1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabadiliko Urusi yanuia kuongeza muda wa Putin madarakani

16 Januari 2020

Rais Vladimir Putin amefanya mabadiliko ya ghafla katika uongozi wa Urusi ambapo amependekeza mabadiliko katika katiba ya nchi hiyo ambayo huenda yakamuweka mamlakani kupindukia mwisho wa muhula wake wa mwaka 2024.

https://p.dw.com/p/3WH9c
Russland Moskau | Wladimir Putin, Präsident | Rede zur Lage der Nation
Picha: picture-alliance/Russian Look/Kremlin

Katika mapendekezo hayo ya katiba aliyoyatangaza katika hotuba yake kwa taifa, rais Putin ameashiria kwamba anataka kubuni nafasi ya uongozi kwake binafsi baada ya kukamilika kwa muhula wake ingawa mabadiliko hayo aliyoyapendekeza hayasemi hasa ni mwelekeo gani atakaochukua ili kusalia kwenye uongozi.

Masaa machache baada ya kupendekeza mabadiliko hayo Waziri Mkuu Dmitry Medvedev alijiuzulu na Putin akamtaja mkuu wa mamlaka ya ushuru nchini humo Mikhail Mishustin kama mtu atakayeichukua nafasi ya Medvedev kama waziri mkuu. Mishustin si maarufu nchini Urusi katika ulingo wa kisiasa.

Medvedev kusalia kushikilia nafasi ya waziri mkuu kwa muda

Lakini Putin amemuweka Medvedev ambaye ni rafiki yake wa zamani katika uongozi wa Kremlin kwa kumteua katika nafasi mpya ya mkuu wa baraza la usalama la rais ingawa ushawishi na majukumu yanayotokana na kuishikilia nafasi hiyo hayajajulikana.

Russland Mikhail Mishustin und Dimitry Medwedew
Mkihail Mishustin (kushoto) akiwa na Dmitry Medvedev (kulia)Picha: picture-alliance/AP Photo/Y. Shtukina

Medvedev alikuwa na haya kusema baada ya kujiuzulu.

"Bila shaka nawashukuru wote walioshiriki katika kazi ya serikali na maamuzi ya siku zijazo sasa yatafanywa na rais," alisema Medvedev.

Lakini anasalia kuishikilia nafasi hiyo ya waziri mkuu kwa sasa hadi pale Mishustin atakapochukua uongozi rasmi.

Wabunge wa Urusi watamkagua Mishustin kama iwapo anastahili kushikilia wadhfa huo ingawa inatarajiwa wamuidhinishe kwa kuwa sehemu kubwa ya bunge nchini humo ni tiifu kwa utawala wa rais Putin.

Lengo ni Putin kusalia kuwa mwanasiasa muhimu zaidi Urusi

Putin mwenye umri wa miaka sitini na saba na ambaye ameiongoza Urusi kwa zaidi ya miaka ishirini, kawaida huwa msiri katika yale anayonuia kufanya hadi katika dakika ya mwisho. Haibainiki pia iwapo Mishustin ameteuliwa katika nafasi hiyo ya waziri mkuu kwa muda mfupi tu au anaweza kupigwa msasa ili awe mrithi wa rais Putin.

Russland Moskau | Alexei Nawalny, Oppositionspolitiker
Kiongozi wa upinzani Urusi Alexei NavalnyPicha: Getty Images/AFP/Y. Kadobnov

Maria Lipman ni mchambuzi huru wa masuala ya Urusi.

"Lengo bila shaka halifichiki. Lengo ni mfumo wa uongozi usalie imara na Putin ashikilie uongozi na asalie yule yule ambaye amekuwa katika miaka ishirini ambayo imepita, yani asalie mwanasiasa muhimu zaidi nchini, mtu anayefanya uamuzi wa mwisho na kiongozi ambaye hawezi kupingwa," alisema Lipman.

Kiongozi maarufu wa upinzani nchini Urusi Alexei Navalny ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba lengo la Putin ni kuifanya nchi nzima ya Urusi kama mali yake na kujilimbikizia utajiri wa nchi hiyo yeye na marafiki zake.