1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu ya Waislamu duniani kusherehekea Eid- ul Adha

8 Julai 2022

Maelfu ya Waislamu wamekusanyika siku ya Ijumaa kwenye mlima Arafa katika siku ya kilele cha ibada ya Hijja ambayo kwa miaka mwili iliyopita ilihudhuriwa na idadi ndogo ya waumini kutokana na janga la virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/4Drh3
Saudi-Arabien | Mekka Hadsch
Picha: Ashraf Amra/AA/picture alliance

Makundi ya mahujaji wengi wakiwa na miavuli ya kujikinga na jua walisoma aya za Quran tukufu kwenye eneo hilo la mlima ambako inaaminika mtume Muhammad alitoa hotuba ya mwisho kabla ya kifo chake.

Waislamu wanaamini ibada inayofanywa kwenye mlima Arafa uliopo kiasi kilometa 20 mashariki mwa mji mtakatifu wa Makka ni nafasi adhimu ya kupata msamaha kutoka Mwenyezi Mungu.

Siku ya Jumamosi (09.07.2022) Mahujaji watashiriki ibada ya ishara ya kumpiga mawe shetani huku mamilioni wengine duniani wakisherehekea sikukuu ya Eid al-Adhaa kuashiria kumalizaka kwa ibada ya Hijja ambayo ni miongoni mwa nguzo tano za dini ya kiislamu.

Mjini Mombasa, raia walia na kupanda gharama za maisha

Sherehe za Eid- ul Adha zimepamba moto mjini Mombasa nchini Kenya licha ya mfumko wa bei za bidhaa za msingi. Wafanyibiashara wanalalamika kupungua kwa wateja wao huku wananchi nao wakipunguza manunuzi ya bidhaa.

Mapema siku ya Ijumaa halaiki ya waumini wa Kiislamu Mombasa walifurika kwenye maduka ya nguo, vyakula na sokoni kwa maandalizi ya dakika za mwisho ya sherehe ya Eid- ul Adha inayotarajiwa kuadhimishwa hapo Jumamosi.

BG Hadsch Saudi-Arabien
Mahujaji wakiwa mjini MeccaPicha: Ashraf Amra/Zumapress/picture alliance

Maeneo ya biashara ya Marikiti, Mwembe Kuku, Mwembe Tayari na Maduka makuu ndiyo yaliyowavutia wateja wengi kiasi cha kusababisha msongamano wa watu…

Wateja wengi hata hivyo wanalalamika kupanda kwa bei za bidhaa na wamewahimiza wenye biashara wapunguze bei za bidhaa zao kwasababu wananchi wameumia kimaisha. Aisha Mahmood mkazi wa majengo Mombasa anasema nguo zimepanda pia sawa tu na chakula kilivyopanda.

Abdisheikh Mbarak muuzaji mbuzi katika soko la Kikowani,  ameieleza DW kuwa wateja wao wa kununua mbuzi wamepungua japo kwa kiasi kidogo mwaka huu ikilinganishwa na eid ya mwaka 2021kutokana na gharama kubwa ya maisha iliyosababisha kupanda kwa bei ya mbuzi.

Hata hivyo baadhi ya wateja wa mbuzi wananunua idadi ndogo ya mifugo hao kulingana na uwezo walionao kwa sasa. Abdalla Juma kutoka Bombolulu ni mmoja wao, amenunua mbuzi wanne pekee idadi ambayo anasema kuwa ni ndogo sana kwa familia yake lakini hana budi. Sikukuu ya Eid ul-Adha huadhimishwa kuanzia siku ya 10 tangu kuonekana kwa mwezi wa Dhul Hijjah.