1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamia ya waandamanaji wakamatwa Urusi

Daniel Gakuba
10 Septemba 2018

Mamia ya watu wamelala korokoroni nchini Urusi, baada ya kukamatwa katika maandamano ya nchi nzima, kupinga mageuzi katika mfumo wa pensheni. Maandamano hayo yalifanyika sambamba na uchaguzi wa serikali za mitaa.

https://p.dw.com/p/34bAg
Russland Proteste in Moskau
Picha: Reuters/S. Karpukhin

Kamata kamata iliyofanywa na polisi iliwatia mbaroni watu takriban 840, wengi wakitoka katika miji ya Saint Petersburg na Ekaterunburg, jiji lililo katika eneo la milima ya Ural. Waliokamatwa walikuwa wakishiriki katika maandamano yaliyoitishwa na kiongozi wa upinzani aliyeko kizuizini, Alexei Navalny, kupinga mabadiliko katika mfumo wa pension.

Katika mji mkuu, Moscow, watu wapatao 2000 waliingia mitaani, wakati uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa ukiendelea katika jiji hilo, ambapo mgombea anayeungwa mkono na Ikulu ya Kremlin ana uhakika wa kupata ushindi. Baadhi ya waandamanaji hao walitamka maneno ya kumkashifu Rais wa Urusi Vladimir Putin, wakimwita mwizi na kumtaka aondoke madarakani.

''Kwa nini Putin achukuwe fedha zetu ambazo tumezipata kihalali, ambazo tumejiwekea akiba maisha yetu yote, ambazo nimejiwekea, ambazo kila mtu amejiwekea'', alisema mmoja wa waandamanaji hao, Alexander Trubin.

Russland Präsident Putin Rentenreform
Mageuzi haya katika mfumo wa pensheni yamemshushia umaarufu Rais Vladimir PutinPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Druzhinin

Mwingine, Vera Kirchenko akaongeza, ''Tunayo faida nzuri tu kutokana na pensheni  yetu, lakini serikali inaichukua, na hakuna mtu anayewajibishwa. Kwa nini wasiweke sheria zinazowazuia watu kupora katika mifuko ya pensheni?

Putin asota na mashine

Rais Vladimir Putin anayenyoshewa kidole cha lawama, nusura ashindwe kupiga kura yake mjini Moscow, baada ya mashine ya kupiga kura kuikataa karatasi yake mara mbili. Hata hivyo, mara ya tatu, alifanikiwa.

Waandamanaji wanaishutumu serikali yake kujiingiza katika nmizozo ya kimataifa, huku ikikosa uwezo wa kuwahudumia wafanyakazi wake wa zamani. Mmoja wa waandamanaji hao, Tatyana Rechetskaya, alisema mageuzi katika mfumo wa pensheni nchini Urusi ni pigo la mwisho kwa wafanyakazi, ambalo hawawezi kulivumilia.

Kulingana na sheria ya mageuzi hayo kwenye mfumo wa pensheni, wanawake ambao awali walikuwa wakistaafu wakiwa na umri wa miaka 55 watakuwa sasa wakienda katika likizo ya uzeeni wakiwa na miaka 63, nao wanaume ambao hadi sasa walikuwa wakistaafu kwenye umri wa miaka 60, watasubiri miaka mingine mitano. Sheria hii imeshusha umaarufu wa Rais Vladimir Putin.

Umri mdogo wa kuishi kwa Warusi

Russland - Proteste gegen die Erhöhung des Rentenalters
Wengi wa waandamanaji wanasema mfumo mpya ni hujuma ya akiba waliyojiwekeaPicha: picture-alliance/dpa/TASS/V. Smirnov

Haya ni mabadiliko ya kwanza katika mfumo wa pensheni kwa muda wa miaka 90 nchini Urusi, na yanausogeza mfumo wa nchi hiyo na ule wa mataifa ya Magharibi. Hata hivyo wakosoaji wanasema kwa kuzingatia matarajio ya umri wa kuishi nchini Urusi, wengi hawatafikisha umri huo wa kustaafu kuweza kufaidi akiba ya uzeeni waliyojiwekea.

Mtandao wa internet wa Google ulilazimika kuliondoa tangazo la kiongozi wa upinzani Alexei Navalny, baada ya shinikizo kutoka serikali ya Urusi, haya yamethibishwa na afisa aliyeko karibu na kiongozi huyo wa upinzani.

Matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa yaliyofanyika Urusi jana, yanatarajiwa kutangazwa baadaye leo Jumatatu.

Mwanishi: Daniel Gakuba/afpe, rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga