Makubaliano na Iran yatazuia mashindano ya silaha za nyuklia Mashariki ya Kati | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.07.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Makubaliano na Iran yatazuia mashindano ya silaha za nyuklia Mashariki ya Kati

Wakati Rais Barack Obama amesema makubaliano yaliyofikiwa na Iran maana yake ni kuzuia mashindano ya silaha za nyuklia katika Mashariki ya Kati, Waziri Mkuu wa Israel amesema makubaliano hayo ni makosa makubwa

Ujumbe wa Iran kwenye mazungumzo ya mjini Vienna

Ujumbe wa Iran kwenye mazungumzo ya mjini Vienna

Makubaliano baina ya Iran na mataifa makubwa duniani, juu ya mpango wa nyuklia wa nchi hiyo yatausimamisha kwa muda mpango huo,lakini haina maana kwamba Iran itaacha kabisa utafiti wa nyuklia na urutubishaji wa madini ya uran katika siku za usoni.

Kwa mujibu wa mapatano yaliyofikiwa jana ,Iran itausimamisha mpango wake wa kinyuklia kwa muda wa miaka 10. Wachunguzi wanasema baada ya kipindi hicho kumalizika Iran itaweza kuitumia mitambo ya kisasa kwa ajili ya kurutibishia madini ya uran.

Lakini Rais Barack Obama amesema makubaliano yaliyofikiwa jana yatazuia mashindano ya uundaji wa silaha za nyuklia katika Mashariki ya kati.

Netanyahu ayapinga makubaliano

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kuwa mapatano hayo ni makosa makubwa ya kihistoria.Bwana Netanyahu amesema Israel inao waasi wasi kwamba nchi ya kiislamu ya Iran itafunguliwa njia ya uhakika ya kuelekea kwenye silaha za nyuklia. Netanyahu ameeleza kuwa vikwazo vilivyowekwa vya kuizuia Iran kuunda silaha za nyuklia vitaondolewa, kutokana na makubaliano yaliyofikiwa.

Waziri Mkuu wa Israel Netanyahu amesema makubaliano yaliyofikiwa na Iran hayataleta usalama zaidi duniani.

Nchini Marekani wapinzani wa makubaliano yaliyofikiwa na Iran ikiwa pamoja na Spika wa Bunge John Boehner amesema huenda mapatano hayo yakachochea mashindano ya uundaji wa silaha za nyuklia duniani.Hata hivyo Bunge la Marekani ,linao muda wa siku 60 wa kuyadurusu maudhui ya mapatano.

Rais Obama anakabiliwa na changamoto kutoka kwa Republican wanaolidhibiti Bunge waliosema kwamba watayapinga makubaliano yaliyofikiwa na Iran.

Makubaliano hayo yalipokewa kwa shangwe kubwa katika mitaa ya miji ya nchini Iran, na Rais wa nchi hiyo Hassan Rouhani amesema Mwenyezi Mungu ameziitikia sala za watu wa Iran.

Umoja wa Ulaya na mfungamano wa kijeshi wa Nato pia unaunga mkono mapatano yaliyofikiwa mjini Vienna baina ya Iran na ,Marekani,Urusi,China, Uingereza,Ufaransa pamoja na Ujerumani. Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius amesema nchi yake haitasubiri kuanza kunufaika na fursa za kibiashara zinazotokana na makubaliano yaliyofikiwa na Iran.

Waziri wa fedha wa Uturuki Mehmet Simsek amesema hatua iliyofikiwa mjini Vienna jana itasaidia katika kuiweka bei ya mafuta katika kiwango cha chini na pia itaipunguza mivutano ya kikanda.

Mwandishi:Mtullya Abdu.rtre,afp

Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com