Malala Yousafzai azuru Pakistan baada ya miaka sita | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.03.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Pakistan

Malala Yousafzai azuru Pakistan baada ya miaka sita

Malala Yousafzai amerejea Pakistan miaka sita tangu aliposhambuliwa na wanamgambo wa Kitaliban. Yousafzai alikuwa na umri wa miaka 15 alipopigwa risasi kichwani na wapiganaji wa Taliban wakati alipokuwa anakwenda shule.

Mshindi huyo wa tuzo ya amani ya Nobel Malala Yousafzai amerejea nchini Pakistan ambayo ni nchi yake ya asili kwa mara ya kwanza tangu alipopigwa risasi na wapiganaji wa Taliban mnamo mwaka 2012. Wakati huo alipokuwa na umri wa miaka 15 Malala alilengwa na kundi la Taliban baada ya kuanzisha blogu iliyokuwa ikichapisha taarifa kuhusu maisha chini ya utawala wa Taliban.

Mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu cha Oxford cha  Uingereza aliwasili mjini Islamabad akiongozana na wazazi wake, ambako baadaye alikutana na Waziri Mkuu wa Pakistan Shahid Khaqan Abbasi. Afisa mmoja wa serikali amesema hata hivyo maelezo juu ya ziara ya Malala ya siku nne  yatakuwa ya siri kutokana na  hali ilivyo.

Wapakistani wengi wamefurahishwa na ziara hiyo, miongoni mwao ni mwanasheria Syed Raza Abidi, ambaye alimpokea msichana huyo shujaa na mwenye nguvu wa Pakistan alipowasili  nchini mwake.

Kulia: Malala Yousafzai (picture-alliance/ZumaPress)

Kulia: Malala Yousafzai

MalalaYousafzai alianza kuandika kwenye blogu ya idhaa ya Kiurdu ya BBC mwaka 2009, akiwa na umri wa miaka 11 tu. Mtetezi wa muda mrefu wa elimu kwa ajili ya wasichana, aliandika na kutoa mahojiano juu ya matatizo ya kupata elimu sahihi chini ya utawala wa ukandamizaji wa Wataliban katika bonde la Swat.

Mnamo Oktoba 9 mwaka 2012, watu waliokuwa wamejihami kwa bunduki walipanda basi la shule la akina Malala na kuanza kuuliza "Malala ni nani?" walipomtambua ndipo wakampiga risasi kichwani.

Alisafirishwa hadi Birmingham nchini Uingereza kwa ajili ya matibabu, na kisha baada ya kupona alibakia huko kwa ajili ya kuendelea na shule. Mwaka wa 2014, akawa mtu mwenye umri mdogo kabisa kupokea Tuzo ya Amani ya Nobel kutokana na kazi yake ya utetezi.

Malala Yousafzai (Getty Images/AFP/O. Andersen)

Malala Yousafzai

Yousafzai alishiriki katika kuandika kitabu bora kilichouza mno kuhusu uzoefu wake na hatimaye aliteuliwa kupokea tuzo ya kumbukumbu ya - Academy.

Licha ya umaarufu wake mkubwa, Malala pia ana wapinzani  wake nchini Pakistan. Kama mwandishi wa habari Huma Yusuf alivyowaelezea  kwa muhtasari wa wakosoaji wa Yousafzai, mwandishi huyo amesema "umaarufu wa Malala unaonyesha kipengele hasi nchini Pakistani (yaani kushamiri kwa makundi wapiganaji), ambapo kwa baadhi ya watu wanaonelea kuwa kampeni ya elimu ya binti huyo inendeleza ajenda ya nchi za Magharibi.

Mwandishi: Zainab Aziz/p.dw.com/p/2vA0c

Mhariri: Yusuf Saumu

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com