maisha au afya ya mama. Wataalam wa afya ya uzazi wameukosoa uamuzi wa mahakama ya Rufaa. Prudence Mutiso ni Wakili wa Shirika la haki ya Uzazi.
"Mahakama ya Rufaa imebuni kitu kinaitwa "athari ya kuhofisha”, sio tu kwa wanawake na wasichana lakini pia kwa watoaji huduma za afya, kimsingi inamaanisha wanawake na wasichana watachelewa kutafuta msaada.”
Aidha Shirika la kimataifa la haki za binadamu, Center for Reproductive Rights, limetaja uamuzi huo kuwa ni hatua ya kurudisha nyuma, hatua zilizopigwa kwenye Nyanja hiyo na kusema litaelekea Mahakama ya Juu ya Kenya kuupinga.
Maoni kinzani kuhusu uamuzi huo wajitokeza wazi Kenya
Aidha, shirika la kidini la Kenya Wataalamu wa Kikristo pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali walikuwa wamewasilisha rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu wa mwaka 2022. Wakili wao, ambaye pia ni mwenyekiti wa zamani wa jukwaa hilo, Charles Kanjama, alisema uamuzi wa Mahakama ya Rufaa "umerejesha mizani ya kikatiba iliyokuwa imevurugwa na uamuzi wa Mahakama Kuu.”
Kanjama aliongeza kuwa mtu yeyote anayeshtakiwa chini ya vifungu vya 158, 159 au 160 vya Sheria ya Adhabu atalazimika kutoa ushahidi kuthibitisha kuwa hakuhusika katika utoaji mimba usio halali. Lakini Wakenya wanasemaje kuhusu uamuzi huo?
Majaji walifafanua kuwa Kifungu cha 26(3) na (4) kinaweka masharti finyu yanayoruhusu utoaji mimba kutekelezwa kisheria. Masharti hayo ni pamoja na pale ambapo, kwa maoni ya mhudumu wa afya aliyehitimu, kuna haja ya matibabu ya dharura au ambapo maisha au afya ya mama yako hatarini.
Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2025 iliyochapishwa kwa pamoja na Wizara ya Afya, Kituo cha Idadi ya Watu, Utafiti na Afya Pamoja na Tasasisi ya Guttmacher, utoaji mimba ni miongoni mwa sababu kuu za vifo vya akina mama, huku takribani mimba 792,000 zikikadiriwa kutolewa nchini Kenya kati ya Aprili 2023 na Mei 2024.