1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mambo yanapamba moto Syria

16 Agosti 2011

Majeshi ya Syria leo yameushambulia mji wa Latakia kwa mabomu na kuendelea kuusakama mji huo wa bandari

https://p.dw.com/p/12HlK
Mji wa bandari wa Latakia, SyriaPicha: AP Photo / SHAMSNN

Majeshi ya Syria leo yameushambulia mji wa Latakia kwa mabomu na kuendelea kuusakama mji huo wa bandari ambapo tayari madarzeni ya watu wamekufa na kuwafanya wakimbizi wa Kipalastina kuukimbia. Jumuiya ya kuchunguza utekelezaji wa haki za binadamu katika Syria imesema mabomu mazito na risasi zilitumiwa katika maeneo ya Latakia. Tangu jumapili, raia 30 wameuliwa kwenye mji huo katika hujuma ambayo, kwa mujibu wa wanaharakati wa haki za binadamu, mashua za kivita zilitumiwa na majeshi ya usalama ya Syria, kwa mara ya kwanza tangu kuanza uasi wa kutaka demokrasia katika nchi hiyo.

Lakini shirika rasmi la habari la Syria limekanusha juu ya kufanyika operesheni zozote kutokea baharini. Shirika  la Umoja wa Mataifa la kuwasaidia wakimbizi wa kipalastina limeripoti kwamba zaidi ya nusu ya wakimbizi 10,000 wa kutoka kambi ya Ramel, kusini mwa Latakia, wamekimbia, huku wakiwa wanashambuliwa kwa risasi. Shahidi mmoja alisema vifaru 15 vimewekwa kuzunguka Ramel.

Tote bei den Protesten in Latakia Syrien NO FLASH
Jeneza la maiti wa mtu aliyeuliwa na majeshi ya Syria huko Latakia linaongozwa kwenda kuzikwaPicha: picture-alliance/dpa

Hujuma hizo zilizofanywa Latakia zimelaaniwa na nchi za Kiarabu. Katibu mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Palastina, PLO, Yasser Abed Rabbo, amesema hujuma hizo ni sehemu ya uhalifu dhidi ya ubinadamu, yakiwalenga Wasyria na Wapalastina kwa pamoja.

Gazeti la kila siku la Syria, al-Watan, limesema mji wa Latakia uko chini ya udhibiti wa jeshi, na kwamba mambo yamedhibitiwa katika mji huo, hasa baada ya jeshi kuwakamata madarzeni ya watu waliokuwa na silaha katika operesheni iliokuwa ngumu. Gazeti hilo lilisema watu waliokuwa na silaha waliweka vizuwizi na kutega mabomu kulizuwia jeshi lisisonge mbele, hivyo kusababisha wakaazi kuikimbia mitaa yao

Mkaazi wa Latakia aliliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP, kwamba milio ya bunduki ilikuwa ikisikika mfulullizo, na kwamba milio ya bunduki inatoka kwa wanajeshi walioko katika mapaa ya majumba yanayozunguka shule kadhaa. Mkaazi mwengine amesema wanajeshi wamefyetua risasi za kuonya kwa waumini waliokuwa wanatoka msikitini na kuwakamata watu. Pia alisema majeshi ya usalama yamekata usambazaji wa umeme, wanaingia kwa nguvu katika majumba, vizuwizi vimewekwa katika barabara za mji huo na maduka yote yamefungwa.

Wakimbizi wa kipalastina walikusanyika katika uwanja wa michezo. Pia wanaharakati katika mji wa Homs walisema majeshi ya usalama yalifyetua risasi  leo katika mitaa ilioko kwenye viunga vya mji huo. Walisema vifo katika operesheni za jeshi katika mji huo na katika mji wa karibu wa Hula vimefikia idadi ya watu 12 tangu jana, jumatatu.

Tangu kuanza mwezi huu mtukufu wa Ramadhan watu 260, wakiwemo wanawake 14 na watoto 13, wamehesabiwa kuwa wamekufa. Rais  Barack Obama wa Marekani amesema Rais Bashar al-Assad wa Syria amepoteza uhalali wake na kwamba wananchi wa Syria watakuwa katika hali ilio bora bila ya yeye. Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Jay Carney, alisema watu wa Syria wanastahiki kuwa na kipindi cha mpito cha amani kuelekea demokrasia, wanastahiki kuwa na serikali isiotesa , isiowakamata na isiowauwa. Hata hivyo, wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani imesema haijaweza kuhakikisha juu ya ripoti zinazosema kwamba manuwari za Syria ziliushambulia mji wa Latakia kwa mabomu.

Jana Jordan iliingia katika mkumbo wa nchi za Kiarabu zilizolaani ukandamizaji unaofanywa huko Syria dhidi ya wapinzani, na kuutaka utawala wa Damascus kusitisha mara moja michafuko hiyo, na usikilize sauti za busara.

Bingwa wa taaluma ya siasa katika Syria, Dr. Yasser Saad Aldin, alisema malalamiko ya kimataifa dhidi ya Syria yatazidi kuongezeka:

" Utawala wa Syria unazidharau lawama kutoka nje ya nchi, na inaungwa mkono tu na Iran. Jumapili mwanazuoni wa Iran walisema kumuunga mkono Rais Bashar al-Assad ni wajibu wa kidini. Jambo hilo ni la ajabu, kwamba chama tawala cha Baath ambacho kwa miaka 50 kimekuwa kisioelemea dini huko Syria kinaungwa mkono na serekali ya kidini ya Tehran! Hali yote  inaweza ikawa mzozo wa kidini."

Nalo shirika rasmi la habari la Syria limesema majeshi ya nchi hiyo yameondoka kutoka mji wa mashariki wa Deir al-Zor.

Mwandishi: Miraji Othman

Mhariri. Mohammed Abdulrahman