Maafisa wa fedha duniani kuchukua hatua za kuukuza uchumi | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.10.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Maafisa wa fedha duniani kuchukua hatua za kuukuza uchumi

Maafisa wa fedha kutoka nchi zenye nguvu zaidi kiuchumi duniani wanahimimizwa kuchukua hatua madhubuti kuepusha uchumi wa dunia usitumbukie katika mkwamo mpya ambapo ukuaji wa uchumi umesalia katika kiwango cha kudumaa

Mawaziri wa fedha na magavana wa benki kuu za kundi la nchi ishirini zenye nguvu zaidi kiuchumi duniani ambazo ni pamoja na miamba wa uchumi wa tangu jadi Marekani, Ujerumani na Japan pamoja na nchi zinazoinukia kwa kasi kiuchumi kama Urusi na China wanakamilisha misururu ya mazungumzo ya siku mbili hii leo mjini Washington, Marekani huku wakitoa taarifa ya pamoja kuhusu malengo na kutarajiwa kuhutubia wanahabari baadaye leo.

Mikutano hiyo inakuja wakati kuna taarifa kutoka barani Ulaya kuwa hali ya kiuchumi ya nchi wanachama kumi na nane zinazotumia sarafu ya euro sio ya kutia moyo na huenda kuna hatari ya kushuhudia msukosuko mwingine wa kiuchumi katika kanda hiyo.

Ujerumani yapata hasara

Ujerumani hapo jana iliripoti mauzo yake ya nje yameshuhudia anguko kubwa zaidi katika kipindi cha miaka mitano mwezi Agosti, kufuatia kupungua kwa kiasi kikubwa cha mahitaji kutoka kwa washirika muhimu wa kibiashara wa taifa hilo katika kanda ya sarafu ya euro.

Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble

Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble

Australia ambayo ni mwenyeji wa mkutano wa kundi la nchi ishirini zenye nguvu zaidi za kiuchumi duniani mwaka huu inataka kupitishwa kwa mpango makhususi wa kuchukuliwa hatua ambazo zitaweka malengo ya kuuchochea uchumi wa dunia kwa angalau asilimia mbili katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Makadirio hayo ya ukuaji yanamaanisha kutahitajika kuongezeka kwa uzalishaji wa kiviwanda wa kiasi cha dola trilioni mbili ili kuliafikia lengo hilo katika kipindi hicho cha miaka mitano ijayo.

Baada ya kuidhinishwa na maafisa wakuu wa fedha, mpango huo wa kufufua uchumi utawasilishwa kwa Rais wa Marekani Barack Obama na viongozi wengine wa nchi za G 20 kutiwa saini katika mkutano wa kilele unaotarajiwa katikati ya mwezi ujao mjini Brisbane, Australia.

Vitisho kadha wa kadha vikwazo

Maafisa wa kiuchumi wamesema kuongeza matumizi ya fedha kwa ajili ya barabara, viwanja vya ndege an miundo mbinu mingine hakutatosha kuuinua uchumi wa dunia hadi kiwango thabiti hasa kutokana na kuongezeka kwa vitisho dhidi ya ukuaji wa uchumi kutoka kanda mbalimbali duniani.

Mkuu wa shirika la fedha duniani IMF Chrstine Lagarde

Mkuu wa shirika la fedha duniani IMF Chrstine Lagarde

Uchumi wa dunia unakabiliwa na vitisho mbali mbali vikiwemo mzozo wa Ukraine, kitisho cha kuongezeka kwa uasi unaoenezwa na makundi ya wanamgambo wenye itikadi kali kama linalojiita dola la kiislamu IS nchini Iraq na Syria na kuzuka kwa ugonjwa wa Ebola magharibi mwa Afrika.

Majadiliano hayo ya G20 yanafanywa kabla ya mikutano ya kila mwaka ya nchi wanachama 188 wa shirika la fedha duniani IMF na benki ya dunia.

Mwandishi:Caro Robi/ap

Mhariri:Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com