1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais John Magufuli wa Tanzania asema taifa  hilo si maskini

Angela Mdungu
1 Agosti 2019

Rais John Magufuli wa Tanzania amesema taifa  hilo siyo maskini na ataendelea kufanya maamuzi katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo bila kuwategemea wahisani

https://p.dw.com/p/3NBVL
John Magufuli Präsident Tansania
Picha: picture-alliance/AA/B. E. Gurun

Rais Magufuli ambaye leo amezindua jengo la tatu la abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere amesisitiza kwamba, Tanzania inapaswa kujiamulia mambo yake. Amesema wapo watu waliojaribu kuaminisha dunia kwamba Tanzania ni taifa maskini na hivyo haliwezi kufanya mambo yake bila kutegemea usaidizi.

Ameeleza, kudhihirisha kwamba Tanzania siyo maskini na iko tayari kujiamulia mambo yako, tayari inatekeleza miradi mikubwa ya kimaendeleo ikiwamo ujenzi wa reli ya kisasa(SGR), mradi wa kuzalisha umeme wa mto Rufiji yaani Stiagles Gorge pamoja na uamuzi wa serikali yake kuhamia Dodoma.

Ama, Rais Magufuli ametumia fursa hiyo kuelezea hali ya uchumi wa taifa akisema mwelekeo ni mzuri na kuitaja Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa machache barani afrika ambayo uchumi wake unakuwa kwa asilimia saba.

Awaonya watendaji wazembe

Pia, alionya kuhusu watendaji wazembe huku pia awanyoshea kidole wale aliowaita mafisadi. Amesema zama zao sasa zimekwisha na serikali imebana mianya yote waliyokuwa wakitumia kufuja fedha.

Einweihung des neuen Flughafen Terminals: Julius Nyerere International Airport  in Dar es salaam Tansania
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli akipiga Pusha up kabla ya uzinduzi wa jengo jipya la uwanja wa ndege wa JNIA jijini Dar es salaam Picha: DW/E. Boniphace

Kuhusu jengo hilo lililozinduliwa linatajwa kuwa la kisasa likiwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni sita kwa mwaka. Kwa maana hiyo kwa kuunganisha majengo yote matatu uwanja huo utakuwa na uwezo wa kuwahudumia abiria milioni nane kwa mwaka.

Uzinduzi huo umefanyika katika wakati ambapo shirika la ndege la Tanzania likipata uhai mpya kwa kupatiwa ndege nane wakati nyingine tatu zikitarajiwa kuwasili nchini mwezi disemba.

Uzinduzi wa jengo hilo huenda pia ukaongeza idadi ya watalii wanaokuja Tanzania hasa wakati huu ambapo vivutio vya utalii vikitangazwa zaidi, licha ya kuwa ni kivutio cha  mashirika  mengi  ya ndege  ya  kigeni kutua katika  uwanja  huo na kufanya shughuli  zao kwa njia  bora  zaidi.

Mwandishi: George Njogopa, DW, Dar Es Salaam