1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Malaysia: Waziri mkuu wa zamani ahojiwa kuhusiana na rushwa

Zainab Aziz
22 Mei 2018

Waziri Mkuu wa zamani wa Malaysia Najib Razak amehojiwa leo hii juu ya kashfa ya rushwa. Mkuu mpya ya kupambana na rushwa nchini humo amesema uchunguzi wa aina hiyo zamani haungeweza kufanyika. 

https://p.dw.com/p/2y64u
Malaysia Ex-Premier Najib Razak
Picha: Reuters/A. Perawongmetha

Kabla ya kuhojiwa, Najib Razak aliwahi kuitwa na Tume ya Kupambana na Rushwa ya Malaysia karibu wiki mbili zilizopita baada ya serikali yake ya mseto kushindwa kwenye uchaguzi wa taifa hilo uliofanyika tarehe 9 mwezi huu wa Mei. Matokeo ya uchaguzi huo kwa kiasi fulani yanachukuliwa kuwa ni adhabu kutoka kwa umma wenye hasira dhidi ya kiongozi huyo. Wapiga kura walimwangusha waziri huyo mkuu wa zamani wa Malaysia kutokana na kutoweka kwa fedha za mfuko wa uwekezaji ambao Najib aliuanzisha.

Najib daima amekuwa akikanusha kuhusika na wizi wa fedha hizo ambapo amesema amekasirishwa na mashambulizi mabaya ya kibinafsi dhidi yake.

Waziri mkuu wa zamani wa Malaysia Najib Razak
Waziri mkuu wa zamani wa Malaysia Najib RazakPicha: picture-alliance/AP Photo/V. Thian

Katika mahojiano ya leo maafisa walitaka kujua zaidi kwa nini kiasi cha ringgit milioni 42 sawa na dola milioni 10.6 zilihamishiwa kwenye akaunti ya benki ya Najib kutoka shirika la kimataifa la SRC, kitengo cha zamani cha mfuko aliouanzisha waziri huyo mkuu wa zamani wa 1MDB, kwa kutumia kampuni nyingi kama kiungo cha kati.

Fedha hizo zilikuwa ni pamoja na karibu dola milioni 700 ambazo wachunguzi wa Marekani wamesema ziliingia kwenye akaunti ya benki ya Najib. Wachunguzi hao wa Marekani wamesema washirika wa Najib waliiba kiasi cha dola bilioni $4.5 kutoka kwenye mfuko huo wa 1MDB kati ya mwaka 2009 na mwaka 2014, huku baadhi ya fedha hizo zikiwa zimeingizwa kwenye akaunti ya benki ya Najib.

Mkuu mpya wa tume ya kupambana na rushwa nynchini Malysia Mohd Shukri Abdull
Mkuu mpya wa tume ya kupambana na rushwa nynchini Malysia Mohd Shukri Abdull Picha: picture-alliance/AP Photo/V. Thian

Baada ya mahojiano hayo mkuu mpya wa tume ya kupambana na rushwa nchini Malaysia Mohamad Shukri Abdull aliwaambia waandishi habari kuwa mashtaka ya jinai dhidi ya Najib yanaweza kufunguliwa kwa haraka. Shukri aliongoza uchunguzi huo mnamo mwaka wa 2015, lakini alikimbilia Marekani muda mfupi baada ya mwanasheria mkuu wa Malaysia aliyepanga kufungua mashtaka dhidi ya Najib kufukuzwa kazi na Shukri mwenyewe alipata tetesi kuwa angekamatwa kwa madai ya kuwa na njama za kutaka kuipindua serikali.

Waziri huyo mkuu wa zamani na mke wake wamezuiwa kuondoka nchini Malaysia baada ya serikali mpya kuanzisha uchunguzi juu ya kashfa hiyo. Polisi walivamia na kufanya msako nyumbani kwa Najib na katika nyumba zake nyingine huku wakikamata mamia ya bidhaa za gharama kubwa kama mikoba na mafurushi yaliyojazwa fedha na vito vya thamani.

Mwandishi: Zainab Aziz/APE

Mhariri: Grace Patricia Kabogo